Jumamosi, 10 Disemba, 2016
Leo ni Jumamosi tarehe 10 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1438 Hijria sawa na tarehe 10 Disemba 2016 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1483 iliyopita yaani miaka 45 kabla ya Hijra, alifariki dunia babu yake Mtume, Abdul Muttalib katika mji wa Makka. Mtukufu huyo alikuwa miongoni mwa wakuu wa kabila la Kuraish kabla ya kudhihiri Uislamu na alikuwa hodari mno katika fasihi ya lugha ya Kiarabu. Bwana Abdul Muttalib alikuwa msimamizi na mshika ufunguo wa nyumba tukufu ya al-Kaaba. Aidha babu huyo wa Mtume alikuwa akitayarisha chakula na maji kwa ajili ya watu wanaozuru nyumba hiyo ya Mwenyezi Mungu na kazi hiyo aliirithi kutoka kwa baba yake. Aliheshimu mno mikataba na ahadi zake na kwa sababu hiyo alikuwa na ushawishi mkubwa baina ya watu. Miongoni mwa watoto wa mtukufu huyo ni Abdullah, baba yake Mtume wetu Muhammad (saw) na Abu Twalib, baba yake Imam Ali bin Abi Twalib (as).

Katika siku kama ya leo miaka 1466 iliyopita tarehe 10 Mfunguo Sita Rabiul Awwwal yaani miaka 28 kabla ya Hijra, Mtukufu Mtume Muhammad (saw) alimuoa Bibi Khadija binti Khuwailid (as). Bibi Khadija alikuwa mwanamke sharifu, mwenye imani na maarufu kwa ukarimu wake katika zama za ujahilia na alikuwa maarufu kwa lakabu ya "Twahira" kwa maana ya msafi na mtoharifu. Baada ya kufunga ndoa na Nabii Muhammad (saw) Bibi Khadija alikuwa msaidizi mkubwa na mwenza wa mtukufu huyo katika hatua zote za maisha yake. Alisabilia kila kitu kwa ajili ya Uislamu na Mtume Muhammad (saw). Aidha Bibi Khadija (as) aliishi pamoja na Mtume kipindi cha miaka 25 na daima alikuwa mke mwema na mwenye kujitolea kwa mumewe yaani Mtume Muhammad (saw) Mbora wa Walimwengu.

Miaka 120 iliyopita katika siku kama hii ya leo, alifariki dunia mwanakemia maarufu wa Sweden, Alfred Bernhard Nobel. Nobel alizaliwa mwaka 1833 na kuhamia nchini Russia wakati wa ujana wake. Alfred Nobel alifanikiwa kuvumbua dynamite au baruti baada ya kufanya utafiti mkubwa kwa miaka kadhaa katika uwanja wa sayansi ya kemia. Hata hivyo mada hiyo badala ya kutumiwa kwa matumizi ya amani, ilianza kutumiwa kama kifaa cha kivita. Ni kwa sababu hiyo, ndipo Nobel akatoa pendekezo la kutolewa tuzo kila mwaka kwa shakhsia aliyefanya juhudi kubwa katika uwanja wa kuimarisha amani na usalama duniani. Tuzo hiyo ambayo imepewa jina la mwasisi wake yaani Nobel mwenyewe, hutolewa katika nyanja tano za fizikia, kemia, tiba, fasihi na amani ya kimataifa kwa wasomi waliofanya jitihada kubwa za kuleta amani na mafanikio ya kielimu, uvumbuzi, na mambo mengine makubwa duniani. Hata hivyo uteuzi wa washindi wa tuzo ya Nobel hususan ile ya amani duniani umeathiriwa na ushawishi wa baadhi ya madola makubwa na kuiondoa tuzo hiyo katika mkondo wa asili wa mwanzilishi wake.
Na miaka 68 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 10 mwezi Disemba mwaka 1948, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipasisha Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu na kuidhinisha haki za kimsingi na kijamii za binadamu. Azimio hilo la haki za binadamu lilitayarishwa kwa maelekezo ya Umoja wa Mataifa kupitia jopo la wawakilishi wa nchi kadhaa duniani. Kipengee nambari moja cha azimio hilo kinasisitiza kuwa binadamu wote ni sawa. Licha ya kupasishwa azimio hilo, leo hii vitendo na siasa za madola ya Magharibi hasa Marekani vinakinzana wazi na azimio hilo. Leo hii pia baadhi ya madola hayo ya Magharibi yamekuwa yakilitumia suala la haki za binaadamu kama wenzo wa kuyashinikiza mataifa mengine.