Nov 18, 2016 01:01 UTC
  • Ijumaa tarehe 18 Novemba, 2016

Leo ni Ijumaa tarehe 18 Safar 1438 Hijria sawa na 18 Novemba, 2016.

Miaka 1401 iliyopita yaani mwaka 37 Hijria, kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi, Uwais al Qarani, mmoja wa tabiina watukufu na wafuasi watiifu wa Imam Ali bin Abi Talib (as) aliuawa shahidi katika vita vya Siffin. Uwais aliishi katika eneo la Qaran huko Yemen na hakufanikiwa kuonana na Mtume (saw) kutokana na kumuuguza mama yake aliyekuwa mgonjwa. Hata hivyo Mtukufu Mtume daima alikuwa akimtaja kwa wema na kumuombea dua Uwais. Baada ya kufariki dunia Mtume (saw), Uwais al Qarani alikuwa miongoni mwa masahaba wa karibu wa Imam Ali bin Abi Talib. Alipigana katika vita vya Siffin vilivyotokea kati ya jeshi la Imam Ali (as) na Muawiya bin Abi Sufian na akauawa shahidi katika vita hivyo. Haram ya Uwais al-Qarani inapatikana katika mji wa ar-Raqqah, Syria.

Tarehe 28 Aban miaka mitatu iliyopita kundi la kigaidi na kitakfiri la Batalioni ya Abdullah Azzam chini ya uongozi wa gaidi wa Saudi Arabia, Maajid al Maajid lilishambulia ofisi ya ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Beirut kwa kutumia magaidi mawaili waliojilipua kwa mabomu. Mashambulizi hayo mawili yaliyofuatana yaliua shahidi watu 23 akiwemo Mwambata wa Jamhuri ya Kiislamu mjini Beiruti, Hujjatul Islam Walmuslimin Ibrahim Ansari na mke wa mwanadiplomasia mwingine wa Iran. Watu wengine 160 walijeruhiwa. Baada ya mashambulizi hayo ya kigaidi kiongozi Msaudi wa kundi hilo Maajid al Maajid alikamatwa lakini kabla ya kutoa taarifa yoyote aliuawa katika mazingira ya kutatanisha akiwa katika hospitali ya kijeshi mjini Beirut na mwili wake ukakabidhiwa kwa maafisa wa Saudi Arabia.

Shambulizi la kigaidi dhidi ya ubalozi wa Iran mjini Beiruti

Siku kama ya leo miaka 53 iliyopita Kanali Abdul Salam Arif alishika hatamu za uongozi nchini Iraq baada ya kufanya mapinduzi ya umwagaji damu. Ikulu ya Rais na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iraq zilishambuliwa kwa mabomu na kupelekea kuuawa Abdul Karim Kasim aliyekuwa Rais wa nchi hiyo. Itakumbukwa kuwa, Abdul Karim Kasim naye aliingia madarakani mwaka 1958 baada ya kufanya mapinduzi ya umwagaji yaliyohitimisha utawala wa Kifalme nchini humo.

Kanali Abdul Salam Arif

Miaka 60 iliyopita na katika siku kama ya leo yaani tarehe 18 Novemba mwaka 1956, nchi ya Morocco ilipatia uhuru. Kabla ya hapo ardhi hiyo ilikuwa chini ya tawala na mataifa mbalimbali. Hata hivyo kufuatia kuenea dini Tukufu ya Kiislamu katika maeneo mbalimbali duniani, yakiwemo maeneo ya kaskazini mwa Afrika, ardhi ya Morocco nayo ikawa miongoni mwa ardhi za utawala wa Kiislamu. Mwaka 1921 Ufaransa iliidhibiti Morocco hadi mwaka 1956 wakati nchi hiyo ilipojitangazia uhuru.

Bendera ya Morocco

Katika siku kama ya leo miaka 177 iliyopita, duru ya pili ya mapambano ya wananchi wa Algeria dhidi ya mkoloni Mfaransa ilianza kwa uongozi wa Abdul Qadir bin Muhyiddin. Mwaka 1830 Ufaransa iliishambulia kijeshi Algeria ikitaka kuikalia kwa mabavu nchi hiyo. Abdul Qadir akiwa na wapiganaji wake 50,000 alifanikiwa kukabiliana na mashambulio hayo hadi mwaka 1847. Hatimaye alishindwa na kuchukuliwa mateka.

Bendera ya Algeria

Siku kama ya leo miaka 113 iliyopita ulitiwa saini mkataba wa Mfereji wa Panama kati ya Marekani na Jamhuri ya Panama. Kwa mujibu wa mkataba huo mfereji huo ulikodishwa milele kwa Marekani mkabala wa Panama kupewa dola milioni 10 taslimu na dola laki mbili na nusu kila mwaka. Baadaye wananchi wa Panama walianzisha mapambano ya kupinga mkataba huo na hatimaye wakailazimisha Marekani kutazama upya kipengee cha kukodishwa mfereji huo milele. Kwa msingi huo mwaka 1978 Jimmy Carter na Jenerali Omar Efraín Torrijos viongozi wa wakati huo wa Marekani na Panama walitia saini mkataba mpya ambao kwa mujibu wake mfereji wa Panama ulirejeshwa chini ya mamlaka kamili ya nchi hiyo mwishoni mwa mwaka 1999.

Mfereji wa Panama

Siku kama ya leo miaka 54 iliyopita alifariki dunia msomi na mwanafizikia wa Denmark, Niels Bohr, akiwa na umri wa miaka 82. Bohr alizaliwa mwaka 1885 na kuvutiwa mno na elimu ya hisabati. Msomi huyo alifanya uchunguzi na uhakiki mkubwa katika elimu hiyo.

Niels Bohr pia alifanya uhakiki katika masuala ya atomu na mwaka 1945 alitunukiwa Tuzo ya Nobel katika medani ya fizikia kutokana na uvumbuzi wake katika masuala ya atomu.

Niels Bohr

Na katika siku kama ya leo miaka 229 iliyopita Louis Daguerre mchoraji, mvumbuzi na mtaalamu wa elimu wa fizikia wa Kifaransa alifariki dunia. Mwaka 1789 mtaalamu huyo alifanikiwa kuvumbua mambo kadhaa. Miongoni mwa uvumbuzi muhimu wa Louis Daguerre ni ule wa mwaka 1839 ambapo alifanikiwa kuvumbua camera ya kupigia picha na kwa kutumia camera hiyo akapiga picha ya kwanza iliyokuwa ikionekana vizuri.

Louis Daguerre