Oct 20, 2016 01:13 UTC
  • Alkhamisi 19 Oktoba, 2016

Leo ni Alkhamisi tarehe 18 Muharram 1438 Hijria sawa na Oktoba 20, 2016.

Siku kama ya leo miaka 5 iliyopita, dikteta wa zamani wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi alikamatwa na wanamapinduzi karibu na mji wa bandari wa Sirte kaskazini mwa nchi hiyo na kuuawa. Gaddafi aliuawa baada ya miezi kadhaa ya mapigano na wanamapinduzi ambapo jeshi lake liliwaua maelfu ya wananchi hususan katika miji ya Benghazi na Tripoli. Gaddafi ambaye aliitawala Libya kwa zaidi ya miaka 42, alizaliwa mwaka 1942. Aliingia madarakani mwaka 1969 kupitia mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa madarakani mfalme Mohammad Idris al-Sanusi.

Muammar Gaddafi

Miaka 64 iliyopita muwafaka na siku kama hii ya leo, Jomo Kenyatta mwanaharakati, mwanasiasa na mpigania uhuru mashuhuri barani Afrika na Rais wa Kwanza wa Kenya alitiwa mbaroni kufuatia amri ya utawala wa kikoloni nchini Kenya. Mzee Kenyatta alikuwa miongoni mwa watu 100 mashuhuri nchini humo waliotiwa mbaroni katika kipindi cha masaa 24 ikiwa ni katika fremu ya mpango wa kuibana Mau Mau, kundi la wapiganaji wa Kenya waliokuwa wakiupinga utawala wa kikoloni wa Waingereza. Wakenya huadhimisha siku hii kama Sikukuu ya Mashujaa na kuwakumbuka wale wote waliopigania uhuru wa taifa hilo.

Jomo Kenyatta

Siku kama ya leo miaka 129 iliyopita, alizaliwa Ayatullah Sayyid Ahmad Khansari, faqihi na marjaa mkubwa wa Kishia. Akiwa na miaka 20, Ayatullah Ahmad Khansari alielekea mjini Najaf, Iraq na kustafidi na elimu kutoka kwa wasomi wakubwa kama vile Muhaqqiq Khorasani, Sayyid Muhammad Kadhim Yazdi, Shariat Isfahani na Muhaqqiq Naaini. Ayatullah Sayyid Ahmad Khansari alielekea mjini Arak, Iran katika kipindi cha kuasisiwa chuo kikuu cha kidini (hauza) mjini humo na kujishughulisha na ukufunzi. Baadaye msomi huyo alishirikiana na Ayatullah Sheikh Abdul-Karim Hairi katika shughuli za tablighi na baada ya kuasisiwa hauza ya Qum chini ya usimamizi wa Ayatullah Hairi Yazdi, Ayatullah Ahmad Khansari alikuwa imamu wa Swala ya jamaa katika chuo cha Faiziya mjini humo. Mwaka 1370 Hijiria, Ayatullah Ahmad Khansari alielekea mjini Tehran na kuwa imamu wa Swala ya jamaa katika msikiti maarufu wa ‘Sayyid Azizullah’. Hadi mwisho wa uhai wake msomi huyo alisalia mjini Tehran na baada ya kufariki dunia akazikwa mjini Qum.

Ayatullah Ahmad Khansari

Siku kama ya leo, miaka 145 iliyopita alizaliwa Allamah Haidar Qali Sardar Kabuli, alimu mkubwa na mtaalamu wa fiqhi mjini Kabul, Afghanistan. Akiwa kijana mdogo Allamah Sardor Kabuli alipata kusoma kwa wasomi wakubwa wa enzi hizo kama vile, Mirza Hussein Nuri na Sayyid Swafiyyud-Din Hassan bin Hadi Kadhimi, sanjari na kustafidi na elimu kutoka kwa maulama na maraajii watajika kama vile, Sayyid Hassan Sadr naHaji Sheikh Abbas Qumi, ambapo pia alipata ijaza (idhini) ya kunakili na kuandika hadithi. Mwaka 1310 Hijiria, Allamah Haidar Qali Sardar Kabuli alielekea mjini Kermanshah, Iran na kujishughulisha na ufundishaji kwa wakazi wa mji huo sanjari na kuandika vitabu kadhaa. Aidha msomi huyo alipata kusomea lugha kadhaa za dunia, kama vile Kiarabu, Kingereza, Kiebrania na Urdu. Kitabu cha ‘Tarjama ya Injili ya Barnaba’ na ‘Hadithi 40 katika fadhila za Amirul-Muuminin’ ni miongoni mwa athari za msomi huyo. Allamah Haidar Qali Sardor Kabuli alifariki dunia mwaka 1372 Hijiria, akiwa na umri wa miaka 79 na kuzikwa mjini Najaf, Iraq.

Haidar Qali Sardar

Siku kama ya leo miaka 157 iliyopita, alizaliwa John Dewey, msomi na mwandishi mashuhuri wa Marekani. Dewey alikuwa amebobea mno katika elimu ya malezi na aliweza kujifunza mengi alipokuwa katika chuo kikuu cha Colombia. John Dewey alifanikiwa kuandika vitabu vingi kuhusiana na malezi na makuzi ya mtoto. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya msomi huyo ni pamoja na "How we think", "The Public and its Problems" na "Freedom and Culture" John Dewey alifariki dunia mwaka 1962 akiwa na umri wa miaka 92.

John Dewey

Na miaka 189 iliyopita kama leo vita vya majini vya Navarino au The Battle of Navarino vilitokea katika ghuba ndogo ya Navarino kwenye bahari ya Mediterranean. Katika vita hivyo, meli za kivita za Uingereza, Russia na Ufaransa zilizishambulia meli za kivita za utawala wa Othmania kwa lengo la kuihami Ugiriki. Vita hivyo vilifikia tamati kwa kushindwa vibaya utawala wa Othmania.

The Battle of Navarino