Jan 06, 2017 23:48 UTC
  • Jumamosi, 7 Januari, 2017

Leo ni Jumamosi tarehe 8 Mfunguo Saba Rabiu Thani 1438 Hijria mwafaka na tarehe 7 Januari mwaka 2017 Miladia.

Siku kama ya leo 1206 yaani mwaka 232 Hijria, Mtukufu Imam Hassan Askary (AS) mjukuu wa Mtume na mmoja wa Maimamu na watu watoharifu wa Nyumba Tukufu ya Bwana Mtume (SAW) alizaliwa katika mji mtakatifu wa Madina. Alilazimika kuhajiri akiwa mdogo pamoja na baba yake kutokana na mashinikizo ya viongozi wa utawala wa Bani Abbas na kuelekea katika ardhi ya Samarra nchini Iraq. Imam Askary alibaki mjini humo kwa muda wa miaka 13 na kustafidi na bahari ya elimu ya baba yake yaani Imam Hadi AS. Baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Hassan Askary alichukua jukumu zito la kuwaongoza Waislamu sambamba na kueneza mafunzo sahihi ya dini tukufu ya Kiislamu. Kama walivyokuwa Maimamu wengine watukufu, Imam Hassan Askary naye aliitumia karibu sehemu yote ya umri wake kulinda na kueneza mafunzo sahihi na a'ali ya dini tukufu ya Kiislamu. ***

Haram ya Imam Hassan Askary (as)

Katika siku kama ya leo miaka 1081 iliyopita, Abu Feras Hamdani mshairi na mwandishi wa Kiarabu alifariki dunia. Sambamba na kuwa mshairi, Abu Feras alikuwa mpiganaji vita na alikuwa mmoja wa watu wa karibu wa Seif al-Daulah mtawala wa Halab na alikuwa mmoja wa makamanda wa jeshi.  ***

Abu Feras Hamdani

Miaka 170 iliyopita yaani mwaka 1268 Hijria, alizaliwa Sayyid Murtadha Kashmiri, mmoja wa maulama na maurafaa mahiri. Alimu huyo alizaliwa katika familia iliyokuwa ikiheshimika. Akiwa kijana mdogo alianza kusoma elimu za Kiislamu kwa baba yake na kwa maulama wengine wa eneo hilo. Akiwa na umri wa miaka 16 Murtadha Kashmiri alifunga safari na kuelekea Iraq kwa ajili ya kujiendeleza zaidi kielimu. Msomi huyo wa Kiislamu ameandika vitabu pia katika maudhui mbalimbali. ***

Ayatullah Sayyid Murtadha Kashmiri

Siku kama ya leo miaka 165 iliyopita, Mirza Taqi Khan Amir Kabir mwanasiasa na Kansela wa kipindi cha utawala wa Qajar nchini Iran aliuawa kwa amri ya Nassir Deen Shah. Kutokana na Mirza Taqi Khan Amir Kabir kuwa na kipaji na ustahiki mwingi alichaguliwa kuwa Kansela katika kipindi cha utawala wa Qajar. Amir Kabir alikuwa mtu huru, mwenye imani, mwenye uzalendo na kupenda nchi na mwenye mapenzi na utamaduni na anahesabiwa kuwa mmoja wa waasisi wa misingi ya marekebisho na fikra za juu katika uwanja wa utoaji elimu, malezi na utamaduni nchini Iran. ***

Mirza Taqi Khan Amir Kabir

Miaka 99 iliyopita katika siku kama ya leo kulingana na kalenda ya Hijria aliaga dunia Sheikh al-Shari'a Isfahani mwalimu mkubwa wa Chuo Kikuu cha Kidini cha mjini Najaf Iraq. Alizaliwa mwaka 1266 Hijria katika mji wa Isfahan nchini Iran. Mwaka 1295 Hijria alielekea Najaf Iraq kwa lengo la kujiendeleza zaidi kimasomo na kufanikiwa kuhudhuria masomo na darsa za wanazuoni mahiri wa zama hizo kama Mullah Ahmad Sabzawar, Muhammad Hussein Kadhmeini, na Mirza Habibullah Rashti. Miongoni mwa wanafunzi wake ni Muhammad Taqi Khonsari, Abdul Karim Hairi na Muhammad Hussein Borujerdi. Sheil al-Shar'ia aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 73 na amezikwa katika haram ya Imam Ali bin Abi Talib mjini Najaf Iraq. ***

