Nov 09, 2016 23:34 UTC
  • Alkhamisi, 10 Novemba, 2016

Leo ni Alkhamisi tarehe 10 Safar 1438 sawa na 10 Novemba 2016.

Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilitoa azimio nambari 3379 lililoutambua uzayuni (Zionism) kuwa ni aina fulani ya ubaguzi wa kizazi. Azimio hilo lilitoa pigo kubwa kwa utawala wa Kizayuni wa Israel na kufichua utambulisho halisi wa utawala huo. Azimio hilo la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliikasirisha sana Israel na waungaji mkono wa utawala huo wa kibaguzi hususan Marekani. Tofauti na mafundisho ya Kiyahudi, fikra za uzayuni ambazo zilianzishwa mwishoni mwa karne ya 19 zinawatambua wafuasi wa dini hiyo kuwa ni ndio kizazi bora zaidi ya wengine wote duniani. Kwa mujibu wa fikra hiyo Wazayuni wa Israel wanawatambua watu wa Palestina kuwa ni kizazi dunia na hakiri zaidi na kwa sababu hiyo wanawakandamiza, kuwaua na kuwafukuza katika makazi na nchi yao.

Miaka 52 iliyopita katika siku kama ya leo mwafaka na tarehe 10 Novemba 1964, Leonid Brezhnev alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha CPSU katika Urusi ya zamani na hivyo kuchukua rasmi jukumu la kukiongoza chama hicho. Brezhnev aliendelea kushikilia cheo hicho cha ukatibu mkuu hadi kifo chake mwaka 1982. Katika kipindi chake cha uongozi, Umoja wa Usovieti ulipata nguvu zaidi kijeshi lakini pia ulikumbwa na matatizo mengi ya kiuchumi. Viongozi wa kikomunisti waliokuja baada yake walisema matatizo aliyoyaacha Leonid Brezhnev ndiyo yaliyopelekea Umoja wa Usovieti kuporomoka na kuvunjika kabisa mwaka 1991.

Miaka 533 iliyopita muwafaka na leo, alizaliwa Martin Luther mpigania mageuzi ya kidini wa Kijerumani. Luther alikuwa padri wakati akiwa kijana. Mitazamo ya Martin Luther kuhusuiana na dini ya Kikristo ilitofautiana na baadhi ya mitazamo ya Papa na viongozi wa ngazi ya juu wa kanisa na kuanzia mwaka 1517, Luther alidhihirisha mapambano na upinzani wake dhidi ya dhulma na ukandamizaji wa kanisa. Martin Luther alipinga waziwazi agizo la Papa wa Kanisa Katoliki kwa kuifasiri Injili kwa lugha ya Kijerumani na akaanzisha harakati ya kiprotestant dhidi ya kanisa hilo.

Siku kama ya leo miaka 104 iliyopita yaani tarehe 10 Novemba 1912, Morocco alianza kukoloniwa na Ufaransa na Uhispania. Kabla ya hapo nchi hiyo inayopatikana kaskazini mwa Afrika ilikuwa ikikaliwa na madola mbalimbali kama vile dola la Othmania, Roma na Italia. Baadaye Uhispania na Ufaransa zilianza kukosana na muungano wao katika kuikoloni Morocco ukavunjika. Ufaransa iliendelea kuikoloni nchi hiyo na baada ya muda usio mrefu, wananchi wakaanzisha mapambano yao dhidi ya Wafaransa. Hatimaye mapambana hayo yalipata ushindi na Morocco ikajipatia uhuru wake 1956.

Siku kama ya leo miaka 217 iliyopita yaani tarehe 10 Novemba mwaka 1899, kulitokea mapinduzi ya kijeshi yaliyofahamika kwa jina la Brumaire nchini Ufaransa. Brumaire lilikuwa jina la mwezi wa pili katika kalenda ya mapinduzi ya Ufaransa ambao unaenda sambamba na mwezi wa Novemba kwa kalenda ya Milaadia. Siku hiyo Napolione Luis Banaparte ambaye alikuwa akijihusisha na ushindi dhidi ya nchi za kaskazini mwa Afrika na Misri, alirejea kwa siri nchini kufuatia mwaliko wa kiongozi mmoja wa utawala wa Ufaransa. Aidha Luis Banaparte kwa kutegemea uungaji mkono wa askari jeshi na Bunge la nchi hiyo alifanikiwa kupindua utawala uliokuwepo nchini Ufaransa na kuanza kuiongoza rasmi nchi hiyo.

Siku kama ya leo miaka 175 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 10 Safar 1263 Hijria, alifariki dunia Mulla Jaafar Shariatmadar Tehrani, mwandishi na msomi mkubwa wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 1197 Hijria na alipitisha kipindi cha ujana wake akitafuta elimu. Msomi huyo aliamua kurejea nchini Iran baada ya Daud Pasha, kamanda wa utawala wa Othmania kuuzingira mji mtakatifu wa Karbala nchini Iraq. Mbali na kuhudumu kama jaji, Mulla Jaafar Tehrani alikuwa hodari katika kutunga na kusoma mashairi. Hata hivyo umashuhuri mkubwa zaidi wa msomi huyo unatokana na vitabu vyake kadhaa katika taaluma za fiqhi, usulul fiqhi, teolojia na maadili. Vitabu mashuhuri zaidi vya mwanazuoni huyo wa Kiislamu ni "Al Shariul Kabiir", "Safinatun Najat", "al Masabiih" na "al Barahinul Qaatwia".

Na tarehe 10 Novemba mwaka 1981 wakati wa vita vya Saddam Hussein dhidi ya Iran, Ufaransa na Iraq zilitiliana saini mkataba wa mauzo ya silaha uliokuwa na thamani ya dola bilioni moja. Mkataba huo ulikuwa moja kati ya mikataba kadhaa ya mauzo ya silaha baina ya Ufaransa na utawala wa dikteta wa zamani wa Iraq wakati wa mashambulizi ya Iraq dhidi ya Iran. Ufaransa ilikuwa bega kwa bega na utawala wa Saddam Hussein tangu mwanzoni mwa mashambulizi na uvamizi wa Iraq dhidi ya Iran na ilihesabiwa kuwa muuzaji mkubwa wa pili wa silaha kwa utawala wa dikteta Saddam Hussein baada ya Russia. Silaha hizo zilijumuisha ndege za kisasa za kivita, makombora ya aina mbalimbali, vifaru, mizinga na aina nyingine za zana za kivita. Ufaransa pia ilimsaidia Saddam Hussein katika kutengeneza silaha za kemikali. Vilevile iliupatia utawala wa Iraq mkopo wa dola bilioni 5 wakati wa vita vyake dhidi ya Iran na imekataa kulipa deni la dola bilioni moja kwa Iran.