Jumatano, Oktoba 19, 2016
Leo ni Jumatano tarehe 17 Mfunguo Nne Muharram 1438 Hijria sawa na 19, Oktoba 2016.
Siku kama hii ya leo miaka 540 iliyopita Nuruddin Abdulrahman Jami, malenga na mwanafasihi mkubwa zaidi wa Kiirani wa karne ya Tisa Hijria alifariki dunia katika mji wa Harat katika Afghanistan ya leo ambao wakati huo ulikuwa sehemu ya ardhi ya Iran. Alielekea huko Samarqand wakati wa ujana wake na akiwa huko alijifunza masomo ya dini, fasihi na historia. Vitabu muhimu vya malenga huyo ni pamoja na "Silsilatu Dh-hahab", Nafahatul Uns, Shawahidu Nubuwah na "Baharistan."
Siku kama ya leo miaka 479 iliyopita alizaliwa Bahauddin al Amili maarufu kwa jina la Sheikh Bahai, faqihi na aalim mkubwa wa Kiislamu huko katika mji wa Baalbek nchini Lebaon. Baba yake Sheikh Bahai alikuwa mmoja wa maulamaa wakubwa wa Lebanon ambaye alisafiri naye nchini Iran akiwa mtoto. Sheikh Bahai alitumia kipaji chake kikubwa na kuweza kufikia daraja ya uanazuoni katika kipindi kifupi. Aalim huyo alipewa jina la Sheikhul-Islam kutokana na kipawa cha kielimu cha hali ya juu alichokuwa nacho. Sheikh Bahai ameacha zaidi ya vitabu 88 alivyoviandika kwa lugha za Kifarsi na Kiarabu. Baadhi ya vitabu vyenye thamani vya msomi huyo wa Kiislamu ni kama vile ya Jame Abbasi, Kashkool kilichojumuisha riwaya na hadithi, Tashrih al Aflaq na vingine vingi alivyoviandika kuhusu masuala ya hisabati na kemia. Sheikh Bahai alifariki dunia mwaka 1030 Hijria huko Isfahan Iran.
Siku kama ya leo miaka 13 iliyopita, alifariki dunia Ali Ezzat Begovic, mwanasiasa na mwandishi wa Bosnia Herzegovina. Ali Begovic alizaliwa mwaka 1925 na kupata taaluma ya sheria katika Chuo Kikuu cha Sarajevo katikati mwa Bosnia. Alianza kupambana na utawala wa kikomunisti wa Yugoslavia ya zamani akiwa kijana mdogo na kufungwa jela mara kadhaa. Mwaka 1989 Ali Begovic aliasisi chama kipya cha siasa kwa jina la Democratic Action kilichokuwa na nafasi kubwa katika uhuru wa Bosnia mwaka hapo 1991. Mwanasiasa huyo wa Kiislamu ambaye baada ya uhuru wa taifa hilo alichaguliwa kuwa rais, alikuwa na nafasi kubwa katika kuwatetea raia wa Bosnia katika mashambulizi ya askari wa Serbia dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo.
Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, Ali Hassan Salamah mmoja kati ya viongozi wa ngazi za juu wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) aliuawa shahidi nchini Lebanon kupitia njama za vibaraka wa shirika la ujasusi la utawala haramu wa Israel MOSSAD. Salamah alikuwa afisa wa usalama wa PLO na aliuawa shahidi baada ya kuripuka bomu lililotegwa katika gari lake mjini Beirut. Jinai hiyo ya utawala haramu wa Israel ndani ya Lebanon kwa mara nyingine iliweka wazi ugaidi na uvamizi wa Israel dhidi ya ardhi ya nchi nyingine.
Miaka 235 iliyopita katika siku inayofanana na ya leo, Charles Cornwallis, kamanda wa kikosi cha wanajeshi wa Uingereza nchini Marekani alisalimu amri mbele ya George Washington, kamanda wa kikosi cha wanajeshi wa Marekani na kwa msingi huo vita vya kuikomboa Marekani vikamalizika rasmi. Vita hivyo vilianza mwaka 1775 kati ya wahajiri wa Kimarekani na wakoloni wa Kiingereza. Miaka miwili baada ya ushindi wa mwisho wa wahajiri, pande mbili hizo zilisaini makubaliano mwaka 1783 ambapo kwa mujibu wake Uingereza ilitambua rasmi uhuru wa Marekani.