Jan 06, 2017 04:20 UTC
  • Ijumaa, 6 Januari, 2017

Leo ni Ijumaa tarehe 7 Rabiuthani 1438 Hijria sawa 6 Januari 2017.

Tarehe 17 Dei miaka 39 iliyopita wananchi Waislamu wa Iran walifanya maandamano makubwa kote nchini wakilalamikia kuchapishwa makala iliyomvunjia heshima mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu. Maandamano hayo yalizidisha vuguvugu na kasi za Mapinduzi ya Kiislamu kuelekea katika ushindi. Utawala wa Shah ambao ulikuwa ukifahamu vyema ushawishi na uungaji mkono mkubwa wa Imam Khomeini miongoni mwa wananchi, ulikuwa ukidhani kwamba kumvunjia heshima Imam Khomeini kungeweza kupunguza kiwango cha mapenzi na uungaji mkono mkubwa wa wananchi kwa shakhsia huyo. Katika kufanikisha lengo hilo, gazeti la Ittilaat lililokuwa likitolewa mjini Tehran liliandika makala ya kumvunjia heshima Imam Khomeini katika toleo lake la mwezi Dei mwaka 1356 Hijria Shamsiya. Hata hivyo makala hiyo ilikuwa kama cheche ya moto iliyochochea zaidi harakati za mapinduzi na hatimaye tarehe 22 mwezi Bahman mwaka 1357, utawala kibaraka wa Shah ukang'olewa madarakani kwa mapambano ya wananchi wa Iran.

Siku kama ya leo miaka 81 iliyopita, Reza Khani Pahlavi mfalme wa wakati huo wa Iran, alitoa amri ya kuwazuia wanawake kuvaa aina yoyote ya vazi la Kiislamu yaani hijabu hapa nchini. Amri hiyo ilitolewa baada ya utekelezwaji wa mpango wa kubadili mavazi ya kiume kwa lengo la kufuta kabisa athari za Kiislamu na kufuata kibubusa siasa za madola ya Magharibi. Kabla ya hapo mfalme huyo alikuwa amefanya safari nchini Uturuki na kukutana na Rais wa nchi hiyo Mustafa Kemal Atatürk, ambaye naye alikuwa amepiga marufuku vazi la Kiislamu la mwanamke wa Kiislamu hijabu nchini humo kwa kufuata siasa za Magharibi. Kufuatia hatua hiyo vibaraka wa mfalme huyo walianza kuwafanyia dhihaka na kuwadunisha wanawake wa Kiislamu waliokuwa wakivaa vazi hilo la heshima.

Reza Khani Pahlavi

Siku kama ya leo miaka 156 iliyopita, yaani sawa na tarehe 6 Januari mwaka 1861 kuliasisiwa nchi ya Romania. Mpango wa kupatikana nchi hii msingi wake ulikuwa kutiwa saini kwa muungano wa miji miwili midogo iliyojulikana kwa jina la Moldavia na Wallachia, makubaliano yaliyofikiwa tarehe 13 Disemba mwaka 1859. Baada ya miaka miwili majimbo na miji mingine ya jirani vikajiunga na muungano huo. Kwa utaratibu huu ikapatikana nchi iliyokuja kutambulika kwa jina la Romania.

Bendera ya Romania