Jumatatu, 14 Novemba, 2016
Leo ni Jumatatu tarehe 14 Safar 1438 Hijria sawa na Novemba 14, 2016.
Siku kama ya leo miaka 483 iliyopita ardhi ya Ecuado iliyoko Amerika ya Kusini ilivgunduliwa na Uhispania na kuanza kukaliwa nchi hiyo. Kwa karne tatu nchi hiyo ilitawaliwa na kukoloniwa na Uhispania, lakini mnano mwaka 1822 Milaadia wanaharakati wa kupigania uhuru wa nchi hiyo wakiongozwa na Simon Bolivar waliikomboa Ecuador na kuiunganisha na Shirikisho Kubwa la Colombia.
Siku kama ya leo miaka 219 iliyopita inayosadifiana na tarehe 14 Novemba mwaka 1897. Charles Lyell mtaalamu wa masuala ya ardhi na mwanasayansi wa Scottland alizaliwa. Lyell alikuwa mtu wa kwanza kuweka misingi na sheria sahihi za kielimu katika masuala ya ardhi.
Miaka 127 iliyopita katika siku kama ya leo alizaliwa Dakta Taha Hussein, mwandishi na mwanafasihi maarufu wa Misri. Dakta Taha Hussein alipokuwa mtoto alipoteza macho yake, lakini uwezo wake mkubwa wa kiakili ulimsaidia kupata elimu ya juu katika vyuo vikuu vya Misri na Ufaransa na kupata shahada ya Uzamivu au PHD. Dakta Hussein ameandika vitabu vingi vya fasihi ya Kirabu na kushika nyadhifa mbalimbali za ngazi za juu za kiutamaduni na kielimu nje na ndani ya Misri. Miongoni mwa vitabi mashuhuri vya msomi huyo ni Hitoria ya "Fasihi ya Waarabu" na "Masiku".
Siku kama ya leo miaka 127 iliyopita, Jawaharlal Nehru mmoja kati ya viongozi wakubwa wa harakati ya mapambano ya India dhidi ya mkoloni Mwingereza alizaliwa huko Allahabad kaskazini mwa India. Nehru alianza mapambano dhidi ya mkoloni Mwingereza baada ya kujiunga na harakati ya kitaifa ya ukombozi wa India. Jawaharlal Nehru alitiwa mbaroni mara kadhaa na kufungwa jela kutokana na mchango na nafasi yake kubwa katika mapambano hayo. Baada ya Mahatma Ghandi kujiunga na harakati ya kitaifa ya India, wanaharakati hao wakiongoza mapambano ya kupigania uhuru ya wananchi wa India walitoa pigo kubwa kwa mkoloni Mwingereza. Hatimaye India ilipata uhuru Agosti 15 mwaka 1947.
Katika siku kama ya leo miaka 300 iliyopita, Gottfried Wilhelm Leibnitz mwanahisabati na mwanafalsafa wa Kijerumani aliaga dunia mjini Hanover akiwa na umri wa miaka 70. Wilhelm Leibnitz alianza kuzisoma kwa bidii na juhudi elimu za falsafa na hisabati akiwa na umri wa miaka 15 alifanikiwa kupata shahada za juu kabisa katika masomo hayo. Elimu na ufahamu mkubwa na mchango aliotoa katika elimu ya hisabati pamoja na vitabu alivyoandika kuhusiana na elimu hizo, ni mambo yaliyomfanya Gottfried Wilhelm Leibnitz awekwe katika faharasa ya wasomi maarufu wa falsafa na hisabati nchini Ujerumani.
Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita, utungaji na upasishaji wa katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ulikamilishwa na Baraza la Wataalamu. Katiba hiyo iliainisha na kuupasisha mfumo wa Kiislamu uliojengeka juu ya misingi ya mafunzo na matukufu ya Kiislamu hasa uadilifu katika jamii na kuheshimiwa haki za binadamu. Baada ya katiba hiyo kuandikwa kulifanyika kura ya maoni ya wananchi wote na katiba hiyo ikapasishwa kwa wingi wa kura za wananchi.
Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, siku chache baada ya kuvamiwa na kutekwa Pango la Ujasusi la uliokuwa ubalozi wa Marekani hapa mjini Tehran, serikali ya Marekani katika radiamali yake kali dhidi ya hatua hiyo ya kimapinduzi, ilifunga na kuzuia fedha za kigeni za Iran katika mabenki yake yote duniani. Kufungwa kwa akaunti za Iran, kulipelekea mashinikizo ya kiuchumi ya serikali ya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuchukua mkondo mpana zaidi. Siku chache kabla ya hatua hiyo, Iran ilikuwa imesimamisha uuzaji wa mafuta yake kwa Marekani kutokana na hatua na misimamo ya chuki ya Washington dhidi ya Jamhuri ya kiislamu ya Iran.

Na siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, alifariki dunia Allamah Muhammad Hussein Tabatabai mwanazuoni, mwanafalsafa na mfasiri mkubwa wa Qur'ani katika zama hizi akiwa na umri wa miaka 80. Mwanazuoni huyo mkubwa alizaliwa katika mji wa Tabriz, kaskazini magharibi mwa Iran. Msomi huyo wa Kiislamu alikuwa hodari sana katika elimu za falsafa, irfani, tafsiri ya Qur’ani na vilevile katika masuala ya fasihi, hisabati na fiqihi. Allamah Tabatabai ameandika vitabu vingi na miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni tafsiri ya Qur'ani ya al-Mizan.