Jumapili, Oktoba 9, 2016
Leo ni Jumapili tarehe 7 Muharram 1438 Hijria, sawa na Oktoba 9 mwaka 2016 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1377 iliyopita, Omar Bin Saad, alitoa amri ya kuuzuia msafara wa Imam Hussein (as), mjukuu wa Bwana Mtume Muhammad (saw) kutumia kwa aina yoyote maji ya mto wa Furati (Euphrates.) Baada ya Ubaidullah Bin Ziyad, kutuma jeshi kubwa kwa ajili ya kupambana na mjukuu huyo wa Mtume, alituma barua kwa Ibn Saad ili kumzingira Imam Hussein na masahaba zake. Katika ujumbe huo, Bin Ziyad alimtaka Omar Bin Saad kumwamuru Al-Imamul-Hussein kumbai Yazid mwana wa Muawiya. Aidha sehemu nyingine ya barua hiyo ilimtaka kamanda huyo wa jeshi katili kumtenga mjukuu huyo wa Nabii wa Allah na maji ya Mto Furati na asimruhusu kamwe kuweza kuyanywa yeye au vamilia yake. Bila kuchelewa Ibn Saad aliwaamuru askari 500 wapanda farasi kumzuia Imam Hussein na maji ya mto huo. Kitendo hicho cha kikatili, kilijiri ikiwa ni siku tatu kabla ya kuuawa shahidi Imam Huusein (as). Hata hivyo Abul-fadhlil-Abbas alifanya juhudi kubwa kwa ajili ya kuwaletea maji watu wa msafara huo ingawa hata hivyo askari wale katili walimzuia na kumuua kinyama mtukufu huyo. Hadi asubuhi ya siku ya tisa ya mwezi huu wa Muharram, hakukuwa na tone la maji lililokuwa limesalia kwa wafuasi wa mjukuu huyo wa Mtume (Imam Hussein) suala ambalo liliwafanya watukufu hao kuvumilia tabu ya kiu kali kutokana na joto kali lililokuwepo eneo hilo.

Siku kama ya leo miaka 125 iliyopita, alizaliwa Sayyid Mohammad Hadi Milani, marjaa mkubwa wa Waislamu wa Shia. Ayatullahil-Udhma Sayyid Mohammad Hadi Milani alizaliwa tarehe saba mwezi Muharram mwaka 1313 Hijiria Qamaria huko mjini Najaf, Iraq. Alianza kusoma elimu ya dini akiwa na umri mdogo ikiwa ni pamoja na kujifunza Qur'ani Tukufu mjini hapo. Baada ya hapo alijifunza fasihi ya lugha ya Kifarsi na Kiarabu huku akiandika pia vitabu vingi. Aidha kando na shughuli hiyo alikuwa akifundisha idadi kubwa ya wanafunzi elimu ya hawza ya kidini na kufikia daraja ya umarjaa. Msomi huyo alitambulika kwa uchaji-Mungu, taqwa, na tabia njema ya hali ya juu. Kitabu cha 'Muhaadharat fii Fiqhil-Imaamiyyah' ni miongoni mwa athari za msomi huyo.
Siku kama ya leo miaka 49 iliyopita, aliuawa Ernesto Che Guevara mwanamapinduzi mashuhuri wa Amerika ya Latini pamoja na wenzake kadhaa. Che Guevara alizaliwa mwaka 1928 nchini Argentina. Fikra ya Ernesto Che Guevara ya kuendesha mapambano dhidi ya ubepari ilizidi kupanuka baada ya kushuhudiwa umaskini na ubaguzi uliotokana na siasa za kipebari za Marekani za kuyanyonya mataifa ya Amerika ya Latini. Ernesto che Guevara alifahamiana na Fidel Castro wa Cuba huko Mexico na viongozi hao wawili ndio walioongoza mapinduzi ya Cuba hadi kupatikana ushindi. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Cuba mwaka 1959, Che Guevara alielekea Bolivia na kuasisi kundi la wapiganaji wa msituni. Alianza kupambana na serikali ya nchi hiyo iliyokuwa tegemezi kwa Marekani. Lakini katika siku kama ya leo mwaka 1967, wanajeshi wa Bolivia wakisaidiwa na shirika la ujasusi la CIA waligundua maficho ya Che Guevara na kumuuwa kwa kummiminia risasi.
Siku kama ya leo miaka 54 iliyopita, mwafaka na tarehe 9 Oktoba 1962, nchi ya Uganda ilijipatia uhuru wake kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Kuanzia mwaka 1890 Uganda ilikuwa nchini ya makampuni ya Kiingereza yaliyokuwepo Afrika Mashariki, na baada ya kupita miaka kadhaa, ikatawaliwa rasmi na Uingereza. Baada ya kutawaliwa na mkoloni Mwingereza, wananchi wa Uganda walipigania uhuru na hatimaye kufanikiwa kujipatia uhuru wao mwaka 1962 katika siku kama ya leo.

Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, Majid Abu Sharar, shakhsia mwingine wa Palestina aliuawa na utawala haramu wa Israel huko nchini Italia. Abu Sharar ambaye alikuwa afisa wa kampeni ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO aliuawa na vibaraka wa shirika la ujasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel Mosad mjini Roma, Italia. Israel imekuwa ikitumia njia ya kuwauwa kigaidi shakhsiya mbalimbali wa Palestina kama moja ya njia zake kuu za kusitisha mapambano ya ukombozi ya Wapalestina.