Dec 28, 2016 01:49 UTC
  • Jumatano, 28 Disemba, 2016

Leo ni Jumatano tarehe 28 Rabiul Awwal 1438 Hijria sawa na Disemba 28, 2016.

Siku kama ya leo miaka 91 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 28 Disemba 1925 alizaliwa Apolo Milton Obote Rais wa zamani wa Uganda. Obote aliiongoza Uganda kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza mwaka 1962. Aliiongoza Uganda akiwa Waziri Mkuu kuanzia mwaka 1962 hadi 1966. Milton Obote alikuwa Rais wa Uganda kuanzia mwaka 1966 hadi 1971 alpoondolewa madarakani na Idi Amin Dada. Hata hivyo mwaka 1980 alirejea madarakani baada ya Idi Amin kuondolewa uongozi na kuiongoza nchi hiyo hadi mwaka 1985 wakati alipoondolewa madarakani na kulazimika kukimbilia Tanzania na baadaye Zambia. Obote alifariki dunia mwaka 2005 huko Johannesburg, Afrika Kusini kutokana na matatizo ya figo.

Milton Obote

Siku kama ya leo miaka 121 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 28 Disemba 1895 kwa mara ya kwanza katika historia ya sanaa ya filamu, filamu ya kwanza ya kisa ilioneshwa kwenye mkusanyiko wa watu wengi. Filamu hiyo ilitayarishwa na kuandaliwa na ndugu wawili waliojulikana kwa majina ya Auguste na Louis Lumiere. Miaka iliyofuata ilitengenezwa mitambo bora zaidi ya kurekodi na kuonesha filamu na hatua kwa hatua filamu zenye ubora wa juu na za aina mbalimbali zikaanza kuonyeshwa katika nchi mbalimbali duniani.

Auguste na Louis Lumiere

Na siku kama ya leo miaka 242 iliyopita, Joseph Priestley, mwanakemia na mwanafizikia wa Uingereza alifanikiwa kugundua gesi ya oksijeni. Msomi huyo aliishi katika kipindi kilichokuwa maarufu kama zama za dhahabu za kemia. Gesi ya oksijeni ina mchango na nafasi muhimu sana kwa maisha ya mwanadamu na viumbe vingine hai na huingia katika mwili wa mwanadamu wakati wa kupumua na kuchanganyika na chakula. Matokeo ya kazi hiyo ni kuzalishwa nishati ambayo hutumika katika kubakia hai mwanadamu. Joseph Priestley alifariki dunia mwaka 1804.

Joseph Priestley