Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (142)
Assalam Aleikum wapezi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri Ya Kiislamu ya Ira inayokutangazieni kutoka mjini Tehran.
Katika kipidi hiki tutaendelea kujadili na kuzungumzia jibu la Qur’ani Tukufu ambalo tumekuwa tukilijadili katika vipindi kadhaa vilivyopita, ambalo linasemam je, ni kwa nini Mtume Mtukufu (saw) alibana uongofu wa Waislamu katika kushikama kwao na Vizito Viwili ambavyo ni Qura’ni Tukufu na Ahlul Beit wake watoharifu (as), kama ilivyopokelewa katika hadithi mashuhuri ya Thaqalain?
Tulipata kujua majibu kadhaa ya Qur’ani kwamba hadithi hii tukufu ni ufafanuzi na tafsiri ya Mtukufu Mtume (saw) kuhusiana na aya kadhaa za Qur’ani ambazo zinabainisha wazi kuwa kushikamana kiukweli na Qur’ani Tukufu na kunufaika nayo muumini kama inavyotakiwa hutimia tu kwa njia ya kushikamana kikamilifu na wale watu waliopewa elimu ya kitabu hicho chote na Mwenyezi Mungu, nao ni Muhammad na Aali zake watoharifu.
Katika kipindi hiki tutajadili masuala kadhaa ambayo yanasisitiza na kutufikisha katika natija hii kwamba ni Mwenyezi Mungu Mwenyewe tu ndiye anayekilinda kitabu hiki ambacho hakifikiwi wala kuguswa na batili kutoka upande wowote ule. Basi endeleeni kuwa nasi hadi mwisho wa kipindi hiki ili tupate kunufaika kwa pamoja na yale tuliyokuadalieni kwa juma hili, karibui.
Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema katika aya ya tisa ya Surat al-Hijr: Hakika Sisi ndio tulioteremsha Ukumbusho huu, na hakika Sisi ndio tutaoulinda. Na kadhalika anasema katika aya mbili za 41 na 42 za Surat Fuswilat: Kwa hakika wale ambao wanakataa dhikiri inapowajia (wataangamia), na haya bila ya shaka ni Kitabu chenye nguvu na utukufu. Hautakifikia upotovu mbele yake wala nyuma yake. Kimeteremshwa na Mwenye hikima, Msifiwa.
Wanazuoni wametolea hoja haya mbili hizi kuthibitisha kwamba ni Mwenyezi Mungu mwenyewe ndiye anayekilinda kitabu chake hiki kitakatifu na kwamba hakitafikiwa na mikono ya batili ya wapotoshaji kama ilivyofanyika kuhusiana na vitabu vya Torati na Injili. Kwa msingi huo Waislamu wote wanaamini na kuwa na yakini kwamba kitabu hiki cha Qur’ani ambacho kimo mikononi mwa Waislamu wote ndicho kilekile kitabu kilichoteremshiwa Mtume Mtukufu (sw) bila ya kuwa na nyongeza wala upungufu wowote, na kwamba madai yanayotolewa na baadhi ya mapote potevu kwamba kuna Qur’ani nyingine isiyokuwa hii ambayo iko miongoni mwa Waislamu ni uongo mtupu ambao hauna msingi kwa sababu kitabu kama hicho kinachodaiwa kuwepo miongoni mwa baadhi ya Waislamu hakina utajiri wa lugha, nidhamu na mfumo maalumu wa maneno na balagha ya hali ya juu kama inavyoonekana katika kitabu hicho cha mbinguni. Hili linahusiana na ukanushaji wa kuwepo upotoshaji wa maneneo na lafudhi katika kitabu hicho cha mbinguni. Lakini bado kuna upotoshaji mwingine ambao ni upotishaji wa kimaanawi ambapo aya nyingi za Qur’ani zinaashiria kutokea kwa upotoshaji kama huo katika aya zake nyingi, ambapo kwa mfano aya ya saba ya Surat Aal Imran inasema kwamba kuna wale ambao nyoyoni mwao umo upotovu wanaofuata aya zile za mifano kwa kutafuta fitna, na kutafuta maana yake bila ya kuwa na elimu; na kwamba hapana ajuaye maana yake halisi ila Mwenyezi Mungu. Kwa kuzingatia hayo, je, Mwenyezi Mungu anakilinda vipi kitabu hiki kitakatifu kutokana na upotoshi na batili kama alivyoahidi Yeye mwenyewe na upotovu huu hauhusiani tu na upotoshaji wa maneneo na lafudhi tu bali unashamiri hata upotoshaji wa kimaanawi pia?
Katika kujibu swali hili tunarejea baadhi ya hadithi za Bwana Mtume (saw) ambapo tunapata kwamba zinasema waziwazi kuwa majukumu ya Maimamu wa Nyumba ya Mtukufu Mtume (saw) ambao ni Kizito cha Pili kati ya Vizito Viwili alivyotuachia Mtume (saw), ni walindaji shupavu wa dini na Qur’ani Tukufu kutokana na upotovu wa aina yoyote ile uwe ni wa kimaneneo au kimaanawi. Imepokelewa katika kitabu cha al-Mi’yaar wal Muwazana cha Abu Ja’ffar al-Iskafi kuwa Mtume Mtukufu (sw) alisema: ‘Wanabeba elimu hii katika kila upande, Watu wa Nyumba yangu ambao ni sawa na Qur’ani, wanaiepusha mbali na upotovu wa wapotovu (washirikina), ulaghai wa mabatili na tafsiri ya majahili.’
