Jumatatu, Oktoba 17, 2016
Leo ni Jumatatu tarehe 15 Muharram 1438 Hijria sawa na tarehe 17 Oktoba 2016.
Leo ni siku ya kimataifa ya kupambana na umasikini duniani. Umoja wa Mataifa uliainisha siku hii katika kuhamasisha jamii na serikali kupambana na umasikini.
Mwaka 1992 Mkutano Mkuu wa Baraza la Umoja wa Mataifa ulitamka na kuifanya siku hii kuwa “Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Umaskini.” Tangu wakati huo, juhudi zinafanyika kuhakikisha kuwa kila mwandamu anapata mahitaji muhimu ya kimaisha ikiwa ni pamoja na chakula, makazi, mavazi na huduma muhimu za kijamii na tiba. Hata hivyo wakati dunia ikiadhimisha siku ya kung'oa mizizi ya umaskini, idadi kubwa ya watu bado wanaishi katika umasikini wa kupindukia na wanashindwa kukidhi mahitaji yao ya kila siku, wengi wakiwa ni kutoka katika nchi za ulimwengu wa tatu.
Miaka 1085 iliyopita katika siku kama ya leo alifariki dunia Ibn Sakan mwanazuoni na mpokezi mashuhuri wa hadithi wa karne ya nne Hijiria. Alizaliwa mwaka 294 Hijiria huko Baghdad na alisafiri katika nchi mbalimbali kutafuta elimu. Ibn Sakan alikusanya hadithi nyingi katika miji mbalimbali na mwishowe akaweka maskani yake nchini Misri. Mpokezi huyo wa hadithi ameacha athari nyingi moja wapo ni kitabu cha historia kinachohusu maswahaba wa Mtume SAW, kinachoitwa Al Hurufi fis Swahaba.
Tarehe 15 Muharram miaka 849 iliyopita katika siku kama ya leo alizaliwa Ali bin Mussa bin Ja'far maarufu kwa jina la Ibn Twaus, faqihi, mpokezi wa hadithi na mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu katika eneo la Hillah nchini Iraq. Alipitisha kipindi cha utotoni katika mji huo na baadaye alihamia Baghdad ambako aliishi kwa kipindi cha karibu miaka 15. Ibn Twaus alipata umashuhuri mkubwa katika elimu na ucha-Mungu na ameandika vitabu vingi ambavyo ni marejeo ya taaluma za Kiislamu. Kitabu mashuhuri zaidi cha msomi huyo ni "al Luhuf" ambacho ndani yake anazungumzia matukio ya Siku ya Ashura na harakati ya Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) katika medani ya Karbala na katika uwanja huo hakina kifani. Kitabu kingine mashuhuri cha mwanazuoni huyo ni "al Iqbalu Biswalihil Aamal". Ibni Twaus alifariki dunia mwaka 664 akiwa na umri wa miaka 75.
Miaka 43 iliyopita katika siku kama hii ya leo nchi za Kiarabu zinazouza nje mafuta ya petroli zilianza kutekeleza vikwazo vya mafuta dhidi ya Marekani, Uingereza na makampuni yanayouuzia mafuta utawala wa Kizayuni wa Israel. Hatua hiyo ilichukuliwa kutokana na uungaji mkono mkubwa wa Marekani na Uingereza kwa utawala ghasibu wa Israel katika vita vya Israel dhidi ya Syria na Misri. Hatua hiyo ilipandisha sana bei ya mafuta katika masoko ya kimataifa na kutoa pigo kubwa kwa nchi hizo za Magharibi. Muda mfupi baadaye nchi za Kiarabu zilikiuka vikwazo hivyo vya mafuta na kuanza tena kuiuzia mafuta Marekani na Uingereza. Vikwazo hivyo vilionesha kuwa nchi za Kiislamu zina silaha muhimu inayoweza kutumiwa dhidi ya uungaji mkono mkubwa wa nchi za Magharibi kwa utawala katili wa Israel.
Na Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita, aliaga dunia mtaalamu wa masuala ya jamii wa Kifaransa kwa jina la Raymond Aron. Aron alizaliwa mwaka 1905. Msomi huyo wa Kifaransa alikuwa akifundisha pia taaluma hiyo ya masuala ya jamii katika Chuo Kikuu cha Sorbonne, Paris kwa miaka kadhaa. Vilevile alikuwa akiandika makala katika majarida ya Le Figaro na Express mjini Paris. Raymond Aron ameandika vitabu vingi na hapa tunaweza kuashiria vitabu vyake vichache alivyovipa majina ya "Kuanza Vita vya Nyuklia, "Mapambano ya Kitabaka" na "Miaka ya Mwishoni mwa Karne".