Oct 30, 2016 00:17 UTC
  • Wanajeshi wa Hulagu Khan
    Wanajeshi wa Hulagu Khan

Leo ni Jumapili tarehe 28 Muharram mwaka 1438 Hijiria, sawa na tarehe 30 Oktoba mwaka 2016 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 782 iliyopita, baada ya kuuawa Al-Musta'sim, khalifa wa mwisho wa utawala wa Bani Abbasi, na kuhitimishwa silsila ya watawala hao iliyodumu kwa kipindi cha miaka 500 katika maeneo mengi ya ulimwengu wa Kiislamu, hatimaye Baghdad, mji mkuu wa utawala huo wa Bani Abbasi ulidhibitiwa na Hulagu Khan wa utawala wa Mongol. Katika juhudi za kupanua utawala wake, Hulagu Khan alifanya kila aina ya jinai huku akiwa mtu mwenye moyo mgumu sana ambapo katika kuzitawala nchi kadhaa alifanya mauaji ya umati dhidi ya wanavijiji na  wakazi wa miji yote aliyoitwaa. Katika kuudhibiti mji wa Baghdad, kiongozi huyo wa Mongol, aliua maelfu ya watu ikiwa ni pamoja na kuharibu nyumba na majengo muhimu ya mji huo.

Siku kama ya leo miaka 158 iliyopita, alizaliwa Hakim Mirza Muhammad Twahir Tankabani,. Baada ya masomo yake ya awali ya Kiislamu alielekea mjini Tehran na kujifundisha elimu ya sheria za Kiislamu (fiqhi),  usulu fiqhi na falsafa kutoka kwa maulama wakubwa wa enzi hizo. Baadaye Mirza Muhammad Twahir Tankabani alianza shughuli za ufundishaji katika shule ya Sepah Salar mjini hapo. Baadaye aliingia katika uwanja wa siasa na kufanikiwa kuingia bungeni. Hatimaye mwaka 1360 Hijiria akafariki dunia akiwa na umri wa miaka 80. Alifahamika kwa ujuzi wake wa elimu ya falsafa.

Hakim Mirza Muhammad Twahir Tankabani

Siku kama ya leo miaka 145 iliyopita, alizaliwa Paul Valéry, malenga na mtaalamu mashuhuri wa fasihi nchini Ufaransa. Alihitimu masomo yake katika taaluma ya sheria. Kutokana na kuvutiwa sana na fasihi na baada ya kufanya utafiti mwingi wa athari za wasomi wakubwa waliomtangulia, aliingia katika uga wa mashairi na fasihi. Kitabu chake cha kwanza alikisambaza mwaka 1889 Miladia na kupata umaarufu mkubwa. Baada ya hapo Paul Valéry alianza kusoma mashairi mbalimbali na kuingia katika orodha ya malenga maarufu wa Ufaransa enzi hizo. Ameacha vitabu kadhaa katika taaluma ya fasihi na mashairi ambavyo vimehifadhiwa katika maktaba za nchi hiyo.

Paul Valéry

Siku kama ya leo miaka 106 iliyopita, aliaga dunia Henri Dunant, mwasisi wa jumuiya ya Msalaba Mwekendu duniani. Jean Henri Dunant aliasisi jumuiya hiyo mwaka 1862 Miladia kupitia kijitabu kidogo ambacho ndani yake aliwashawishi watu kuunda asasi za kujitolea ambazo zilitakiwa kuwasaidia wagongwa na watu waliojeruhiwa katika vita. Kufuatia pendekezo hilo, katikati ya mwezi Mei mwaka 1863 kulifanyika kongamano la kimataifa mjini Geneva, Uswisi kwa ajili ya kuasisiwa Jumuiya ya  Kimataifa ya Msalaba Mwekendu. Wawakilishi 16 kutoka nchi za Ulaya walishiriki kongamano hilo. Kongamano hilo lilipelekea kutiwa saini ya kuendelezwa juhudi za kuasisiwa kwake hapo tarehe 22 Agosti mwaka 1864. Hatimaye Jean Henri Dunant akafariki dunia tarehe 30 Oktoba mwaka 1910, Miladia.

Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio nambari 540, kufuatia kushambuliwa na utawala wa Baathi wa Iraq, meli za kibiashara katika Ghuba ya Uajemi. Hatua hiyo ilikuja kufuatia utawala wa Iraq kushambulia meli za kibiashara katika kipindi cha vita vyake vya kiuchokozi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hujuma ambazo zilikuwa na lengo la kuchafua usalama wa eneo zima. Kufuatia azimio hilo, meli zote za kibiashara zilitakiwa kufanya safari zake katika maji ya kimataifa kwa uhuru sanjari na nchi za eneo kutakiwa kuheshimu amri hiyo. Aidha azimio hilo lilizitaka pande hasimu za mapigano kuhitimisha uhasama wao na kuheshimu pwani za nchi za ghuba hiyo. Inafaa kuashiria kuwa, azimio hilo lilitolewa huku utawala wa Saddam Hussein ukishadidisha mashambulizi yake dhidi ya meli za mafuta za Iran.

Salman Harati

Na siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, alizaliwa malenga wa zama hizi Salman Harati. Salman Harati ambaye jina lake la asili ni Salman Qanbar Harati, alizaliwa katika kijiji cha Marz Dasht, cha mji wa Tonekabon nchini Iran. Alikuwa malenga mwanamapinduzi na shakhsia wa kidini. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni pamoja na ‘Asman Sabz’ na ‘Dari be Khoneh Khorshid’ kadhalika aliandika kitabu cha ‘Az in Setareh ta un Setareh’ ambacho hufundishwa mashuleni. Alijitahidi kutumia lugha nyepesi katika mashairi yake ili kumuwia rahisi msomaji kuelewa.