Jumamosi, Disemba 31, 2016
Leo ni Jumamosi tarehe Mosi Mfunguo Saba Rabiu Thani 1438 Hijria mwafaka na tarehe 31 Disemba 2016 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 502 iliyopita alizaliwa katika mji mkuu wa Ubegiji Brussels, Andrea Vesalius tabibu na daktari mpasuaji mashuhuri wa nchi hiyo. Umashuhuri wa daktari huyo ulitokana zaidi na juhudi zake alizofanya za kufahamu utendaji wa viungo mbali mbali vya mwili. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana Andrea Vesalius anajulikana kwa jina la baba wa elimu ya anatomia yaani sayansi inayohusu mwili na viungo vyake jinsi vilivyo. Tabibu huyo aliaga dunia mwaka 1564.***
Miaka 325 iliyopita katika siku kama hii ya leo, aliaga dunia Robert Boyle mwanafizikia na mwanakemia wa Ireland. Alizaliwa mwaka 1627 na kuwa chini ya ungalizi na usimamizi wa baba yake ambaye alikuwa akihesabiwa kuwa mmoja wa wanafizikia mashuhuri wa Uingereza. Robert Boyle alisoma masomo yake na kufanikiwa kubobea katika taaluma ya fizikia. Mtaalmu huyo alifanya utafiti mwingi katika uga wa kemia.***
Katika siku kama ya leo miaka 141 iliyopita, Arthur Christensen Mtaalamu wa mambo ya nchi za Mashariki wa Denmark alizaliwa katika mji mkuu wa nchi hiyo Copenhagen. Katika kipindi cha masomo yake, Athur Christensen alikuwa na mapenzi makubwa na masuala ya ardhi za Mashariki hususan Iran. Baadaye alifanya utafiti kuhusiana na historia na fasihi ya Iran. Mtaalamu huyo wa nchi za Mashariki alikuwa akiifahamu vizuri lugha ya kifarsi na aliandika kitabu alichokipa jina la “Iran Katika Zama za Wasasani”. Arthur Christensen aliaga dunia mwaka 1945. ***
Na miaka 17 iliyopita katika siku kama ya leo, Rais Boris Yeltsin wa Russia alijiuzulu na nafasi yake ikachukuliwa na Vladimir Putin. Kipindi fulani Yeltsin alikuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti. Boris Yeltsin alichaguliwa kuwa Rais wa Russia Januari mwaka 1991 na alikuwa akiungwa mkono na madola ya Magharibi. Hata baada ya kusambaratika Umoja wa Sovieti mwishoni mwa mwaka 1991, aliendelea kuwa Rais wa Russia akitumai kwamba, kwa kutumia misaada ya kifedha ya Magharibi angeweza kuiokoa nchi hiyo kutokana na matatizo ya kiuchumi. Kinyume na matarajio yake, viongozi wa madola ya Magharibi hawakutekeleza ahadi zao, hali iliyopelekea siasa za Rais Boris Yeltsin kushindwa. Kushambuliwa kijeshi eneo lililotangaza kujitawala la Chechnia na kukaliwa kwa mabavu ardhi hiyo na majeshi ya Russia, ni miongoni mwa matukio yaliyojiri katika kipindi cha utawala wa Boris Yeltsin nchini Russia.***