Oct 28, 2016 04:02 UTC
  • Ijumaa, Oktoba 28, 2016

Leo ni Ijumaa tarehe 26 Mfunguo Nne Muharram 1438 Hijria sawa na 28 Oktoba, 2016 Milaadia

Siku kama ya leo miaka 1374 iliyopita mji mtakatifu wa Makka ulishambuliwa kwa mabomu baada ya kuzingirwa na jeshi la mtawala mal'uni wa kizazi cha Banii Umayyah, Yazid bin Muawiyya. Baada ya kumuua shahidi mjukuu wa Mtume (saw), Imam Hussein bin Ali na wafuasi wake katika medani ya Karbala, na Watu wa Nyumba ya Mtume wakachukuliwa mateka, Yazid alidharaulika sana na kukosa heshima katika Umma wa Kiislamu. Waislamu katika maeneo mbalimbali walianzisha uasi dhidi ya utawala wake. Harakati hizo za uasi zilifika hadi Hijaz hapo mwaka 63 Hijria ambapo watu wa Makka walimfukuza gavana wa Yazid na kuchukua madaraka ya mji huo. Mtawala huyo alituma jeshi ambalo liliuzingira mji huo mtukufu na kushambulia Msikiti wa Makka na al Kaaba kwa kutumia mabomu.

Msikiti mtakatifu wa Makka

Miaka 415 iliyopita aliaga dunia Sheikh Abdullah Tostari faqihi na msomi wa Kiislamu wa Kiirani. Sheikh Tostari alifikia daraja ya ijtihad baada ya kuhitimu masomo ya kidini chini ya maustadhi wakubwa wa zama hizo. Sheikh Abdullah Tostari baadaye alielekea katika hauza ya kielimu ya mji wa Isfahan nchini Iran na kuanza kufundisha masomo ya dini. Darsa ya mujtahidi huyo ilikuwa ikihudhuriwa na wanafunzi wengi ambao walinufaika na bahari kubwa ya elimu yake. Allamah Majlisi na Mirza Muhammad Naini ni miongoni mwa wanafunzi wa Sheikh Abdullah Tostari. Msomi huyu wa Kiislamu ameandika vitabu vingi kama Khawasul Qur'ani na Jamiul Fawaid.

شیخ عبدالله تستری

Siku kama ya leo miaka 90 iliyopita yaani tarehe 7 Aban mwaka 1305 Hijria Shamsia Ayatullah Sayyid Hassan Modarres aliyekuwa miongoni mwa wanazuoni na wanamapambano maarufu nchini Iran alinusurika jaribio la kuuawa. Jaribio hilo lilifanywa na vibaraka wa Shah Reza Pahlavi aliyekuwa maarufu kwa udikteta, ukatili na upinzani mkubwa dhidi ya maulama wa Kiislamu. Uhasama wa utawala wa kifalme wa Pahlavi dhidi ya Ayatullah Modarres ulitokana na mchango mkubwa wa mwanazuoni huyo wa Kiislamu katika kuwaamsha wananchi na kufichua njama za utawala wa Kipahlavi na muungaji mkono wake yaani serikali ya Uingereza. Kwa kipindi fulani Ayatullah Modarres alikuwa mwakilishi wa wananchi wa Tehran katika Bunge. Baada ya kunusurika kifo katika jaribio hilo Ayatullah Modarres alipelekwa uhamishoni kwa amri ya mfalme dikteta Reza Khan na muda mfupi baadaye aliuawa shahidi na vibaraka wa Shah.

yatullah Sayyid Hassan Modarres

Tarehe 28 Oktoba miaka 68 iliyopita wakati wa vita vya kwanza kati ya utawala wa Kizayuni wa Israel na Waarabu, wanajeshi wa utawala huo waliwaua kwa umati wakazi wa kijiji cha al Dawayima huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Wazayuni hao walivamia msikiti wa kijiji hicho na kuwauwa shahidi Waislamu 75 raia wa Palestina waliokuwa wakisali. Vilevile waliwaua kwa umati watu wa familia 35 waliokuwa wamekimbilia hifadhi katika pango moja nje ya kijiji hicho. Askari jeshi wa utawala haramu wa Israel walikisawazisha na ardhi kijiji hicho baada ya kuwaua kwa umati wakazi wake wote.

Tarehe 28 Oktoba mwaka 1962 ulihitimishwa mgogoro wa makombora wa Cuba baada ya kiongozi wa wakati huo wa Urusi, Nikita Khrushchev kuamuru kurejeshwa nyumbani meli zilizokuwa na makombora ya nyuklia. Hatua ya Urusi ya kujenga vituo kadhaa vya makombora ya nyuklia nchini Cuba katika umbali wa kilomita 90 kutoka Marekani ilizusha mgogoro mkubwa wa makombora uliokaribia kuitumbukiza dunia katika vita vya nyuklia. Wakatri huo Marekani na Russia zilitishia kushambuliana kwa makombora ya nyuklia na kuzusha hofu kubwa hususan kwa watu wa Marekani, Russia na nchi za Ulaya. Hatimaye tarehe 28 Oktoba mwaka 1962 Nikita Khrushchev alitoa amri ya kurejea nchini meli zote zilizokuwa na makombora ya nyuklia na kufungwa vituo vya makombora vya Urusi nchini Cuba.

Nikita Khrushchev

 

Tags