Nov 11, 2016 23:47 UTC
  • Jumamosi, 12 Novemba, 2016

Leo ni Jumamosi tarehe 12 Mfunguo Tano Safar 1438 Hijria sawa na tarehe 12 Novemba 2016 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 98 iliyopita yaani Novemba 12 mwaka 1918, utawala wa kifalme ulifikia tamati nchini Austria na kuanza kipindi cha utawala wa Jamhuri baada ya kushindwa utawala wa Austria na Hungary katika Vita vya Kwanza vya Dunia na kutengana nchi hizo mbili. Mfalme wa mwisho wa Austria, Charles wa Kwanza ambaye alitawazwa kuwa mfalme wa nchi hiyo tarehe 21 Novemba mwaka 1916, alijiuzulu uongozi siku moja tu baada ya kutiwa saini makubaliano ya kusimamisha Vita vya Kwanza vya Dunia hapo tarehe 11 Novemba mwaka 1918 na kuomba hifadhi nchini Uswisi.

Miaka 60 iliyopita katika siku kama ya leo, askari wa utawala haramu wa Israel walifanya mauaji mengine ya umati dhidi ya Wapalestina wasio na hatia katika kambi kubwa ya Wapalestina mjini Rafah huko katika Ukanda wa Gaza. Jinai hiyo ilifanyika siku chache tu baada ya kutangazwa usitishaji vita baina ya Israel, Ufaransa na Uingereza dhidi ya Misri. Hujuma hiyo ya kinyama ilisababisha mauaji ya Wapalestina 110, wakiwemo wanawake na watoto na kujeruhi wengine wapatao 1,000.

Mauaji ya umati ya Wapalestina mikononi mwa Wazayuni

Katika siku kama ya leo miaka 51 iliyopita, Ustadh Said Nafisi mwanafasihi, mwandishi na mhakiki mkubwa wa Kiirani aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 71. Baada ya kumaliza masomo yake ya kati alielekea nchini Ufaransa na kusoma masomo yake ya juu katika taaluma ya sheria na Sayansi ya Siasa. Baada ya kuhitimu masomo yake Ustadh Said Nafisi alirejea nchini Iran na kuanza kufundisha katika vyuo vikuu mbalimbali hapa nchini. Said Nafisi ameacha athari nyingi za vitabu alivyoalifu na kutarjumu ambavyo ni zaidi ya 180.

Said Nafisi

Na miaka 20 iliyopita katika siku kama ya leo aliaga dunia Ayatullah Sayyid Morteza Pasandideh kaka wa Imam Ruhullah Khomeini. Alisoma masomo ya awali ya kidini kwa maulama na wanazuoni wa mji wa Isfahan na kushiriki masomo ya elimuu ya juu ya kidini kwa maustadhi mashuhuri wa zama hizo.  Baadaye alirejea katika mji wa Khomein na kujishuhulisha na ufundishaji wa fikihi, usuul na masomo mengine. Ayatullah Pasandideh anayejulikana kama alimu na mujahidi, kipindi fulani alibaidishwa kutokana na upinzani wake kwa utawala wa kifalme wa wakati huo wa Reza Khan na kusimama kwake kidete dhidi ya utawala huo.

Ayatullah Sayyid Morteza Pasandideh