Nov 02, 2016 02:33 UTC
  • Jumatano, Novemba 2, 2016

Leo ni Jumatano tarehe Pili Mfunguo Tano Safar 1438 Hijria sawa Novemba Pili 2016 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1317 iliyopita aliuawa shahidi Zaid bin Ali bin Hussein mwana wa Imam Sajjad (as) na mjukuu wa Mtume Muhammad (saw). Zaid bin Ali alisimama kupambana na dhulma za Banii Umayyah na kulinda matunda ya mapambano ya babu yake, Imam Hussein bin Ali (as). Baada ya mapambano ya kishujaa, Zaid bin Ali aliuawa shahidi katika mji wa Kufa nchini Iraq. Harakati ya mapambano ya Zaid ni miongoni mwa matunda ya mapambano ya Imam Hussein (as) katika medani ya Karbala hapo mwaka 61 Hijria kwani baada ya mapambano ya siku ya Ashuraa kulijitokeza harakati nyingi baina ya Waislamu zilizopigana jihadi kwa lengo la kuuondoa madarakani utawala dhalimu wa Banii Umayyah.                   

زیدبن علی بن الحسین

Siku kama ya leo miaka 100 iliyopita, sawa na tarehe Pili Novemba 1916, Sharifu Hussein mtawala wa Makka na Madina, alijitangaza kuwa mfalme wa tawala zote za Kiarabu. Mtawala huyo kuanzia tarehe 5 mwezi Juni mwaka huo huo na kwa ushawishi wa Uingerea alianzisha mapambano dhidi ya utawala wa Othmaniyah, wakati utawala huo ulikuwa na vita na waitifaki wake katika Vita vya Kwanza vya Dunia. Uingereza ilimuahidi Sharif Hussein kuwa baada ya vita hivyo, ingemtambua rasmi kama mfalme anayejitegemea wa Saudi Arabia. Hata hivyo Uingereza haikutekeleza ahadi yake hiyo na badala yake ikawaunga mkono watawala wa kizazi cha al-Saud dhidi ya Sharif Hussein. Aidha katika kusafisha sura yake chafu kati ya Waarabu, London iliamua kuwapatia ufalme watoto wa Sharif Hussein katika nchi za Iraq na Jordan, chini ya usimamizi wa Uingereza.

Sharif Hussein

Siku kama ya leo miaka 99 iliyopita inayosadifiana na tarehe Pili Novemba mwaka 1917, lilitolewa tangazo la James Balfour. Tangazo hilo lililotolewa na Arthur James Balfour waziri wa mambo ya nje wa wakati huo wa Uingereza liliandaa uwanja wa kuasisiwa utawala haramu wa Israel huko katika ardhi za Palestina zilizokuwa chini ya wakoloni wa Uingereza. Tangazo hilo pia liliipa idhini serikali ya London kuunda utawala wa Kiyahudi katika ardhi za Palestina sanjari na kuitaka serikali hiyo kufanya kila iwezalo kufanikisha jambo hilo. Mwishowe miaka 30 baada ya kutolewa tangazo hilo la kikoloni mnamo mwaka 1948, utawala wa Kizayuni ulianzishwa kwa msaada wa Uingereza na Marekani na kwa kukanyagwa haki zote za wananchi wa Palestina.

Arthur James Balfour

Siku kama ya leo miaka 67 iliyopita Indonesia ilijipatia uhuru wake baada ya kukoloniwa na Uholanzi kwa karne tatu na nusu. Kwa mujibu wa mkubaliano yaliyotiwa saini siku hiyo kati ya Uholanzi na wanamapinduzi wa Indonesia chini ya uongozi wa Dakta Ahmad Sukarno na Ahmad Hata, vikosi vya wakolozi wa Kiholanzi vilitakiwa kuondoka katika ardhi ya Indonesia. Makubaliano hayo yalitiwa saini baada ya miaka minne ya mapambano ya Waindonesia yaliyoanza mwezi Agosti mwaka 1945, ambapo baada ya uhuru wa Indonesia Dakta Sukarno alichaguliwa kuwa rais wa nchi hiyo, na kubakia madarakani hadi mwaka 1965 baada ya kuondolea madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi.

Bendera ya Indonesia

Siku kama ya leo miaka 52 iliyopita Saud bin Abdul Aziz, mfalme wa Saudi Arabia aliondolewa madarakani katika mapinduzi yaliyofanywa na ndugu yake, Faisal bin Abdul Aziz. Faisal alikuwa waziri mkuu wa Saud bin Abdul Aziz na alitumia ujanja kwa ajili ya kupata uungaji mkono wa idadi kadhaa ya wanafamilia wa kizazi cha Aal Saud na maulama wa Kiwahabi. Wakati Mfalme Saud alipokwenda nje ya nchi kwa ajili ya matibabu, Faisal aliwapa wafuasi wake ndani ya kizazi cha Aal Saud nyadhifa muhimu kama uongozi wa Gadi ya Taifa na kwa njia hiyo akawa amedhibiti nchi. Mapinduzi hayo yaliungwa mkono na wanasiasa na viongozi wa kidini wa Saudi Arabia na Faisal akawa mfalme mpya wa nchi hiyo. Miaka 11 baadaye Mfalme Faisal bin Abdul Aziz mwenyewe pia aliuawa na ndugu yake. Vita vya kuwania madaraka vimekuwepo siku zote ndani ya kizazi cha watawala wa Aal Saud huko Saudi Arabia.

Saud bin Abdul Aziz

Siku kama hii ya leo miaka 43 iliyopita inayosadifiana na tarehe 12 Aban 1352 Hijria Shamsia, alifariki dunia Ayatullah Mirza Abul Hussan Shaarani arifu, faqihi na msomi mkubwa wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 71. Allamah Mirza Shaarani amekwua mashuhuri zaidi kwa tafasiri ya Qurani Tukufu ya 'Manhaju Swadiqiin'. Licha ya kubobea katika elimu za kidini Msomi huyo pia alikuwa mahiri katika kuzungumza lugha za kigeni kama Kifaransa, Kiingereza na Kiarabu. Mbali na tafsiri ya Qurani Tukufu ya Manhaju Swadiqiin yenye juzuu 10. Ayatullah Shaarani ameandika vitabu vingine kadhaa kikiwemo kile cha Sharh Kifayatil-Usuul. Vilevile alikuwa mahiri katika elimu za mujumu na nyota.

Ayatullah Mirza Abul Hussan Shaarani

 

Tags