Sheikh al-Shari'a Isfahani

Miaka 74 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Nikola Tesla mwanafizikia wa Yoslavia. Nikola alizaliwa mwaka 1856 na katika kipindi cha masomo yake alikuwa na mapenzi makubwa na elimu ya fizikia. Msomi huyo wa Kiyugoslavia alifanya tafiti na uvumbuzi wake mwingi katika uwanja wa nishati ya umeme na kupata mafanikio makubwa. Umeme mbadala au Altenative electricity unahesabiwa kuwa miongoni mwa uvumbuzi wa Nikola Tesla. Mwanafikizia huyo alikipa jina lake la Tesla, kifaa kinachotumika kupimia kiwango na mtiririko wa sumaku yaani (magnetic flux).

Nikola Tesla

Katika siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, dikteta wa Cambodia Pol Pot alikimbia nchi kufuatia mashambulizi ya jeshi la Vietnam dhidi ya nchi hiyo na ikaingia madarakani serikali iliyokuwa ikiongozwa na Heng Samrin. Kiongozi huyo wa kundi la Khmer Rouge alikuwa muungaji mkono mkubwa wa fikra za kimao na serikali ya China. Sifa kuu ya serikali ya Pol Pot ilikuwa kutumia mabavu dhidi ya raia, kuwahamishia kwa nguvu vijijini na kufuta kabisa athari zote za utamaduni na ustaarabu asilia. Pol Pot na kundi lake na Khmer Rouge waliua watu wanaokadiriwa kuwa milioni moja na nusu hususan raia wenye asili ya Vietnam katika kipindi cha chini ya miaka mitatu ya utawala wake huko Cambodia. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana jeshi la Vietnam likachukua hatua za kuiondoa madarakani serikali ya Pol Pot. ***

Pol Pot

Katika siku kama ya leo  miaka 31 iliyopita, Suleiman Khater aliyekuwa miongoni mwa polisi wa mpakani wa Misri katika jangwa la Sinai alikufa shahidi akiwa jela. Suleiman Khatwar mwezi Oktoba mwaka 1985 aliwaangamiza Wazayuni wengi katika kulalamikia hatua ya serikali ya Misri ya kusaini hati ya mapatano ya Camp David kati yake na utawala wa Kizayuni. Serikali ya Misri ilimtia mbaroni polisi huyo na kumhukumu kifungo cha maisha jela katika mahakama ya kimaonyesho. Hata hivyo maiti yake ilipatikana baadaye katika kituo cha afya cha magereza ikiwa imeing'inia na serikali ya Misri ikadaiwa kwamba, polisi huyo alijiua.  ***

Suleiman Khater

Na miaka 24 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia mtaalamu wa masuala ya Kiislamu na mtarjumi wa Qur'ani Tukufu kwa lugha ya Kijapani Toshihiko Izutsu. Alizaliwa tarehe 4 Mei 1914 katika mji wa Tokyo na mwaka 1960 alipata shahada ya uzamivu katika taaluma ya lugha na kuanza kufunza lugha na falsafa yake. Toshihiko Izutsu alitunukiwa nishani ya juu kabisa ya elimu kutoka kwa mfalme wa Japan na ameandika vitabu vingi. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni "Historia ya Fikra za Kiislamu", tarjumu ya kitabu cha "al Mashair" cha Mulla Sadra na vilevile tarjumu ya kitabu cha "Fihi Maa Fiih" cha Maulawi kwa lugha ya Kijapan.

Toshihiko Izutsu