Dec 28, 2016 23:11 UTC
  • Alkhamisi, 29 Disemba, 2016

Leo ni Alkhamisi tarehe 29 Rabiul Awwal 1438 Hijria sawa na Disemba 29, 2016.

Siku kama ya leo miaka 1838 iliyopita, mji wa Izmir ulioko magharibi mwa Uturuki ya leo, uliharibiwa na kubomolewa vibaya kufuatia mtetemeko mkubwa wa ardhi. Janga hilo lilipelekea nusu ya wakazi wa mji huo kupoteza maisha na wengine wengi kubaki bila makazi. Katika wakati huo mji wa Izmir ulikuwa chini ya utawala wa Roma na ulihesabiwa kuwa moja ya vituo muhimu vya utawala huo katika Asia Ndogo. Hatimaye mji huo ulijengwa upya kwa amri ya Marcus Aurelius mtawala wa wakati huo wa Roma.

Siku kama ya leo miaka 107 iliyopita, alifariki dunia Mir Sayyid Muhammad Baqai, malenga na mkaligrafia mkubwa wa Iran. Si vibaya kuashiria kuwa, Baqai ni miongoni mwa malenga na wataalamu wa kaligrafia waliopata umashuhuri mkubwa katika karne ya 14 Hijiria. Shakhsia huyo alizaliwa mwezi Dhulhijah mwaka 1257 Hijiria, na baada ya kuinukia kiumri alianza kujifundisha mashairi na kaligrafia na kutokea kuwa mashuhuri katika uga huo. Miongoni mwa athari za Mir Sayyid Muhammad Baqai ni pamoja na diwani ya mashairi na kitabu cha ‘Hashimiyyah’.

Mir Sayyid Muhammad Baqai

Siku kama ya leo miaka 93 iliyopita, alifariki dunia alimu na mtaalamu wa elimu ya fiqhi Ayatullah Sayyid Muhammad Firuzabad. Sayyid Firuzabadi Najafi alikuwa ni miongoni mwa wanafunzi wa Akhund Khorasani na Sayyid Muhammad Kadhim Yazdi. Sayyid Firuzabadi alikuwa marjaa wa Waislamu wa Kishia enzi za uhai wake. Mwanazuoni huyo alifariki dunia usiku wa mwisho wa mwezi Rabiul-Awwal mwaka 1345 Hijria mjini Samarra, Iraq na kuzikwa mjini Najaf. Kitabu cha ‘Jaamiul-Kalima fi Hukmil-Libaasil-Mashkuuk’ ni miongoni mwa athari za msomi huyo.

Ayatullah Sayyid Muhammad Firuzabad

Siku kama ya leo miaka 79 iliyopita, mkataba wa kupata uhuru Jamhuri ya Ireland ulitiwa saini baina ya viongozi wa wapigania jamhuri wa Ireland na utawala wa wakati huo wa Uingereza. Hata hivyo kutokana na kuanza Vita vya Pili vya Dunia, serikali ya Uingereza ilikataa kutekeleza mkataba huo. Baada ya vita hivyo, mnamo mwaka 1949, Jamhuri ya Ireland ya Kusini ilijitangazia rasmi uhuru wake toka kwa mkoloni Muingereza. Uhuru wa Ireland ilikuwa natija ya mapambano ya karne nane ya wapigania Jamhuri wa Ireland dhidi ya Uingereza.

Bendera ya Ireland

Miaka 37 iliyopita mwafaka na siku kama ya leo, baada ya serikali ya kijeshi chini ya uongozi wa Jenerali Azhari hapa nchini Iran kushindwa kukandamiza vuguvugu la mapinduzi la wananchi Waislamu, Muhammad Reza Shah mfalme wa mwisho wa Iran, alimteuwa Shapour Bakhtiar kuwa Waziri Mkuu. Reza Shah na Marekani walikuwa na matumaini kwamba, Bakhtiar kwa kutumia nara na kaulimbiu zenye mielekeo ya utaifa na siasa ambazo kidhahiri zilikuwa zikionekana kama za kutaka mabadiliko, angeweza kuzuia harakati ya mapinduzi ya wananchi wa Iran. Hata hivyo, wananchi wanamapinduzi wa Iran walitambua hila na hadaa hiyo, hivyo walimpinga vikali Bakhtiar na kumuita kuwa kibaraka wa mabeberu. Imam Khomeini (MA) alitoa taarifa na kutangaza kuwa, serikali ya Bakhtiar haikuwa halali na kuwataka wananchi wapambane na serikali hiyo.

Shapour Bakhtiar