Jumanne, tarehe 18 Oktoba 2016
Leo ni Jumanne tarehe 16 Muharram 1438 Hijria sawa na tarehe 18 Oktoba, 2016.
Miaka 178 iliyopita katika siku kama hii ya leo Amir Abdulqadir al Jazairi hatimaye alitiwa mbaroni baada ya kuendesha mapambano ya miaka 15 dhidi ya wavamizi wa Kifaransa nchini Algeria.
Kutokuwa na kambi za kuendeshea mapambano na harakati za ukombozi ndani ya Algeria ilikuwa mojawapo ya sababu zilizopelekea kushindwa Amir Abdulqadir na Wafaransa. Baada ya kushindwa Amir Abdulqadir, nchi yote ya Algeria ikakaliwa kwa mabavu na Wafaransa. Amir Abdulqadir alifungwa katika jela ya Ufaransa kwa kipindi cha miaka 9 na kisha aliachiwa huru kwa sharti kwamba asirejee nchini kwake.
Siku kama ya leo miaka 145 iliyopita alifariki dunia msomi wa Uingereza na mvumbuzi wa mashine ya kikokoteo (Calculator) kwa jina la Charles Babbage. Mwaka 1812 Miladia, Babbage aliasisi taasisi ya uchunguzi kwa ajili ya kuendeleza elimu ya hisabati na akiwa na miaka 24 akateuliwa kujiunga na taasisi ya ufalme ya Uingereza. Ni baada ya hapo ndipo akaanzisha harakati ndefu za utafiti wa kuunda mashine hiyo ya hesabu ambapo hadi kufikia mwaka 1833 Miladia akafanikiwa kuvumbua chombo hicho ambacho kilikuja kuwa mashuhuri kwa jina la Babbage. Baada ya hapo karne moja baadaye wasomi mbalimbali waliifanyia marekebisho muhimu mashine hiyo sanjari na kuifanya itumie nishati ya umeme. Ni kwa ajili hiyo ndio maana Charles Babbage akatambuliwa kwa jina la baba wa kikokoteo (Calculato).
Miaka 149 iliyopita, ardhi ya Alaska ilidhibitiwa na Marekani. Alaska ni ardhi yenye upana wa karibu kilometa mraba milioni moja na laki tano, huko Amerika ya kaskazini magharibi, ambapo hii leo ni moja ya majimbo ya nchi hiyo. Hadi mwaka 1867 Miladia, Alaska ilikuwa ikidhibitiwa na Russia, hata hivyo katika kipindi hicho mfalme wa wakati huo wa Urusi ya zamani hakutilia maanani umuhimu wa ardhi hiyo na hivyo mwezi Oktoba mwaka 1867 Miladia akaamua kuiuza kwa Marekani. Ni vyema ifahamike kuwa, hii leo Alaska inahesabika kuwa moja ya majimbo tajiri sana ya Marekani ambapo mwaka 1960 kulivumbuliwa mafuta na kuanza kuchimbwa katika eneo hilo hadi leo.
Siku kama ya leo miaka 85 iliyopita, msomi aliyegundua umeme kwa jina la Thomas Edison alifariki dunia. Edison alizaliwa mwaka 1847 huko Marekani. Thomas Edison hakuwa na taalumu yoyote kutoka chuo kikuu bali ni tafiti na majaribio yake mengi ndiyo yaliyopandisha juu kiwango chake cha elimu na maarifa. Akiwa kijana, Edison aliasisi maabara moja ya masuala ya kemia na kufanya majaribio makubwa katika maabara hiyo. Bidii ya msomi huyo ilimuwezesha kuvumbua mambo mengi ambapo muhimu kati ya hayo ni hatua yake ya kuvumbua umeme, kutengeneza lampu na gramafoni au santuri.
Miaka 94 iliyopita katika siku kama ya leo, Redio ya BBC iliasisiwa huko Uingereza. Redio ya BBC awali ilikuwa ya mtu binafasi, lakini ilipofika mwaka 1927, redio hiyo ikawa chini ya usimamizi wa serikali na hivyo kuwa katika kalibu ya redio za serikali ya Uingereza. Bajeti ya redio za BBC ambazo zinatangaza kwa lugha mbalimbali za dunia inadhaminiwa na serikali ya Uingereza. Pamoja na kuwa BBC inadai kwamba haipendelei upande wowote katika matangazo yake, lakini katika kipindi cha nusu karne ya hivi karibuni, chombo hicho cha kupasha habari kimegeuka na kuwa wenzo wa propaganda wa serikali ya Uingereza na hivyo kuiandalia London uwanja wa kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine.
Na siku kama ya leo miaka 29 iliyopita manowari za jeshi la Marekani zilishambuulia visiwa vya mafuta vya Jamhuri ya Kiislamu katika Ghuba ya Uajemi wakati wa vita vya Iraq dhidi ya Iran. Mashambulizi hayo yalifanyika baada ya Kuwait iliyokuwa ikiusaidia utawala wa dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein katika vita vyake dhidi ya Iran, kuitihumu Jamhuri ya Kiislamu kuwa imeshambulia meli yake ya mafuta. Marekani ilivishambulia visiwa vya mafuta vya Iran kwa madai kuwa meli ya Kuwait iliyoshambuliwa na Iran ilikuwa na bendera ya nchi hiyo.