Jumatatu, Januari Pili, 2017
Leo ni Jumatatu tarehe 3 Rabiuthani 1438 Hijria sawa na tarehe Pili Januari 2017.
Siku kama ya leo miaka 28 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 13 Dei 1367 Hijria Shamsia, ujumbe wa Imam Ruhullah Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran uliwasilishwa kwa Mikhail Gorbachev kiongozi wa mwisho wa Umoja wa Kisovieti akimlingania dini ya Kiislamu na kumtaka aachane na fikra za Kimaksi. Katika sehemu moja ya ujumbe huo Imam Khomeini alisema: "Tatizo kuu la nchi yako si suala la umiliki, uchumi wala uhuru, bali ni kutokuwa na imani ya kweli juu ya Mwenyezi Mungu; na tatizo hilo ndilo lililoitumbukiza au litakaloitumbukiza Magharibi katika mporomoko wa kimaadili na kuifanya igonge ukuta. Tatizo lenu kubwa ni kupigana vita visivyokuwa na faida dhidi ya Mwenyezi Mungu." Mwishoni mwa ujumbe huo Imam Khomeini alisema: "Tokea sasa Ukomonisti unapaswa kutafutwa kwenye majumba ya makumbusho ya kisiasa duniani; kwani hauwezi kukidhi mahitaji halisi ya mwanadamu." Imam Khomeini alimuusia Gorbachev akisema: "Nakutaka ufanye uchunguzi wa kina kuhusu Uislamu, sio kwa sababu Uislamu na Waislamu wanakuhitajia wewe, hapana, bali kutokana na thamani za hali ya juu na za ulimwengu mzima za dini hiyo ambayo inaweza kuwa wenzo wa ufanisi na uokovu wa mataifa mbalimbali na kukidhi matatizo makubwa ya mwanadamu.
Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 2 Januari 1971, washabiki wa soka wasiopungua 66 nchini Scotland walifariki dunia baada ya kuanguka uzio wa uwanja wa Ibrox Park mjini Glasgow. Watu wengine zaidi ya 200 walijeruhiwa. Maafa hayo yalitokea wakati wa kuchezwa mechi kati ya mahasimu wawili wakuu wa soka nchini humo, klabu ya Celtic na Rangers.
Katika siku kama ya leo miaka 97 iliyopita, alizaliwa Isaac Asimov, mwandishi na mkemia maarufu wa Kimarekani aliyekuwa na asili ya Russia. Asimov alivutiwa mno na elimu ya kemia na akafanikiwa kupata shahada ya uzamivu katika taaluma hiyo. Msomi huyo alifanya utafiti na uhakiki mkubwa wa elimu ya kemia na taaluma nyingine. Hata hivyo jambo lililomtofautisha na wasomi wengine ni uwezo wake wa kuarifisha sayansi mbalimbali kwa lugha nyepesi kwa watu hususan tabaka la vijana. Isaac Asimov ameandika karibu vitabu 270 katika nyanja mbalimbali za sayansi, hisabati na sayansi za jamii. Baadhi ya vitabu vya msomi huyo ni kama The Naked Sun, The End Of Eternity na Nightfall.
Miaka 146 iliyopita katika siku kama ya leo mwaka 1292 Hijiria, alifariki dunia Ayatullah Mirza Abul Qasim Kalantari. Alikuwa miongoni mwa wasomi wakubwa wa Kiislamu wa Tehran. Ayatullah Kalantari alibobea sana katika elimu za hadithi, falsafa na mantiki. Msomi huyo alipata elimu kwa wasomi mashuhuri wa mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq akiwemo Shekh Murtadha Ansari na kufikia daraja ya Ijtihad. Ameandika vitabu vingi hasa katika uwanja wa fiqhi na sheria za Kiislamu.
Miaka 151 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Gilbert Murray, mshairi na malenga wa Australia. Akiwa na umri wa miaka 11 Murray alielekea nchini Uingereza na baada ya kumaliza masomo ya juu katika Vyuo Vikuu nchini humo, alifundisha taaluma ya utamaduni na fasihi ya Kigiriki katika Chuo Kikuu cha Oxford. Murray alifariki dunia mwaka 1957 na kuacha athari za vitabu kadhaa kama vile, 'Historia ya Fasihi ya Ugiriki ya Kale' na 'Imani, Vita na Siasa'.
Siku kama hii ya leo miaka 173 posta ya kwanza yenye muundo wa kisasa ilifunguliwa huko Vienna mji mkuu wa Austria. Kabla ya kuanzishwa chombo makhsusi kwa ajili ya kusafirisha barua na vifurushi vya posta, mizigo hiyo ilikuwa ikisafirishwa kwa kutumia farasi, ngamia au boti makhsusi. Hata hivyo miaka mingi baadaye kulibuniwa mbinu mpya na mfumo wa posta ukaboreshwa zaidi na kuwa na sura ya sasa.