Jumamosi, 05 Novemba, 2016
Leo ni Jumamosi tarehe 5 Mfunguo Tano Safar mwaka 1438 Hijria sawa na tarehe 5 Novemba mwaka 2016 Miladia.
Miaka 1377 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria alikufa shahidi huko Sham Ruqqaiyyah binti mdogo wa Imam Hussein as. Ruqaiyyah aliyejulikana pia kwa jina la Fatma bint al Hussein au Fatma mdogo, alikuwa binti wa mwisho wa Imam Hussein na mama yake alijulikana kwa jina la Ummu Is'haq bin Talha. Imam Hussein alikuwa akimpenda sana binti yake huyo kama ambavyo binti huyo pia alikuwa kimpenda sana baba yake. Ruqaiiyah alikuwa pamoja na baba na kaka zake pamoja na ndugu zake wengine katika tukio la Karbala.
Katika siku kama ya leo miaka 72 iliyopita, Dakta Alexis Carrel, mwanabiolojia na mwanafalsafa wa Kifaransa aliaga dunia. Alizaliwa Juni 28 mwaka 1873 katika mji wa Lyon nchini Ufaransa. Mwaka 1912 Dakta Carrel alitunukiwa tuzo ya heshima ya Nobel kutokana na mchango wake mkubwa katika uwanja wa tiba. Alitumia kipindi fulani katika maisha yake kutalii na kuzitembelea nchi mbalimbali zikiwemo za Kiislamu na kushuhudia kwa karibu mila na tamaduni za nchi hizo. Kwa sababu hiyo Dakta Alexis Carrel amesisitiza mno katika maandishi na vitabu vyake juu ya umuhimu na nafasi ya dini na masuala ya kiroho katika maisha ya mwanadamu. Miongoni mwa vitabu hivyo ni kile alichokipa jina la "The Man Unknown" yaani Mwanadamu, Kiumbe Asiyefahamika."
Katika siku kama ya leo miaka 887 iliyopita, alizaliwa huko Mosul moja ya miji ya Iraq, Kamalddeen Abu Imran mashuhuri kwa jina la Ibn Yunus fakihi, tabibu na mwanahisababti wa Kiislamu. Baada ya kukamilisha masomo yake ya awali ya kidini alianza kujihusisha na usomaji wa elimu ya hisabati na baada ya kutabahari katika uga huo alianza kufundisha. Ibn Yunis alihesabiwa kuwa miongoni mwa wanazuoni mahiri katika zama zake. Alikuwa amebobea pia katika uwanja wa fikihi ya madhehebu mbalimbali za kiislamu na dini nyingine za mbinguni, kiasi kwamba, hata Mayahudi na Wakristo walikuwa wakimuendelea kwa ajili ya kufasiriwa Taurati na Injili.
Na siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, wafanyakazi wa redio na televisheni ya Iran walianza mgomo wakiupinga utawala wa Shah. Mgomo huo ulifanyika kwa shabaha ya kuzidisha mashinikizo dhidi ya utawala wa Shah na kuharakisha mwenendo wa kuipindua serikali yake. Siku hiyo hiyo maafisa wa jeshi la Shah walishambulia taasisi za magazeti na vyombo vya habari na kuwatia nguvuni waandishi kadhaa. Hatua hiyo ilipelekea kusitishwa uchapishaji wa magazeti yaliyokuwa yakichapishwa kwa wingi nchini Iran.