Jumanne, Agosti 11, 2016
Leo ni Jumanne tarehe 9 Mfunguo Nne Muharram 1438 Hijria sawa na 11 Oktoba 2016.
Katika siku kama ya leo miaka 1377 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, katika hali ambayo, majeshi ya Yazid yalikuwa yamejiandaa kikamilifu kumshambulia Imam Hussein AS na masahaba zake katika ardhi ya Karbala, Imam alimtuma ndugu yake aliyesifika kwa ushujaa mkubwa yaani Abul Fadhl Abbas akawaombe maadui hao wampe fursa aupitishe usiku huo kwa Swala na kunong'ona na Mola wake. Usiku huo Imam Hussein aliwakusanya wafuasi wake na baada ya kumhimidi Mwenyezi Mungu na kumsalia Mtume, aliwaambia: ''Kila anayetaka, aitumie fursa iliyobakia ya giza la usiku kwa ajili ya kuyanusuru maisha yake, kwani hakuna atakayebaki hai hapo kesho tutakapokabiliana na jeshi la Yazid.'' Hata hivyo masahaba na wafuasi waaminifu na waumini wa kweli wa mtukufu huyo walikuwa wameshakata shauri la kujitolea mhanga kwa ajili ya Mwenyezi Mungu hadi tone la mwisho la damu zao. Usiku huo wa kuamkia Ashuraa yaani tarehe 10 Muharram, uwanja wa Karbala ulikuwa medani ya ibada kwa mashujaa ambao licha ya kuwa wachache kwa idadi lakini walisimama imara kama mlima na hawakumuacha Imam na kiongozi wao hata dakika moja.
Leo tarehe 20 mwezi wa Mehri kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, inasadifiana na maadhimisho ya Khaja Shamsuddin Muhammad Hafiz Shirazi, mshairi na malenga mkubwa wa Kiirani. Hafiz alizaliwa mwaka 727 Hijiria Shamsia mjini Shiraz moja ya miji ya kusini mwa Iran. Alikuwa mtaalamu katika Tafsiri ya Qur'an, falsafa na fasihi ya Kiarabu na alipata umashuhuri kwa jina la Hafiz kutokana na kuhifadhi kwake Qur'an Tukufu kwa visomo tofauti. Mbali na elimu hizo, Khaja Shamsuddin Muhammad Hafiz, alikuwa mtaalamu mkubwa wa elimu ya Irfan.
Siku kama ya leo miaka 117 iliyopita, vita vya umwagaji damu kati ya wazungu wa Kiholanzi kwa jina la Boers wakazi wa Afrika Kusini na Waingereza vilianza. Wanajeshi wa Uingereza waliwasili Afrika Kusini mwaka 1841 lengo likiwa ni kuikoloni Afrika. Waingereza walidhibiti Afrika Kusini baada ya kujenga maeneo ya kiraia nchini humo. Wahamiaji wengine kutoka Ulaya hususan Waingereza walimiminika huko Afrika Kusini baada ya kugunduliwa madini ya dhahabu na Almasi. Wazungu wa Uholanzi yaani Maboers waliwasili Afrika Kusini katika karne ya 19 na kupinga kuwasili wahamiaji wapya nchini humo. Sababu hiyo ilipelekea kuanza vita kati ya Wazungu hao na wahamiaji wa Kiingereza, lakini uungaji mkono wa serikali ya Uingereza kwa wahamiaji hao, ulitoa pigo kwa Maboers na kwa msingi huo Afrika Kusini ikaloloniwa na Uingereza.
Siku kama ya leo miaka 101 iliyopita alifariki dunia Jean Henri Fabre msomi wa elimu ya sayansi na bingwa wa elimu ya wadudu au entomolojia. Fabre alizaliwa mwaka 1823 nchini Ufaransa. Msomi huyo ambaye pia alikuwa mwandishi amefanya utafiti mkubwa na kuandika vitabu kadhaa kwenye uwanja wa elimu ya wadudu.
Siku kama ya leo miaka 25 iliyopita yaani sawa na tarehe 11 Oktoba mwaka 1991 Miladia, shughuli za Shirika la Ujasusi la Urusi ya zamani (KGB) zilifikia kikomo muda mfupi baada ya kusambaratika nchi hiyo. KGB iliundwa mwaka 1954 kwa lengo la kukabiliana na harakati zilizokuwa na lengo la kuuangusha mfumo wa Kikomonisti wa Urusi ya zamani. Shirika hilo aidha lilikuwa na majukumu kama vile kuwakandamiza wapinzani wa chama cha Kikomonisti na kuendesha operesheni za kijasusi na zile zilizo dhidi ya ujasusi ndani na nje ya Muungano wa Kisovieti.