Dec 06, 2016 00:09 UTC
  • Jumanne tarehe 6 Disemba 2016

Leo ni Jumanne tarehe 6 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1438 Hijria sawa na Disemba 6, 2016.

Miaka 834 iliyopita katika siku kama ya leo alizaliwa Jalaluddin Muhammad Balkhi maarufu kwa jina la Maulawi, mshairi mkubwa wa Iran katika mji wa Balkh ambao ni moja kati ya miji ya Iran ya wakati huo. Maulawi alihesabiwa kuwa mshairi mkubwa na maarufu zaidi katika karne ya 9 Hijria Shamsia na miongoni mwa wanafikra na wachamungu wakubwa katika ulimwengu wa Kiislamu. Baada ya muda Maulawi alihamia katika mji wa Konya akiandamana na baba yake. Baadaye alielekea Syria kwa ajili ya masomo ya juu. Miongoni mwa vitabu muhimu zaidi vya Maulawi ni Mathnawi Maulawi, Fihi ma Fihi, Maktubat Maualana na Rabaiyat. Malenga huyo mkubwa wa Kiirani alifariki dunia mwaka 672 Hijria Shamsia. 

Jalaluddin Muhammad Balkhi

Siku kama ya leo miaka 63 iliyopita, inayosadifiana na 16 Azar 1332 Hijria Shamsia, upinzani wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tehran dhidi ya safari ya Richard Nixon, Makamu wa Rais wa Marekani katika kipindi hicho hapa nchini, ulipelekea wanachuo watatu kuuawa na askari vibaraka wa utawala dhalimu wa Shah. Safari hiyo ilifanyika miezi mitatu na nusu tu baada ya mapinduzi ya Marekani dhidi ya serikali ya Dakta Muswaddeq. Siku ya pili baada ya mauaji hayo, Richard Nixon alitunukiwa shahada ya heshima ya uzamivu wa sheria katika Chuo Kikuu cha Tehran. Kwa mnasaba huo, tarehe 16 Azar kila mwaka huadhimishwa nchini Iran kama "Siku ya Mwanachuo" hapa nchini.

Siku ya Mwanachuo Iran

Siku kama ya leo miaka 24 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 6 Disemba 1992, Msikiti wa Babri ulioko katika mji wa Feizabad katika jimbo la Uttar Pradesh huko nchini India ulibomolewa na Wahindu wenye misimamo ya kufurutu ada. Msikiti huo ulijengwa mwaka 1528 na Dhahirud Deen Muhammad Babri. Kubomolewa Msikiti huo kulipelekea kuzuka mapigano makubwa ya umwagaji damu baina ya Waislamu na Wahindu na Waislamu wengi kuuawa katika mapigano hayo. Mgogoro huo uliendelea hadi tarehe 30 Disemba mwaka 2010 ambapo Mahakama Kuu ya Allah-Abad ya India, ilitoa hukumu ya kuwapatia Waislamu haki ya kuhodhi theluthi moja tu ya msikitu huo na kuwapa Wahidi sehemu iliyobakia. Hukumu hiyo isiyokuwa ya kiadilifu ilipingwa na Waislamu na kutaka suala hilo liangaliwe upya.

Msikiti wa Babri, Feizabad katika jimbo la Uttar Pradesh

Siku kama ya leo miaka 99 iliyopita inayosadifiana na 6 Disemba 1917, nchi ya Finland iliyokuwa chini ya utawala wa Russia ilijipatia uhuru wake. Kuwa jirani Finland na Russia kuliwatia wasi wasi mno viongozi wa Finland, kiasi kwamba, katika karne ya 12 Miladia, waliiomba Sweden iwahami dhidi ya Moscow. Hata hivyo, Wasweden waliikalia kwa mabavu Finland. Mwaka 1721 Russia iliivamia Finland na kudhibiti sehemu ya ardhi ya nchi hiyo. Hatimaye mwaka 1917 vikosi vamizi vya Russia vililazimika kuondoka nchini Finland na nchi hiyo ikajitangazia uhuru.

Bendera ya Finland

Na miaka 238 iliyopita katika siku kama ya leo, sawa na tarehe 6 Disemba mwaka 1778, alizaliwa Joseph Louis Gay-Lussac mwanafizikia na mwanakemia wa Ufaransa. Gay-Lussac amefanya tafiti nyingi na kugundua vitu tofauti katika kipindi cha maisha yake. Miongoni mwa aliyoyagundua mwanakemia huyo ni gesi ya sumu ya halogen, kipimio cha ulevi, hydromita au chombo cha kupimia uzito wa maji na viowevu na kuitambua Chloride na Iodine kama elementi mpya. Miongoni mwa kazi zake muhimu za kisayansi alizofanya mwanakemia huyo ni kuweka kanuni ya kupanuka kwa gesi. Kanuni hiyo iliyopewa jina lake pamoja na la mshirika wake ilijulikana kama Law of Charles and Lussac. Gay-Lussac alifariki dunia mwaka 1850.

Joseph Louis Gay-Lussac