Jumamosi, Novemba 26, 2016
Leo ni Jumamosi tarehe 26 Mfunguo Tano Safar mwaka 1438 Hijria inayosadifiana na tarehe 26 Novemba 2016 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 8 iliyopita, watu karibu 200 waliuawa na wengine wanaokaribia 300 kujeruhiwa katika mji wa Mumbai nchini India kufuatia mashambulio kadhaa ya kigaidi na mapigano ya siku tatu baina ya vikosi vya usalama na magaidi. Hoteli kubwa mbili na kituo kikuu cha treni katika mji huo wa kibiashara wa Mumbai vililengwa katika mashambulio hayo ya kigaidi. Serikali ya India iliibebesha lawama Pakistan na kuituhumu kwamba, ilihusika katika mashambulio hayo. India ilidai kuwa, magaidi hao walipata mafunzo nchini Pakistan. Hata hivyo Pakistan ilikanusha madai hayo na kutangaza kuwa, iko tayari kushiriki katika uchunguzi wa pamoja na India ili kuwasaka wahusika wakuu wa mashambulio hayo ya kigaidi. ***
Katika siku kama ya leo miaka 73 iliyopita, mkutano wa siku 3 wa viongozi wa Marekani, Uingereza na Umoja wa Sovieti ulifanyika mjini Tehran katika hali ambayo, Iran wakati huo ilikuwa chini ya uvamizi wa majeshi ya nchi hizo. Mkutano wa Tehran ulifanyika baada ya Marekani kuingia katika Vita vya Pili vya Dunia na kuzuka kambi mpya dhidi ya jeshi la Ujerumani. Walioshiriki katika mkutano huo walikuwa Rais Franklin Delano Roosevelt wa Marekani, Waziri Mkuu wa Uingereza, Winston Churchill na Joseph Stalin kiongozi wa wakati huo wa Umoja wa Kisovieti. ***
Na siku kama ya leo miaka 161 iliyopita, Adam Mickiewicz mshairi na mwandishi mkubwa wa Kipoland aliaga dunia katika mji mkuu wa wakati huo wa uitawala wa Othmania Istanbul. Alizaliwa mwaka 1798 na kama alivyokuwa baba yake, Mickiewicz alikuwa mpigania uhuru. Aliishi katika zama ambazo Poland ilikuwa imegawanywa baina ya Russia, Austria na Prussia na alikuwa akifanya harakati ili nchi hiyo iunganishwe tena. Ni kutokana na sababu hiyo Adam Mickiewicz akabaidishiwa nchini Russia. Baada ya miaka sita aliikimbia nchi hiyo na kuelekea Ufaransa na kuanza kujishuhghulisha na ufundishaji wa fasihi ya lugha. Hatimaye mwaka 1855 aliafariki dunia kwa maradhi ya kipindupindu huko Istanbul Uturuki. ***