Ijumaa, 30 Disemba, 2016
Leo ni Ijumaa tarehe 30 Rabiul Awwal 1438 Hijria sawa na Disemba 30, 2016.
Siku kama ya leo miaka 10 iliyopita yaani tarehe 30 Disemba mwaka 2006, Saddam Hussein mtawala katili na dikteta wa zamani wa Iraq, alinyongwa baada ya kutolewa hukumu ya kifo dhidi yake. Saddam alizaliwa mwaka 1937 karibu na mji wa Tikrit uliopo umbali wa kilomita 140 kaskazini mwa mji mkuu wa Iraq, Baghdad na kujiunga na chama cha Baath akiwa na umri wa miaka 20. Dikteta huyo alifanikiwa kuwa naibu wa Ahmad Hassan al Bakr kufuatia mapinduzi yaliyojiri ndani ya chama hicho cha Baath mnamo mwaka 1968. Mwaka 1979 Saddam alikuwa Rais wa Iraq na muda mfupi baada ya kushika madaraka alianzisha vita dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akisaidiwa na madola ya Magharibi na kufanya mauaji na maafa mengi. Kwa msaada wa madola hayo, Saddam alipata silaha za kemikali na kuzitumia dhidi ya mataifa ya Iran na Iraq. Saddam aliendelea kufanya mauaji ya kila aina dhidi ya wananchi wa nchi hiyo na nchi jirani, chini ya himaya na uungaji mkono wa madola ya Magaharibi ikiwemo Marekani.
Siku kama ya leo miaka 69 iliyopita, magaidi wa mashirika mawili ya kijasusi ya Israel walishambulia kitongoji cha Balad al-Sheikh huko Palestina na kuchoma moto nyumba za kitongoji hicho. Moto huo uliwateketeza na kuwaua shahidi Wapalestina 60. Siku hiyo hiyo kundi jingine la kigaidi la Israel lililojulikana kwa jina la Irgun lilidondosha mabomu katikati ya kundi la Wapalestina na kuwaua shahidi 17 kati yao. Mashambulio hayo yaliyoshadidi mwishoni mwa mwaka 1947 na mwanzoni mwa 1948, yalikuwa na lengo la kuandaa mazingira ya kuwafukuza kwa nguvu Wapalestina katika ardhi zao ili kuasisisiwa utawala pandikizi na ghasibu wa Israel katika ardhi hizo.
Na miaka 69 iliyopita katika siku kama hii ya leo, uongozi wa kifalme wa Romania uling'olewa madarakani kufuatia kujiuzulu mfalme wa nchi hiyo na badala yake kukaundwa mfumo wa jamhuri nchini humo. Hadi kufikia mwaka 1862, Romania ilijiamualia utawala wa ndani chini ya utawala wa Othmania na kujipatia uhuru wake taratibu hadi kufikia mwaka 1877. Romania ni moja ya nchi masikini za Ulaya ya Mashariki huku siasa za Kikomonisti zinazotawala, zikishindwa kumaliza matatizo ya nchi hiyo.