Alkhamisi, 08 Disemba, 2016
Leo ni Alkhamisi tarehe 08 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1438 Hijria sawa na 08 Disemba 2016 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 1178 iliyopita aliuawa shahidi Imam Hassan Askari (as) ambaye ni mmoja wa wajukuu wa Mtume wetu Muhamamd (saw) katika mji wa Samarra nchini Iraq. Imam Askari alizaliwa katika mji mtakatifu wa Madina mwaka 232 Hijria na alishika hatamu za kuongoza Umma baada ya kuuawa baba yake mwema Imam Ali al Hadi (as). Kipindi cha uongozi wa Imam Hassan Askari kilijawa na misukosuko mingi kutokana na kuzaliwa ndani yake Imam wa Zama Mahdi (as). Kwani viongozi wa utawala wa kizazi cha Abbas walikuwa wakichunga mno na kumsaka imam huyo aliyeahidiwa kudhihiri katika aheri zamani. Alisifika kwa elimu, ukarimu na ucha-Mungu. Imam aliuawa shahidi na watawala madhalimu wa Bani Abbas kwa kupewa sumu katika siku kama hii leo.

Miaka 148 iliyopita mwafaka na leo, ulianguka utawala wa Washugani au kwa jina jingine watawala wa kijeshi huko Japan. Kuanguka kwa utawala huo kulipelekea kuanza kwa marekebisho ya kijamii, kisiasa na kiutamaduni nchini humo. Washugani walikuwa moja kati ya makumi ya silsila zenye nguvu huko Japan, walioanzisha utawala wao wa kidikteta tangu karne ya 12 Miladia.
Miaka 113 iliyopita katika siku kama ya leo aliaga dunia Herbert Spencer mwanafikra na mwanafilosofia wa Kiingereza. Spencer aliazaliwa mwaka 1820 Miladia na kujifunza elimu mbalimbali kutoka kwa baba yake. Aidha alijiongezea ujuzi wa kielimu kutokana na juhudi zake za kupenda kutalii mambo. Herber Spencer aliamini kuwa, mtu anaweza kujipatia elimu kwa kushuhudia na kupata uzoefu.
Siku kama ya leo miaka 102 iliyopita yalijiri mapigano ya baharini ya Falklands pambizoni mwa visiwa vya Falklands katika bahari ya Atlantic kati ya Uingereza na Ujerumani. Vikosi vya wanamaji vya Ujerumani vilipigwa vibaya na vile vya Uingereza na kupelekea visiwa hivyo kwa mara nyingine tena kuwa chini ya himaya ya Waingereza.
Miaka 67 iliyopita katika siku kama ya leo, Chian Kai-shek kiongozi wa wapigania uhuru wa China alikimbilia Taiwan akiwa na wafuasi wake wengi baada ya kushindwa na wapiganaji wa chama cha Kikomonisti chini ya uongozi wa Mao Tse Tung na kuunda serikali ya kitaifa ya Uchina. Uungaji mkono wa Marekani kwa kiongozi huyo wakati huo ulipelekea Taiwan kujitenga na Uchina na kiti cha nchi hiyo katika Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama kikapatiwa Taiwan.
Miaka 25 iliyopita katika siku kama hii ya leo, Umoja wa Mataifa ulitoa ripoti na kuutangaza utawala wa Baath wa Iraq kuwa ndio ulioanzisha vita vya miaka minane dhidi ya Iran. Katika siku hiyo, Javier Perez de Cuellar Katibu Mkuu wa wakati huo wa Umoja wa Mataifa alitangaza katika ripoti yake kuwa Iraq iliivamia Iran tarehe 22 Septemba mwaka 1980. Miji na vijiji vingi vya mpakani mwa Iran vilitekwa na kukaliwa kwa mabavu huku wanawake, watoto na wanaume wengi wakiwa wahanga wa vita hivyo vikubwa katika uvamizi huo ambao uliungwa mkono kwa hali na mali na nchi za Magharibi.
Siku kama ya leo miaka 23 iliyopita, Ayatullahil Udhma Sayyid Muhammad Ridha Golpayegani, alimu, fakihi mkubwa na mmoja wa marajii wakubwa wa Kiislamu ulimwenguni alifariki dunia. Alizaliwa mjini Golpayegan moja ya miji ya Iran na kusoma masomo ya dini kwa maustadhi stadi na waliokuwa wametabahari kielimu katika zama hizo akiwemo Ayatullah Hairi. Ayatullah Golpayegani alianza kufundisha katika Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) cha mjini Qum-Iran baada ya kuasisiwa kwake. Mwanazuoni huyo mkubwa ameandika vitabu vingi katika nyuga mbalimbali.