Jumanne, tarehe 3 Januari, 2017
Leo ni Jumanne tarehe 4 Rabiuthani 1saw ana tarehe 3 Januari 2017.
Siku kama ya leo miaka 1265 iliyopita, alizaliwa Sayyid Abdul Adhim al Hassani aliyekuwa mmoja wa wajukuu wa Imam Hassan al Mujtaba (a.s) huko katika mji wa Madina. Sayyid Abdul Adhim alikuwa mmoja kati ya shakhsiya walioaminiwa na Imam al Hadi (as) na alinukuu hadithi moja kwa moja kutoka kwa maimamu watukufu kama vile Ridha, Jawad na al Hadi (as). Sayyid Abdul Adhim alihamia Iran kutokana na pendekezo la Imam al Hadi (as) kwa ajili ya kuwaongoza Waislamu na akaishi katika mji wa Rei karibu na Tehran ya sasa. Sayyid Abdul Adhim aliuawa shahidi mwezi Shawwal mwaka 250 Hijria. Kaburi la mtukufu huyo liko katika eneo la Rei na ni miongoni mwa maeneo yanayotembelewa na Waislamu kutoka maeneo mbalimbali duniani.
Tarehe 14 Dei miaka 38 iliyopita wakati wa kilele cha harakati za mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya utawala wa Kifalme wa Shah, Jenerali Robert E. Huyser aliyekuwa mshauri mkuu wa kijeshi na Naibu Kamanda wa Jeshi la Anga la Marekani aliwasili kwa siri mjini Tehran. Jenerali Huyser alikuwa na jukumu maalumu la kuisaidia serikali ya Marekani katika kuchukua maamuzi ya baadaye na kupata habari za ndani za Iran katika kipindi cha harakati za Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini. Katika kipindi chote cha zaidi ya siku 30 za kuwepo kwake mjini Tehran Jenerali Huyser alikutana mara moja tu na Shah na katika kikao hicho iliainishwa saa na siku ya kuondoka Shah nchini Iran.
Siku kama ya leo miaka 24 iliyopita Marais Boris Yeltsin wa Russia na George Bush baba wa Marekani walitia saini mkataba wa kupunguza silaha za nyuklia za nchi hizo mbili. Kwa mujibu wa mkataba huo, nchi hizo mbili ziliahidi kupunguza thuluthi mbili ya silaha zao za atomiki. Marekani ilikubali kutia saini mkataba huo baada ya Russia kukubali kushirikiana na Magharibi na kutotambuliwa tena kuwa ni tishio kubwa kwa Marekani baada ya kusambaratika Urusi ya zamani. Hata hivyo badala ya kuharibu silaha zake za nyuklia kwa mujibu wa mkataba huo, Marekani ilijilimbikizia zaidi silaha hizo na Russia ikaamua kusitisha kazi ya kuharibu silaha zake za nyuklia kwa ajili ya kulalamikia uamuzi huo wa Marekani.
Siku kama ya leo, miaka 925, alizaliwa mjini Baghdad Abubakr Muhammad Anbari, faqihi, mtaalamu wa hadithi na lugha. Anbari alipata kusoma elimu ya dini, nahwu na lugha akiwa kijana mdogo kutoka kwa baba yake. Baada ya kuhitimu masomo yake katika nyanja tofauti, alianza kufundisha na kulea wanafunzi wengi. Alitokea kuwa faqihi mkubwa na kutabahari katika elimu ya lugha ya Kiarabu. Msomi huyo ameandika vitabu vingi maarufu zaidi kikiwa ni kitabu cha ‘Manshurul-Fawaaid.’