Oct 06, 2016 01:03 UTC
  • Alkhamisi Oktoba 6 2016

Leo ni Alkhamisi tarehe 4 Muharram 1438 Hijria sawa na Oktoba 6, 2016.

Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, Anwar Sadat Rais wa wakati huo wa Misri aliuawa na maafisa kadhaa wa kundi moja la wanamapambano wa Kiislamu wa Misri lililojulikana kwa jina la al Jihad. Sadat aliuawa kwa sababu ya kutia saini makubaliano maovu ya Camp David mwaka 1978 na utawala wa Kizayuni wa Israel na akatambua rasmi utawala huo ghasibu na haramu. Kwa kitendo hicho Anwar Sadat alisaliti malengo ya Waislamu na Waarabu. Hatua hiyo ya Anwar Sadat ilipelekea kutengwa Misri miongoni mwa nchi za Kiislamu. Sababu hiyo iliyapelekea makundi ya Waislamu na wanamapambano wa Misri kumuuwa Sadat, ambaye walimuona kuwa ni msaliti mkubwa kwa kuutambua rasmi utawala wa maghasibu wanaoikalia kwa mabavu Palestina na kibla cha kwanza cha Waislamo wote duniani. Kiongozi wa mauaji hayo alikuwa Khalid Islambuli, aliyekuwa afisa katika jeshi la Misri.

Siku kama ya leo, miaka 1377 iliyopita, Ubaidullah bin Ziyad, mtawala dhalimu na fasiki wa mji wa Kufa, Iraq alitoa hotuba katika msikiti wa mji huo. Katika hotuba hiyo, Ibn Ziyad alitoa vitisho vikali dhidi ya wafuasi wa Imam Hussein (as), mjukuu wa Bwana Mtume Muhammad (swa) akiwataka kutomsaidia mtukufu huyo katika ardhi ya Karbala na kwamba angemuua mtu yeyote ambaye angefanya hivyo. Kwa kutumia fatwa ya hila iliyotolewa na Shuraihul-Qadhi ya kuhalalisha damu ya Imam Hussein (as), Ibn Ziyad akafunga njia zote za kuingia na kutoka mji wa Kufa huku akitoa fedha kwa wakazi wa mji huo kwa ajili ya kwenda kupambana na mjukuu huyo wa Mtume huko Karbala tukio lililomalizika kwa kuuawa Imam Hussein na watu wa familia ya Mtume (swa).

Siku kama ya leo miaka 953 iliyopita, alifariki dunia Abul-Qasim Muhammad Baghdadi, maarufu kwa jina la Ibn Naqiya, malenga, mwandishi na fasihi mkubwa wa mjini Baghdad, Iraq. Umahiri aliokuwa nao Ibn Naqiya, ndio uliofanya kuwa mashuhuri ambapo hata wataalamu wa mashairi waliyatumia mashairi yake. Kitabu cha ‘Maqaamaat’ ni moja ya athari zinazonasibishwa kwa malenga huyo. Katika kitabu hicho Ibn Naqiya, alizungumzia maovu ya kijamii kupitia hekaya na tenzi. Athari nyingine inayonasibishwa kwa msomi huyo wa Kiislamu, ni kitabu kinachoitwa ‘Al-Jamaan fi Tashbiihaatil-Qur’an’ ambayo ni tafsiri nyepesi ya Qur’an Tukufu. Katika tafsiri hiyo Ibn Naqiya amefafanua aya 226.

Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita, vita vya nne kati ya Waarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel vilianza. Katika siku hiyo, jeshi la Misri lilifanya mashambulio ya kushtukiza dhidi ya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel unaoikalia kwa mabavu Quds tukufu huko katika mfereji wa Suez na kufanikiwa kuingia katika jangwa la Sinai baada ya kuvunja kikosi cha ulinzi cha mstari wa mbele cha utawala wa Kizayuni. Vikosi vya Misri na Syria vililisababishia hasara kubwa jeshi la Israel katika vita hivyo ambapo ndege nyingi za utawala wa Kizayuni ziliangamizwa.