Nov 15, 2016 23:27 UTC
  • Jumatano, 16 Novemba, 2016

Leo ni Jumatano tarehe 16 Safar 1438 Hijria sawa na Novemba 16, 2016.

Siku kama ya leo miaka 70 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 16 Novemba mwaka 1946, kwa mara ya kwanza ilitengenezwa mvua bandia. Mvumbuzi wa mvua hiyo aliyekuwa mtaalamu wa masuala ya hali ya hewa wa Marekani akishirikiana na mwanakemia mmoja wa nchi hiyo, walitumia gesi ya kaboni na hewa katika kutengeneza mvua hiyo. Mvua bandia hutumiwa katika maeneo yenye ukame au yenye uhaba wa mvua.

Mvua

Tarehe 16 Novemba mwaka 1945 katika siku kama hii ya leo, vikosi vya jeshi la Ufaransa viliishambulia Vietnam na wananchi wa nchi hiyo wakaanza mapambano ya muda mrefu kwa ajili ya kuikomboa nchi hiyo. Baada ya Ufaransa kuikoloni Vietnam kwa kipindi cha karne moja, wakati wa Vita vya Pili vya Dunia Japan iliidhibiti nchi hiyo. Japan iliondoka Vietnam baada ya kushindwa katika vita hivyo, na Vietnam ikavamia tena na Ufaransa hadi wananchi walipofanikiwa kuwafukuza wavamizi hao nchini humo hapo mwaka 1954 chini ya uongozi wa Ho Chi Minh.

Bendera ya Vietnam

Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita ulianzishwa tena uhusiano wa Iran na Libya. Uhusiano huo ulikatwa kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini. Sababu ya kukatwa uhusiano huo ni msimamo wa kiongozi wa zamani wa Libya Kanali Muammar Gaddafi aliyeitambua serikali ya Shah nchini Iran kuwa ilikuwa tegemezi kwa ubeberu wa Marekani na kwamba ilitanguliza mbele maslahi ya nchi za Magharibi na utawala ghasibu wa Israel kuliko maslahi ya nchi za Kiarabu na Wapalestina.

Na tarehe 26 Aban miaka 32 iliyopita aliuawa shahidi Meja Jenerali Mahdi Zainuddun aliyekua kamanda wa kikosi cha 17 cha Ali bin Abi Twalib katika vita vya miaka 8 vya kujitetea kutakatifu. Jenerali Zainuddin ambaye alikuwa miongoni mwa makamanda wa ngazi za juu wa Iran katika mapambano ya kukabiliana na wavamizi wa kibaath na na dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein, alizaliwa katika mji wa Khorramabad katika mkoa wa Loristan hapa nchini mwaka 1338 Hijria Shamsia. Baada ya ushindi wa Mapindzi ya Kiislamu, shahidi Zaunuddin alianza shughuli zake katika taasisi ya jihadi ya Ujenzi na kisha akawa mwanachama rasmi katika Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Hadi anauwa shahidi Meja Jenerali Mahdi Zainuddin alikuwa miongoni mwa makanda wakuu wa heshi hulo.