Jumamosi, Agosti 8, 2016
Leo ni Jumamosi tarehe 6 Mfunguo Nne Muharram 1438 Hijria mwafaka na tarehe 8 Oktoba mwaka 2016 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 11 iliyopita mtetemeko mkubwa wa ardhi uliokuwa na ukubwa wa 7.8 kwa kipimo cha rishta uliyakumba maeneo ya kaskazini mashariki mwa Pakistan. Kitovu cha mtetemeko huo kilikuwa katika mji wa Muzaffarabad. Watu karibu 90,000 walipoteza maisha yao na wengine 3,300,000 kubaki bila makazi. ***
Katika siku kama ya leo miaka 105 iliyopita, vita vya Balkan vilianza kwa ushiriki wa Bulgaria, Serbia na Ugiriki dhidi ya Utawala wa Othmania. Ufalme wa Othmania kwa miaka kadhaa mtawalia ulikuwa umefanikiwa kuyafanya maeneo mengi ya magharibi mwa Asia, kaskazini mwa Afrika na mashariki mwa Ulaya kuwa chini ya udhibiti wake na hivyo ukawa umetanua utawala wake. Vuguvugu la kulitaka kujitenga nchi zilizokuwa chini ya utawala huo lilikuwa likipelekea kutokea vurugu mara kwa mara na vita vya Balkan ni moja ya harakati hizo.***
Miaka 1032 iliyopita katika siku kama ya leo kulingana na kalenda ya Hijria aliaga dunia Sayyid Muhammad Hussein Musawi Baghdadi mashuhuri kwa jina la Sayyid Radhi msomi, alimu na mshairi mkubwa wa Kiislamu. Alisoma kwa wanazuoni mahiri kama Sheikh Mufid. Sayyid Radhi alianza kutunga mashairi tangu katika kipindi cha ujana. Mwanazuoni huyo mahiri ameandika vitabu vingi, lakini Kitabu cha Nahaj al-Balagha kilichokusanya, barua, hotuba na nasaha za Imam Ali AS ndicho kilichompatia umashuhuri zaidi msomi huyo. ***
Siku kama ya leo miaka 1377 iliyopita yaani tarehe 6 Mfunguo Nne Muharram mwaka 61 Hijria, Imam Hussein AS alimuandikia barua fupi na muhimu kaka yake yaani Muhammad bin Hanafia pamoja na kundi la wafuasi wake mjini Madina. Barua hiyo ilisema: Bismillahir Rahmanir Rahim. "Kila atakayeungana na mimi atauawa shahidi na ambaye hatofanya hivyo hatoufikia ushindi." Barua hii fupi ya Imam Hussein ilikuwa na jumbe kadhaa. Mosi, iliweka wazi na kubainisha kwamba, kuuawa shahidi Imam huyo na masahaba zake ni jambo lisilo na shaka. Pili, ilibainisha kwamba, watu wote watauawa shahidi hivyo kama kuna mtu ameungana naye kwa lengo jingine basi hajachalewa kubadilisha msimamo wake na kurudi nyuma. ***