Dec 21, 2016 00:21 UTC
  • Jumatano, Disemba 21, 2016

Leo ni Jumatano tarehe 21 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1438 Hijria sawa na 21 Disemba 2016.

Siku kama ya leo miaka 28 iliyopita, watu 270 walipoteza maisha yao baada ya ndege ya abiria ya Marekani kuripuka katika anga ya Lockerbie huko Scotland. Marekani na Uingereza ziliwatuhumu raia wawili wa Libya kuwa ndio waliotega bomu katika ndege hiyo. Kufuatia mashinikizo ya nchi mbili hizo, mwaka 1992, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliiwekea vikwazo vya mafuta, anga na kijeshi nchi ya Libya, kwa tuhuma za kuwaficha Walibya hao. Hata hivyo kufuatia makubaliano kati ya Washington na serikali ya Tripoli, mwaka 1999 watuhumiwa hao walikabidhiwa kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai yenye makao yake makuu mjini The Hague, Uholanzi ambapo baada ya kesi hiyo mmoja kati ya watuhumiwa hao aliachiliwa huru baada ya kutopatikana na hatia, na wa pili alihukumiwa kifungo cha maisha jela.

Mabaki ya ndege ya abiria ya Marekani, Lockerbie, Scotland

Katika siku kama ya leo miaka 52 iliyopita, Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) iliasisiwa. PLO iliundwa kutokana na makundi manane ya mapambano, taasisi za kielimu, kijamii, kitiba na kiutamaduni. Mwaka mmoja baadaye tawi la kijeshi la Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) la Fat-h lilianza harakati zake. Mwaka 1974, PLO ilikubaliwa kuwa mwanachama mtazamaji katika Umoja wa Mataifa, na hadi mwaka 1982, harakati hiyo ilikuwa na uhusiano rasmi na nchi zaidi ya 100 duniani.

Na siku kama ya leo miaka 192 iliyopita alifariki dunia tabibu na mtaalamu wa masuala ya ardhi wa Uingereza, James Parkinson. Alijifunza tiba kwa baba yake na alikuwa wa kwanza kueleza kwamba ugonjwa wa appendix unaweza kusababisha kifo. Parkinson aligundua ugonjwa wa Parkinson na namna unavyotokea. Kwa sababu hiyo ugonjwa huo ulipewa jina la tabibu huyo. Dalili za ugonjwa huo ni kama vile kutetemeka sana na kwa muda mrefu kwa ulimi, kichwa na mikono na kushindwa kuvuta miguu wakati wa kutembea hususan katika kipindi cha uzeeni na pia kukakamaa misuli katika sehemu yoyote ya mwili. Ugonjwa wa Parkinson unasababishwa na baadhi ya matatizo katika ubongo na hadi kufikia sasa hakuna dawa mujarabu iliyopatikana kwa ajili ya kutibu maradhi hayo.

James Parkinson