Nov 28, 2016 23:33 UTC
  • Jumanne, 29 Novemba, 2016

Leo ni Jumanne tarehe 29 Safar 1438 Hijria sawa na Novemba 29, 2016.

Siku kama ya leo 496 iliyopita, Ferdinand Magellan baharia wa Kihispania alifanikiwa kuvuka mkono bahari ambao leo hii umepewa jina lake yaani Lango Bahari la Magellan na akafika katika bahari ya Pacific kupitia bahari ya Atlantic. Wakati huo Ferdinand Magellan alikuwa akijishughulisha na masuala ya uvumbuzi wa baharini katika pwani ya Amerika ya Kusini.

Katika siku kama ya leo miaka 73 iliyopita, Harakati ya Ukombozi ya Kupambana na Ufashisti iliundwa nchini Yugoslavia chini ya uongozi wa Josip Broz Tito. Wapiganaji wa harakati hiyo walitoa pigo kubwa kwa wanajeshi wa Ujerumani wakati Yugoslavia ilipokuwa ikikaliwa kwa mabavu na jeshi la Ujerumani. Mwaka 1944 wapiganaji wa harakati ya ukombozi ya kupambana na Ufashisti nchini Yugoslavia waliwafukuza nchini mwao wanajeshi vamizi wa Ujerumani kwa kusaidiwa na jeshi Jekundu la Urusi ya zamani.

Josip Broz Tito

Miaka 69 iliyopita katika siku kama ya leo, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliunga mkono kwa wingi wa ushindi mdogo suala la kugawanywa ardhi za Palestina baina ya serikali mbili yaani ya Palestina na ya Kiyahudi. Uamuzi huo usio wa kiadilifu na usio wa kimantiki ulichukuliwa chini ya ushawishi wa serikali za Magharibi hususan Marekani na Uingereza.

Siku ya Kimataifa ya Kushikamana na Watu wa Palestina

Na tarehe 29 Safar miaka 1121 iliyopita aliaga dunia Abu Abdullah Muhammad bin Jabir bin Sinan ambaye alikuwa mwanahesabati mkubwa na mashuhuri wa Kiislamu. Muhammad bin Sinan alikuwa miongoni mwa wanafalsafa, wanajimu na wataalamu wakubwa na gwiji wa nyota wa Kiislamu. Hakuwa na mfano katika elimu ya hisabati katika zama hizo. Msomi huyo wa Kiislamu alizaliwa nchini Misri na alitumia muda wa miaka 40 kufuatilia sayari na nyota. Abu Abdullah bin Sinan alifanikiwa kuainisha wakati halisi wa mwaka wa jua na ameandika vitabu kadhaa kama vile Taadilul Kawakib na Miqdarul Ittisalat.

Abu Abdullah Muhammad bin Jabir bin Sinan