Nov 23, 2016 04:21 UTC
  • Jumatano, Novemba 23, 2016

Leo ni Jumatano tarehe 23 Safar 1438 hijria, sawa na tarehe 23 Novemba 2016 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipasisha suala la kuundwa nchi huru ya Palestina. Suala la Palestina lilikuwa miongoni mwa mambo ya mwanzo kabisa kujadiliwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Hata hivyo maazimio mengi ya Umoja wa Mataifa yamekuwa yakiathiriwa na nchi kubwa zinazowaunga mkono Wazayuni wa Israel na utawala huo ulitumia moja ya maazimio hayo hapo tarehe 14 Mei 1948 kuanzisha dola haramu la Israel katika ardhi ya Palestina.

Siku kama ya leo miaka 16 ilioyopita alifariki dunia mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Ayatullah Sayyid Mahdi Rouhani. Alizaliwa mwaka 1303 Hijria Shamsia katika familia ya kidini katika mji mtakatifu wa Qum nchini Iran na baada ya masomo ya mwanzo alielekea Karbala nchini Iraq kwa ajili ya elimu ya juu. Alifanya utafiti mkubwa kuhusu dini na madhehebu mbalimbali na kuwa gwiji katika taaluma hiyo. Wakati wa harakati za Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, Ayatullah Rouhani alikuwa bega kwa bega na wananchi wa Iran katika mapambano yao dhidi ya utawala wa kifalme wa Shah wakiongozwa na hayati Imam Khomeini. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu vingi vikiwemo vile vya Firqatus Salafiyyah", "Buhuth Ma'a Ahlisunna Wassalafiyyah" na "Firaq wa Madhahibu Islamiyyah".

Tarehe 23 Novemba miaka 40 iliyopita, alifariki dunia André Malraux mwandishi na msanii maarufu wa Ufaransa. Malraux alizaliwa mwaka 1901 mjini Paris na katika ujana wake alikwenda nchini China na India zilizokuwa chini ya ukoloni wa Ufaransa na kujishughulisha na mapambano dhidi ya ukoloni wa nchi yake huko Mashariki mwa Asia. Wakati akirejea katika safari yake hiyo, aliandika kitabu maarufu kwa jina la ‘Hatma ya Mwanadamu.’ Katika vita vya ndani nchini Uhispania, Malraux alishirikiana na wapigania uhuru wa nchi hiyo, huku katika Vita vya Pili vya Dunia akitiwa mbaroni mara mbili na askari wa Kinazi na kutoroka. André aliyekuwa akipinga vita na umwagaji damu, hali kadhalika alitetea pia uhuru wa mwanadamu. ‘Vilio vya Ukimya’, ‘Ushawishi wa Magharibi’, ‘Tumaini la Mwanadamu’ na ‘Washindi’ ni miongoni mwa vitabu vilivyoandikwa na msanii huyo wa Kifaransa.

Miaka 110 iliyopita katika siku kama ya leo ambayo ni sawa na tarehe 3 Azar mwaka 1285 Hijria Shamsia, gazeti la 'Majlis' lililokuwa na kurasa 8 lilianza kuchapishwa nchini Iran. Mhariri Mkuu wa gazerti hilo alikuwa Adib al Mamalik Farahani ambaye alikuwa miongoni mwa waandishi mashuhuri wa zama hizo. Mbali na gazeti hilo kuandika habari za ndani na nje ya nchi, liliakisi pia mazungumzo yote ya Majlisi ya Ushauri yaani Bunge la Iran.

Na miaka 137 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia msomi mkubwa na mtaalamu wa fiq'hi wa Kiislamu Sheikh Muhammad Baqir Agha Najafi Isfahani. Sheikh Agha Najafi alizaliwa mnamo mwaka 1234 Hijiria nchini Iran na baada ya kusoma elimu mbalimbali za kidini mjini Isfahan, alielekea Najaf huko Iraq kwa ajili ya kukamilisha masomo yake. Baada ya kurejea kutoka Najaf msomi huyo aliweka makazi yake mjini Isfahan na kujikita katika kufundisha na kuwalea wanafunzi sambamba na kuandika vitabu. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni pamoja na "Lubbul-Fiq'h" na "Lubbul-Usuul."

 

Tags