Dec 21, 2016 23:30 UTC
  • Alkhamisi, 22 Disemba, 2016

Leo ni Alkhamisi tarehe 22 Rabiul Awwal 1438 Hijria inayosadifiana na Disemba 22, 2016.

Siku kama ya leo miaka 1434 iliyopita, yaani tarehe 22 Rabiul-Awwal mwaka wa 4 Hijiria, kulianza vita kati ya Waislamu na Mayahudi wa kabila la Bani Nadhir baada ya watu wa kabila hilo kufanya njama za kutaka kumuua Mtume Muhammad (SAW). Bani Nadhir ni moja ya makundi matatu ya Mayahudi waliokuwa wakiishi katika vitongoji vya mji wa Madina, ambao kwa mujibu wa mkataba waliotiliana saini na Mtume (SAW), hawakutakiwa kuchukua hatua yoyote iliyo dhidi ya mtukufu huyo na Waislamu kwa ujumla. Baada ya Mayahudi kuvunja mkataba huo, Mtume Muhammad (SAW) aliwaamuru waondoke Madina. Hata hivyo Mayahudi hao ambao tayari walikuwa wamepewa ahadi za kuungwa mkono na wanafiki wa mji huo, hawakuwa tayari kutii amri hiyo. Ni kwa sababu hiyo, ndipo mtukufu Mtume kwa kushirikiana na Waislamu akazizingira ngome za watu hao kwa muda wa siku kadhaa na kuwalazimisha kuondoka katika maeneo yao. 

Mabaki ya ngome ya Mayahudi wa Bani Nadhir

Siku kama ya leo miaka 2162 iliyopita, duru ya tatu na ya mwisho ya vita vya kihistoria na vya umwagaji damu kati ya tawala za kifalme za Carthage na Roma ilimalizika kwa kupata ushindi Waroma na kuanguka utawala wa Wacartharge. Vita vya falme hizo mbili vilijulikana kwa jina mashuhuri la vita vya Punic. Utawala wa kifalme wa Carthage ulikuwa moja kati ya tamaduni kongwe huko kaskazini magharibi mwa Afrika na katika pwani ya bahari ya Mediterrania.

Vita vya tawala za kifalme za Carthage na Roma

Tarehe 22 Disemba miaka 323 iliyopita, ulitokea mtetemeko mkubwa wa ardhi katika kisiwa cha Sicily kusini mwa Italia. Kufuatia zilzala hiyo, miji mitatu mikubwa ya kisiwa hicho iliteketezwa na kusababisha hasara kubwa kwa miji mingine yakiwemo makao makuu ya kisiwa hicho yaani Palermo. Mtetemeko huo wa ardhi unahesabiwa kuwa mkubwa zaidi wa ardhi kuwahi kutokea nchini Italia. Zaidi ya watu elfu themanini walipoteza maisha yao katika janga hilo la kimaumbile.

Siku kama ya leo miaka 377 iliyopita alizaliwa Jean Racine malenga na mwandishi wa michezo ya kuigiza wa Kifaransa. Racine alianza kazi ya uandishi baada ya kujisomea kwa muda fulani na katika ujana wake alipata umashuhuri kutokana na kuandika mchezo wa tanzia alioupa jina la Andromaque.

Jean Racine

Siku kama ya leo miaka 60 iliyopita, Ufaransa na Uingereza zilihitimisha udhibiti wao wa siku 50 dhidi ya bandari ya Port Said ya nchini Misri na kutoa majeshi yao katika bandari hiyo. Inafaa kuashiria hapa kwamba, baada ya utawala haramu wa Israel kufanya mashambulio katika jangwa la Sinai, mashambulio ya pamoja ya anga ya Uingereza na Ufaransa dhidi ya Misri nayo yalianza. Mashambulio hayo, yalipelekea kutokea hasara kubwa dhidi ya Kanali ya Suez. Sababu ya kufanywa mashambulio hayo ambayo baadaye yalikuja kujulikana kwa jina la Vita vya Kanali ya Suel, ni hatua ya Rais Gamal Abdul-Nassir wa Misri kuitangaza kanali hiyo kuwa mali ya taifa. Umoja wa Mataifa uliiunga mkono Misri wakati wa mashambulio hayo na kwa utaratibu huo tawala tatu hizo, yaani Uingereza, Ufaransa na utawala wa Kizayuni wa Israel zikaondoa majeshi yao katika ardhi ya nchi hiyo.

Mfereji wa Port Said mwaka 1880

Siku kama ya leo miaka 27 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 22 Disemba 1989, uliangushwa utawala wa Rais Nicolae Ceausescu wa Romania.

Rais Ceausescu, ambaye pia alikuwa kiongozi wa chama cha Kikomonisti nchini humo, aliuawa kwa kupigwa risasi pamoja na mkewe Elena ambaye alikuwa kiongozi katika serikali ya mumewe, siku tatu tu baada ya kuangushwa utawala wake. Mipango mibovu ya kiuchumi ya Ceausescu tokea mwanzoni mwa muongo wa 1980, ilipelekea kushadidi matatizo ya kiuchumi ya Romania na kuanza kukabiliwa na malalamiko na ukusoaji mkubwa wa wananchi. Mara baada ya jeshi kutangaza uungaji mkono wao kwa wapinzani, Ceausescu na mkewe walitiwa mbaroni na kisha kuuawa walipokuwa katika harakati za kutoroka nje ya nchi.

Rais wa zamani wa Romania Nicolae Ceausescu