Jumapili, Disemba 18, 2016
Leo ni Jumapili tarehe 18 Mfunguo Sita Rabiul Awwali 1438 Hijria sawa na Disemba 18, 2016.
Siku kama ya leo miaka 1437 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria Qamaria, ilianza kazi ya ujenzi wa Msikiti wa Mtume mjini Madina ambao ni msikiti wa pili kwa utukufu duniani baada ya Masjidul Haram mjini Macca. Mtume (SAW) alitoa amri ya kujengwa msikiti wa Madina baada tu ya kuhamia mjini humo na yeye mwenyewe alishiriki katika ujenzi wake. Kandokando ya msikiti huo kulijengwa vyumba vya Mtume na baadhi ya maswahaba zake. Mtume hakuutumia msikiti kwa ajili ya ibada tu, bali alitumia pia sehemu hiyo kwa ajili ya masuala kama kutoa hukumu baina ya watu, vikao vya mashauriano, mafunzo ya kivita na utatuzi wa masuala mbalimbali ya Waislamu.
Miaka 114 iliyopita katika siku kama ya leo, kituo cha kwanza cha redio duniani kiliasisiwa na Guglielmo Marconi, mvumbuzi na mbunifu wa Kiitalia. Kwa utaratibu huo, kukaweko mawasiliano ya haraka baina ya Ulaya na Amerika. Katika zama hizo redio ilikuwa ikitumiwa zaidi kama chombo cha mafunzo. Marconi alifikia hatua hiyo kutokana na bidii na shauku kubwa aliyokuwa nayo tangu awali ya kufanya utafiti katika uwanja huo.
Miaka 102 iliyopita katika siku kama ya leo, Uingereza iliikoloni rasmi Misri. Inafaa kukumbusha kwamba, wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia, utawala wa Othmania ulikuwa mwitifaki wa madola yaliyokuwa yakiipinga Uingereza yaani Ujerumani na Austria. Uingereza nayo ikiwa na lengo la kukabiliana na kitendo hicho, iliikalia kwa mabavu Misri, ambayo hadi katika kipindi hicho ilikuwa chini ya udhibiti na utawala wa Othmania. Harakati za ukombozi za wananchi wa Misri dhidi ya mkoloni Mwingereza zilizaa matunda mwaka 1922, ambapo nchi hiyo ilijitangazia uhuru wake.
Siku kama ya leo miaka 78 iliyopita msomi wa Ujerumani, Otto Hahn, alifanikiwa kupasua kiini cha atomu, hatua ambayo ilikuwa mwanzo wa zama za atomu. Mtaalamu huyo wa kemia alizaliwa mwaka 1879 huko Frankfurt na kupata shahada ya uzamivu katika taaluma ya kemia. Tangu wakati huo alijishughulisha na utafiti katika taaluma ya fizikia. Baada ya utafiti mkubwa na katika siku kama hii ya leo Otto Hahn alifanikiwa kupasua kiini cha atomu. Hatua hiyo iliibua nishati kubwa ambayo baadaye ilianza kutumika katika vinu na mabomu ya nyuklia. Mwaka 1944 Otto Hahn alitunikiwa tuzo ya Nobel katika taaluma ya kemia.
Tarehe 18 Disemba miaka 37 iliyopita Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipasisha makubaliano ya kufuta aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake. Makubaliano hayo yalikusudiwa kuondoa dhulma zinazofanywa dhidi ya wanawake duniani. Hata hivyo makubaliano hayo, kama yalivyo mengine mengi ya kimataifa, yanatawaliwa na mitazamo ya kimaada ya Magharibi inayosisitiza usawa wa jinsia mbili za mwanamke na mwanaume katika kila jambo. Hii ni katika hali ambayo mwanamke na mwanaume wanatofautiana kimwili na kiroho. Kwa sababu hiyo dini za Mwenyezi Mungu hususan Uislamu zinasisitiza kuwa njia ya kuwakomboa wanawake ni kuwatayarishia mazingira ya uadilifu kwa kutilia maanani uwezo wao wa kimwili na kiroho.