Oct 16, 2016 03:08 UTC
  • Jumapili, Oktoba 16, 2016

Leo ni Jumapili tarehe 14 Muharram mwaka 1438 Hijria, sawa na tarehe 16 Oktoba mwaka 2016 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 223 iliyopita, yaani tarehe 16 Oktoba mwaka 1793, alinyongwa kwa kukatwa kichwa na shoka, malikia wa Ufaransa Marie Antoinette kupitia amri ya baraza la katiba la nchi hiyo na pia amri ya Maximilien Robespierre. Louis wa 16 alikuwa mume wa  Antoinette ambaye naye miezi 10 kabla ya hapo alikumbwa na hatma hiyo hiyo iliyomkuta mke wake. Marie Antoinette, alikuwa binti wa Maria Theresa Walburga, mtawala wa Austria na Ufaransa. Antoinette aliolewa na Louis, mrithi wa kiti cha ufalme wa Ufaransa, mnamo mwaka 1770 Miladia akiwa na umri wa miaka 14. Hatua ya Louis ya kumuoa mwanamke huyo ilikuwa ni kujaribu kuzikurubisha pamoja nchi za Austria na Ufaransa ambazo wakati huo zilikuwa zikishindana barani Ulaya. Hata hivyo Wafaransa wengi hawakuridhia ndoa hiyo kiasi cha kuwafanya kuendelea kumwita kwa lakabu ya ‘Muaustria’ hata kipindi alipokuwa tayari ni malikia wa Ufaransa.

Marie Antoinette

Siku kama ya leo miaka 71 iliyopita liliasisiwa Shirika la Chakula Duniani (FAO). Hati ya kuasisiwa shirika hilo ilipasishwa Oktoba 16 mwaka 1945 katika mji wa Québec nchini Canada. Lengo la kuasisiwa shirika la FAO ni kuzisaidia nchi wanachama kukusanya taarifa, ripoti na takwimu zinazohusiana na chakula, kilimo, utunzaji wa misitu na uvuvi na kufanya tathmini kuhusu uzalishaji wa chakula, ugavi wake na juhudi za kuboresha uzalishaji, masoko ya chakula, kulinda maliasili, kupanga sera zinazohusiana na kilimo na chakula na kadhalika. Siku hii pia inatambuliwa kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Chakula.

Shirika la Chakula Duniani

 

Siku kama ya leo miaka 201 iliyopita, kipindi cha pili cha kubaidishwa Napoleon Bonaparte, mfalme aliyeshindwa wa Ufaransa, kilianza kwa yeye kufika katika kisiwa cha Saint Helena. Napoleon ambaye awali alitaka kudhibiti dunia nzima, baada ya kutwaa eneo pana la Ulaya, hatimaye alishindwa katika vita vikali na Waingereza na kisha kubaidishwa katika kisiwa hicho. Napoleon alifariki dunia mwaka 1821 akiwa kizuizini.

Napoleon Bonaparte

Siku kama ya leo miaka 175 iliyopita, alifariki dunia mjini Isfahan, moja ya miji maarufu ya Iran, Sayyid Sadrud-Din Musawi Amili, msomi na mtaalamu wa hadithi wa Kiislamu. Sayyid Sadrud-Din Musawi Amili alizaliwa katika moja ya viunga vya mji wa Jabal Amel, nchini Lebanon. Akiwa kijana mdogo alisafiri nchini Iraq ambapo baada ya kuhitimu masomo yake ya awali katika hawza ya elimu ya mjini Najaf, alianza kufanya utafiti katika elimu kadhaa kama vile fiqhi, usulu fiqhi na hadithi na kufikia daraja la juu katika uwanja huo. Sayyid Sadrud-Din Musawi Amili ameandika vitabu mbalimbali katika uga wa elimu ya sheria, nahawu na mifano ya aya za Qur’an Tukufu.

Sayyid Sadrud-Din Musawi Amili

Siku kama ya leo miaka 162 iliyopita alizaliwa Oscar Wilde mwandishi mashuhuri mjini Dublin , Ireland. Awali Oscar Wilde alisoma elimu ya msingi katika mji wa Skyline, kaskazini mwa Ireland, huku akijiunga na chuo kikuu cha Trinity na baadaye Oxford. Oscar Wilde alipata umaarufu baada ya kuandika kisa cha Mwanamfalme wa Bahati. Mwandishi huyo ameandika vitabu vingi vya mashairi ambavyo vinapatikana katika maktaba tofauti.

Oscar Wilde

Siku kama ya leo miaka 128 iliyopita, alizaliwa mjini New York Eugene O'Neill mwandishi mashuhuri wa Kimarekani. Baba yake Eugene O'Neill alikuwa mwanachama wa kundi la wasanii ambapo alifanya safari katika maeneo mengi ya dunia akiambatana na mwanaye huyo. Baadaye alisitisha masomo yake ya chuo kikuu. Mwaka 1916 Miladia aliandika makala mawili mafupi yaliyopata umaarufu mkubwa nchini humo. Mafanikio yake yalikuwa makubwa kiasi kwamba, mwaka 1922 alishinda zawadi ya fasihi. Katika mwendelezo wa kazi zake za uandishi alitunukiwa zawadi ya Nobel mwaka 1936.

Eugene O'Neill

Siku kama ya leo miaka 114 iliyopita, alifariki dunia Sayyid Abul Qasim Lahore. Abul Qasim Bin Hussein Bin Naqi Ridhawi Taqawi Lahore na aliyekuwa faqihi na mfasiri wa Qur'an Tukufu alizaliwa mjini Kashmir. Aidha Sayyid Abul Qasim Lahore alikuwa miongoni mwa maulama wakubwa nchini India huku akiwa ameandika vitabu vingi katika uwanja huo. Msomi huyo alizikwa mjini Lahore. Miongoni mwa vitabu vyake ni pamoja na 'Burhanu Shaqqul-Qamar wa Raddun-Nayril-Akbar' 'As-Swiraatul-Mustaqim.'

Sayyid Abul Qasim Lahore