Madhumuni ya hadithi hii pia yaneonekana katika hadithi kadhaa ambazo zimepokelewa kwa wingi katika vitabu vya Masuni bila kutajwa jina la Ahlul Beit wa Mtume (saw). Imepokelewa katika Tafsiri ya Furat al-Kufi, Ghaibat an-Nu’mani, Ith’bat al-Wasiya cha al-Mas’udi kutoka kwa Imam Ja’ffar as-Swadiq (as), kupitia kwa baba zake kutoka kwa Mtume (saw) kwamba alisema katika sehemu ya hadithi ndefu: ‘Hakika Mwenyezi Mungu alichagua kitu kutoka katika kila kitu… Alichagua siku ya Ijumaa kweye siku, mwezi wa Ramadhani kwenye miezi, Leilatul Qadr kwenye nyusiku na akachagua kutoka kwangu na kwa Ali, al-Hassan na al-Hussein na kukamilisha Maimamu kumi na wawili katokana na kizazi cha al-Hussein wa tisa wao ni batini na dhahiri yao…… naye ni Qaim wao, wanapinga upotovu wa wapotoshaji kwenye dini, ulaghai wa mabatili na tafsiri ya majahili.’
Na Imam Ja’ffar as-Swadiq (as) amepokelewa akisema katika kitabu cha al-Kafi: …..Basi tazameni mnaichukua elimu yenu hii kutoka kwa nani kwani miongoni mwetu Ahlul Beit katika kila zama kuna waadilifu ambao hupinga upotovu wa wapindukiaji mipaka, ulaghai wa mabatili na tafsiri ya majahili.’
Ndugu wasikilizaji mbali na hadithi hii tuliyoitaja, kuna hadithi na aya nyingine nyingi za Qur’ani Tukufu ambazo zinafafanua na kuthibitisha kwamba Ahlul Beit wa Mtume Mtukufu (saw) ndio dhikiri tuliyoamrishwa na Mwenyezi Mungu kuiuliza tunapokumbwa na matatizo na maswali yasiyoweza kujibiwa na watu wengine kuhusiana na masuala mbalimbali na hii ni kwa sababu ni Mwenyezi Mungu mwenyewe ndiye aliyewapa uwezo na elimu hiyo ya kufafanua na kuyapatia ufumbuzi maswali na matatizo yanayowakumba wanadamu maishani. Kwa ufupi wao ndio walio na elimu ya kitabu kizima na kitakatifu cha Qur’ani kama zinavyothibitisha hilo aya ya mwisho ya Surat ar-Ra’d, aya ya ‘Hawaigusi isipokuwa watoharifu,’ aya ya Tat’hir na aya nyingine nyingi. Kwa msingi huo hao ndio watu wanaofaa kulinda kitabu kitakatifu cha Mwenyezi Mungu kutokana na upotoshaji wowote unaoenezwa na maimamu wa upotovu na wanaojitwisha elimu wasiyokuwa nayo kuhusiana na Qur’ani pamoja na majahili wanaofasiri kitabu hiki kitakatifu cha mbinguni kwa msingi wa matakwa na matamanio yao binafsi, hata kama hawatakuwa na kusudio na nia mbaya ya kufanya hivyo moja kwa moja.
Na jambo lenye faida hapa ni kurejea mambo yaliyopokelewa kutoka kwa Imam Hassan al-Askari (as) katika kuepusha fitina ya kitabu kilichoandikwa na mwanafalsafa mashuhuri kwa jina la Is’haq bin Ya’qub al-Kindi katika kupinga Qur’ani Tukufu. Imam Askari (as) alimfundisha mmoja wa masahaba zake hoja ambayo angeitumia kuvunja moja kwa moja msingi alioutegemea al-Kindi katika uandishi wa kitabu chake hicho. Aliposikia hoja hiyo al-Kindi alifahamu mara moja kosa alilokuwa amelifanya katika kutegemea msingi huo katika uandishi wa kitabu hicho na hivyo kuchukua uamuzi wa kukichoma moto. Kwa njia hiyo Imam Hassan al-Askari (as) aliweza kulinda na kuhifadhi Kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu kutokana na fitina na upotovu wa watu wasiokuwa na elimu ya kutosha kuhusu kitabu hicho.
Na hatimaye tunafupisha mambo tuliyosoma kwenye kipindi hiki wapenzi wasikilizaji kwa kusema kwamba moja ya siri kuu na muhimu za Mtume Mtukufu (saw) kubana uongofu wa Waislamu na kuwaepusha na upotovu kwa kushikamana sambamba na kwa wakati mmoja na Vitu Viwili Vizito alivyotuachia, yaani Kitabu cha Mwenyezi Mungu Qur’ani Tukufu na Ahlul Beit wake watoharifu (as), ni kwa sababu Mwenyezi Mungu aliwajaalia Ahlul Beit hao kuwa njia, hoja na wenzo wa kulinda kitabu hicho kitakatifu kutokana na upotoshaji wa wanaovuka mipaka ya imani, mabatili, walaghai na majahili wanaojaribu kufasiri kitabu cha mwenyezi Mungu bila ya kuwa na elimu ya kutosha kuhusiana na suala hilo.
Na kufikia hapa ndio tunafikia mwisho wa kipindi chetu cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain kwa juma hili wapenzi wasikilizaji, kipindi ambacho kama kawaida kimekujieni moja kwa moja kutoka Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Tunakushukuruni nyote kwa kuwa pamoja nasi hadi mwisho wa kipindi. Msikose kujiunga nasi tena katika kipidi kijacho panapo majaaliwa ili kusikiliza mengine mengi ambayo tutakuwa tumekuandalieni katika kipindi hicho. Hadi wakati huo basi tuakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.