Jan 05, 2017 01:06 UTC
  • Alkhamisi, 5 Januari, 2017

Leo ni Alkhamisi tarehe 6 Rabiuthani 1438 Hijria sawa na Januari 5, 2016.

Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita kulitokea hamasa ya mashahidi wa Huweize iliyoongozwa na Shahidi Alamul Huda katika miezi ya mwanzoni mwa uvamizi wa Iraq dhidi ya ardhi ya Iran. Mwezi Dei mwaka 1359 Hijria Shamsia na baada ya jeshi la Iran ya Kiislamu kuvishinda vikosi zaidi ya viwili vya jeshi la Iraq huko kusini mwa eneo la Susangerd, kundi moja la Jeshi al Sepah la Ahwaz huko kusini mwa Iran lilitumwa katika mji wa Huweize kwenda kuulinda mji huo mbele ya mashambulizi ya Iraq. Hata hivyo kutokana na kuchelewa kufika zana na hujuma kubwa ya Iraq, jeshi la Iran lililazimika kurudi nyuma. Wakati huo zaidi ya wapiganaji mia moja wa Jeshi la Sepah, wapiganaji wa kujitolea na wanafunzi wa vyuo vikuu wafuasi waaminifu wa Imam Khomeini wakiongozwa na Sayyid Muhammad Hussein Alamul Huda walibakia katika mji huo wa Huweize wakipambana na adui na wakauawa shahidi. Baadaye jeshi la Iraq liliuvunja kabisa mji wa Huweize na kuusawazisha na ardhi. Pamoja na hayo ushujaa wa vijana hao shupavu wa Iran waliosabilia roho zao kulinda ardhi ya Jamhuri ya Kiislamu umebakia hai katika historia ya Iran.

Siku kama ya leo miaka 57 iliyopita alifariki dunia Ali Isfandiyari mashuhuri kwa jina la Nima Yushij mwasisi wa mashairi ya kisasa nchini Iran. Isfandiyari alizaliwa katika mojawapo ya vijiji vya mkoa wa Mazandaran kwa jina la Yush huko kaskazini mwa Iran. Malenga huyo baadaye alielekea Tehran na kuanza kujifunza lugha ya Kifaransa. Nima Yushij alianza kutunga mashairi na kubuni mfumo mpya wa mashairi. Miongoni mwa sifa za mfumo huo wa mashairi mapya ni kueleza masuala ya jamii kwa lugha nyepesi na kutokuwa na wizani. Kazi muhimu zaidi ya malenga huyo mashuhuri wa Iran ni maarufu kwa jina la "Afsaneh".

Siku kama ya leo miaka 326 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 5 Januari 1691, ilichapishwa na kusambazwa noti ya kwanza huko Ulaya. Noti hiyo ilichapishwa na Benki ya Stockholm na kutumiwa kama fedha. Kabla ya kuchapishwa noti hiyo nchini Sweden, miamala ya kibiashara ilikuwa ikifanyika kwa kutumia sarafu za dhahabu zenye pembe nne. Moja kati ya noti za awali kabisa kuchapishwa nchini Sweden, inahifadhiwa kwenye makumbusho ya Benki ya Stockholm.

Siku kama ya leo miaka 585 iliyopita, sawa na tarehe sita Rabiuth-Thani mwaka 852 Hijiria, alizaliwa Ebn-e Eyas, mwanahistoria mashuhuri wa nchini Misri. Ebn e-Eyas alinakili habari mbalimbali za kihistoria kwa mfumo wa nathari nyepesi, mfumo ambao ulikuwa hautumiwi na wanahistoria wengine. Mfumo huo ulikuwa na umuhimu mkubwa kwenye fani ya lugha ya Kiarabu. Miongoni mwa athari muhimu ya kihistoria za Ebn-e Eyas ni pamoja na kitabu cha "Badaaiuz-Zuhuur fii Waqaaiud-Duhuur" ambacho kinaelezea historia ya Misri tangu karne za nyuma hadi kipindi chake. Aidha alifafanua maisha ya watawala wa Misri, ujenzi na uimarishwaji wake na mambo mbalimbali yaliyowahi kuikumba nchi hiyo katika karne za nyuma.

Siku kama ya leo miaka 622 iliyopita alifariki dunia Mir Sayyid Sharif Gorgani, mtaalamu wa fasihi wa Iran huko Shiraz. Gorgani alizaliwa mwaka 740 Hijiria karibu na mji wa Gorgani ya leo, kaskazini mwa nchi hii. Mir Sayyid Sharif Gorgani alihesabika kuwa msomi mkubwa katika zama hizo hususan katika uga wa elimu ya fasihi. Ameacha athari mbalimbali mojawapo ikiwa ni kitabu kiitwacho "Risaalatul-Kubra fil-Mantwiq" na "Sharhu Mawaaqif Qadhi Adhdud-Diin Iji."

Siku kama ya leo miaka 1313 iliyopita, alifariki dunia Hisham Bin Abdul-Malik, kiongozi wa 10 katika silsila ya watawala wa Bani Umayyah baada ya kuwa madarakani kwa karibu kipindi cha miaka 20. Hisham aliyekuwa dikteta alizaliwa mwaka 72 Hijiria na kushika uongozi wa Waislamu mwaka 105 Hijiria. Aidha Hisham anafahamika kwa kuwa bahili, katili na dhalimu, ambaye aliwakandamiza Waislamu wa zama zake hususan wafuasi wa Ahlul Bayt wa Mtume (saw) yaani Mashia. Mtawala huyo wa Bani Umayyah aliishi katika kipindi cha Imam Muhammad Baqir (as) mmoja wa wajukuu watukufu wa Nabii wa Uislamu ambapo alimfanyia maudhi mengi mtukufu huyo na baadaye kutoa amri ya kuuawa kwake. Mbali na hapo Hisham alifanya ukandamizaji mkubwa dhidi ya harakati za Zaid bin Ali, mjukuu wa Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as). Baada ya kuuliwa Zaid, mtawala huyo dhalimu alitoa amri ya kuchomwa moto mwili wa mtukufu huyo. Licha kwamba katika kipindi cha utawala wa Bani Umayyah, Uislamu ulienea maeneo ya mashariki na magharibi mwa dunia, lakini kulishuhudiwa harakati kadhaa za Kiislamu za kupinga dhulma, kutokana na kushadidi dhulma na ukandamizaji wa Hisham bin Abdul-malik, harakati ambazo zilipelekea kudhoofika kwa dola hilo la Bani Umayyah.

هشام بن عبدالملک

Miaka 1414 iliyopita katika siku kama ya leo vita vya miaka 24 kati ya tawala za Roma na Iran vilianza. Chanzo cha kuzuka vita hivyo ni kuuawa Morris  mtawala wa wakati huo wa Roma aliyekuwa mtetezi na rafiki wa karibu wa Khosro Parviz Mfalme wa wakati huo wa Iran.