Jumatatu, 28 Novemba, 2016
Leo ni Jumatatu tarehe 28 Safar 1438 Hijria sawa na Novemba 28, 2016.
Siku kama ya leo miaka 1427 iliyopita inayosadifiana na tarehe 28 Safar mwaka 11 Hijria, alifariki dunia Mtume Mtukufu Muhammad (saw) akiwa na umri wa miaka 63. Kutokana na kuwa na tabia ya ukweli na uaminifu tangu alipokuwa na umri mdogo, Mtume Mtukufu (saw) alipata umashuhuri kwa jina la "Muhammad Mwaminifu". Akiwa na umri wa miaka 40 Mwenyezi Mungu SW alimteua kuwa Mtume Wake, ili aweze kuwalingania watu ibada ya Mungu Mmoja na kuondoa ukabila, dhulma na ujinga. Watu wa dini, madhehebu na mirengo tofauti na hata wale wasiokuwa na dini kabisa wamesema mengi kuhusu shakhsia adhimu ya Nabii Muhammad (saw). Mwandishi wa Ulaya Stanley Lane Poole ameandika kwamba, Mtume Muhammad alipendwa na watu wote na kila aliyemuona, na kwamba hajawahi kuona wala hatamuona tena mtu mithili yake.
Miaka 1388 iliyopita inayosadifiana na tarehe 28 Safar mwaka wa 50 Hijria, aliuawa shahidi Imam Hassan bin Ali bin Abi Twalib al Mujtaba (as) mjukuu wa Mtume Mtukufu (saw). Imam Hassan (as) ni mtoto wa Bibi Fatima al Zahra na Imam Ali bin Abi Talib (as), na alizaliwa mwaka wa 3 baada ya Mtume (saw) kuhamia Madina. Imam Hassan alichukua jukumu zito la kuongoza Umma wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 37 baada ya kuuawa shahidi baba yake. Mjukuu huyo wa Mtume aliuawa shahidi kwa kupewa sumu katika njama iliyopangwa na Muawiya bin Abi Sufiyan.

Siku kama ya leo miaka 259 iliyopita, alizaliwa William Blake mshairi na mchoraji wa Kiingereza. Blake alikuwa na mapenzi na sanaa tangu akiwa mdogo na alipofikisha rika la ubarobaro alijihusisha na kusoma vitabu vya falsafa na mashairi. Athari za mshairi huyo zilikuwa zikipingana wazi na kanisa, hali ambayo iliwakasirisha mno viongozi wa dini ya Kikristo na watawala wa Uingereza. Hadi anaaga dunia mwaka 1827, msomi huyo wa Uingereza alikuwa ameandika vitabu 13. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni The Marriage of Heaven and Hell, The Tiger, The Chimney Sweeper na The Lamb.
Tarehe 28 Novemba mwaka 1820 alizaliwa Friedrich Engels mwanafalsafa mashuhuri wa Ujerumani. Alikuwa rafiki na mshirika wa karibu wa mwanafalsafa mwingine wa Ujerumani yaani Karl Marx. Engels alifuatiliwa na kusakwa na vyombo vya dola kutokana na harakati zake za kisiasa na mwaka 1850 alikimbilia nchini Uingereza. Engels na Karl Marx walitayarisha Manifesto ya Ukomonisti iliyotangazwa na vyama vya kikomonisti katika mkutano wao wa kwanza mnamo mwaka 1848. Baada ya Karl Marx, Friedrich Engels alikuwa na nafasi muhimu katika kujitokeza nadharia ya ukomonisti.
Katika siku kama ya leo miaka 104 iliyopita, nchi ya Albania ilipata uhuru wake. Nchi hiyo ilikuwa huru miaka mingi kabla ya kuzaliwa Nabii Issa Masih AS, lakini baada ya kuasisiwa ufalme wa Roma ilikaliwa kwa mabavu na utawala huo. Mwaka 1501 Albania ilidhibitiwa na utawala wa Othmaniya. Mwanzoni mwa karne ya 19 utawala huo ulidhoofika na kupoteza nchi za Balkan ilizokuwa ikizitawala na kwa juhudi za wapigania uhuru, hatimaye mwaka 1912 Albania ikajipatia uhuru.
Miaka 56 iliyopita katika siku kama ya leo, Mauritania ilitangaza rasmi uhuru wa nchi hiyo. Mauritania ilikuwa ikikoloniwa na Ureno tangu karne ya 15 Miladia. Baadaye Uholanzi na Uingereza ziliivamia nchi hiyo na mwaka 1903 Mauritania ikawa koloni la Ufaransa. Katika nusu ya pili ya karne ya ishirini Miladia, wananchi wa Mauritania walishiriki kura ya maoni wakitaka kuasisiwa utawala wa Jamhuri yenye mamlaka ya ndani. Hatimaye mwaka 1960 Mauritania ilipata uhuru kamili baada ya kusainiwa makubaliano kati yake na serikali ya Ufaransa.
Miaka 22 iliyopita katika siku kama ya leo alifariki dunia Ayatullah Muhammad Ali Araki, mmoja wa marjaa wakubwa wa taqlidi wa Waislamu akiwa na umri wa miaka 103. Mwanzuoni huyo wa Kiislamu alizaliwa katika mji wa Arak katikati mwa Iran na kujifunza elimu ya dini kwa maulamaa wakubwa hususan Ayatullahil Udhma Hairi. Ayatullah Muhammad Ali Araki alifundisha katika chuo kikuu cha kidini cha Qum kwa kipindi cha miaka 35 na kulea wanazuoni na wasomi hodari. Mwanazoni huyo mkubwa wa Kiislamu amezikwa katika Haram tukufu ya Maasuma (as) katika mji mtakatifu wa Qum.
Siku kama ya leo miaka 6 iliopita, Madakta Majid Shahriyari na Fereydun Abbasi waliokuwa wahadhiri wa Fizikia ya Nyuklia wa Iran walilengwa katika mashambulio mawili tofauti ya kigaidi mjini Tehran. Dakta Abbasi alijeruhiwa ambapo Dakta Majid Shahriyari Mhadhiri wa Chuo Kikuu, Mwanafizikia na Msomi wa Nyuklia wa Iran aliuawa shahidi katika shambulio hilo. Magaidi waliofanya jinai hiyo walitiwa nguvuni na kukiri kwamba walishirikiana na shirika la ujasusi la Israel MOSSAD kutekeleza jinai hiyo.
