Ijumaa Oktoba 14
Leo ni Ijumaa tarehe 12 Muharram 1438 Hijria sawa na 14 Oktoba 2016.
Tarehe 12 Muharram mwaka 61 yaani siku kama hii ya leo miaka 1377 iliyopita msafara wa mateka uliokuwa na wanawake na watoto wa mashahidi wa Karbala, uliwasili katika mji wa Kufa, nchini Iraq.
Kiongozi wa msafara huo alikuwa Bibi Zainab (as) dada wa Imam Hussein bin Ali (as) pamoja na Imam Ali bin Hussein Sajjad (as), mtoto wa Imam Hussein (as). Imam Sajjad na Bibi Zainab (as) walifichua dhulma na jinai zilizofanya na utawala wa Yazid bin Muawiya na kutekeleza vyema majukumu yao kwa kufikisha ujumbe wa Imam Hussein kwa jamii ya Waislamu licha ya mashaka na masaibu mengi waliyokumbana. Katika siku hii ya tarehe 12 Muharram mwaka 61 Hijria pia miili ya mashahidi wa Karbala ukiwemo mwili mtoharifu wa mjukuu wa Mtume Imam Hussein (as) na watu wengine wa familia yake ilizikwa na watu wa kabila la Bani Asad, siku mbili baada ya kubakia katika jangwa la Kabala bila ya kuzikwa. Watu waliogopa kuzika mwili wa mjukuu wa Mtume (saw) ndugu na masahaba 72 waliouawa siku ya Ashura kwa muda wa siku mbili kwa kuogopa kufuatiliwa na kuuawa na utawala dhalimu wa Yazid.
Siku kama ya leo miaka 1343 iliyopita, kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi ya historia, Imam Ali Zainul Abidin maarufu kwa lakabu ya Sajjad mwana wa Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) na mmoja wa wajukuu wa Mtume Mtukufu S.A.W, aliuawa shahidi. Imam Zainul Abidin alizaliwa mwaka 38 Hijria huko katika mji wa Madina. Mtukufu huyo aliishi katika zama ambapo watu wa Nyumba ya Mtume Mtukufu walikuwa wakikabiliwa na masaibu mengi. Imam Sajjad A.S ambaye alikuwa mgonjwa wakati wa tukio la Karbala, baada ya harakati adhimu ya Imam Hussein, alibeba jukumu kubwa la kueneza ujumbe wa mapambano hayo na kuendeleza njia ya baba yake.
Siku kama ya leo miaka 17 iliyopita alifariki dunia kiongozi wa zamani wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Nyerere Alizaliwa mjini Butiama mkoani Mara mwaka 1922. Mwaka 1955 aliingia katika ulingo wa siasa akiongoza chama cha Tanganyika Africa Nation Union (TANU). Mwaka 1961 Nyerere alikuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika na mwaka mmoja baadaye akawa Rais wa nchi hiyo. Kutokana na juhudi zake mwaka 1964 ziliungana Tanganyika na Zanzibar na kuunda nchi moja ya Tanzania. Nyerere aliendelea kuongoza nchi hiyo hadi mwaka 1985 ambapo aliachia hatamu za uongozi. Hata hivyo Nyerere aliendelea kuwa na ushawishi mkubwa katika siasa za Tanzania hadi alipofariki dunia.
Tarehe 14 Oktoba miaka 72 iliyopita Erwin Rommel kamanda maarufu wa jeshi la Manazi wa Ujurumani aliyejulikana kwa lakabu ya 'Mbweha wa Jangwani' alijiua kwa amri ya dikteta Adolph Hitler. Katika Vita Vya Pili vya Dunia, Erwin Rommel alikuwa kiongozi wa jeshi la Ujerumani huko kaskazini mwa Afrika na aliweza kulishinda jeshi la Uingereza na kulirejesha nyuma hadi kaskazini mwa Misri suala lililopelekea kupandishwa cheo na kuwa Field Marshall. Mwaka 1944 Field Marshall Rommel alikuwa kamanda wa jeshi la Ujerumani huko Italia na Balkan hata hivyo alihitilafiana na Hitler juu ya namna ya kuendesha vita katika maeneo hayo.
Na siku kama ya leo miaka 63 iliyopita Wazayuni wa Israel walivamia kijiji cha Qibya kilichoko katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kufanya jinai kubwa za kutisha. Katika mashambulizi na uvamizi ulioendelea katika kijiji hicho kwa muda wa siku mbili, Wazayuni walitekeleza mauaji na ukatili mkubwa dhidi ya raia wa Kipalestina wasio na hatia. Mbali na Wazayuni hao kuwaua na kuwajeruhi kwa umati raia wa Kipalestina zaidi ya 42, askari wa Israel waliokuwa wakiongozwa na waziri mkuu wa zamani wa Israel, Ariel Sharon, walibomoa makumi ya nyumba na shule za kijiji hicho. Mauaji hayo ya halaiki ni miongoni mwa mifano ya ugaidi wa utawala ghasibu wa Israel hususan waziri mkuu wa zamani wa utawala huo, Ariel Sharon.