Jumapili, Januari 8, 2017
Leo ni Jumapili tarehe 9 Rabiuth-Thani mwaka 1438 Hijria, sawa na tarehe 8 Januari 2017 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 375 iliyopita, alifariki dunia msomi mashuhuri, mnajimu na mtaalamu wa fizikia wa Italia Galileo Galilei akiwa na umri wa miaka 78. Alizaliwa katika mji wa Pisa na alisoma fasihi hadi alipofikisha umri wa miaka 19 na baadaye akajishughulisha na fizikia na hisabati. Galileo alitumia lenzi iliyovumbuliwa na msomi na mnajimu mashuhuri wa Kiislamu, Ibn Haitham kutengeneza darubini ya elimu ya nujumu kwa ajili ya kutazamia nyota na sayari. Galileo alitumia chombo hicho kuthibitisha kwamba sayari ikiwemo ya ardhi, zinazunguka jua. Utafiti huo wa Galileo Galilei ulithibitisha nadharia ya Abu Raihan Biruni msomi mashuhuri wa Iran ambaye karne kadhaa kabla yake alithibitisha kwamba ardhi inazunguka jua. Baada ya kusambaa nadharia hiyo ya Galileo kuhusu mzunguko wa ardhi na sayari nyingine kando ya jua, Kanisa la Roma lilimtuhumu kuwa ni kafiri na akahukumiwa. Baadaye msomi huyo alilazimika kukanusha nadharia hiyo kwa ajili ya kuokoa maisha yake.
Siku kama ya leo miaka 134 iliyopita alifariki dunia Ayatullah Haj Mirza Abdul Rahim Nahavandi, alimu na msomi mkubwa wa sheria za Kiislamu. Ayatullah Nahavandi alibobea katika elimu ya fiqhi na usulu fiqhi, na kutokana na hali hiyo wasomi wengi wa Iraq na Iran waliweza kustafidi na elimu yake. Inafaa kufahamisha kwamba, Ayatullah Haj Mirza Abdul Rahim Nahavandi, alizaliwa katika mji wa Nahavand, ulio magharibi mwa Iran na akiwa kijana alielekea mjini Najaf, Iraq na kusoma kwa walimu wakubwa wa zama hizo hususan Sheikh Murtadha Answari, ambapo kwa kipindi cha miaka 30 alijikita katika shughuli ya ufundishaji wa sheria za Kiislamu.
Siku kama ya leo miaka 134 iliyopita, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 58, Ayatullah Sayyid Haidar Hilli. Abul-Hassan Sayyid Haidar Bin Sulaiman Bin Daud Hilli Husseini, ni miongoni mwa malenga na viongozi mashuhuri wa fani hiyo katika zama hizo. Ufasaha na uwezo mkubwa wa kiimani aliokuwa nao, vilimsukuma katika kuwasifu Ahlu Baiti wa Mtume (saw) kupitia mashairi yake. Miongoni mwa athari zake ni pamoja na kitabu cha 'ad-Duraru-Yatim' na 'al-Aqdul-Mufaswal.'
Siku kama ya leo miaka 84 iliyopita, yaani tarehe 8 Januari mwaka 1932 Miladia, ulianza utawala wa kifalme wa Abdul-Aziz Ibn Saud katika eneo la Bara Arabu kupitia msaada wa Uingereza. Abdul-Aziz Ibn Saud, aliyekuwa mmoja wa viongozi wa makabila ya Hijaz, alianzisha mapambano makali dhidi ya utawala wa Othmania uliokuwa umebeba bendera ya Usuni, mwishoni mwa karne ya 19 na mwanzoni mwa karne ya 20 Miladia, ambapo pia alipata ushindi mkubwa. Mwaka 1903 Miladia Waturuki wa Othmania walitimuliwa kutoka maeneo ya al-Ahsa yaliyokuwa ndani ya Hijazi, ambapo kuliambatana na kuasisiwa utawala wa Aal-Saud katika maeneo hayo. Katika kipindi cha kujiri Vita vya Kwanza vya Dunia, Aal-Saud waliingia ubia wa urafiki na Uingereza. Hatimaye mwishoni mwa vita hivyo, vilivyomalizika kwa kushindwa vibaya utawala wa Othomania, utawala huo ulifikia tamati kikamilifu katika eneo hilo la Bara Arabu. Aidha katika vita vilivyopiganwa baina ya Abdul-Aziz Ibn Saud na mtawala wa Kisuni Hussein Bin Ali Shrif na aliyekuwa mtawala wa mji wa Makkah, Ibn Saud aliibuka mshindi na hivyo kuitwaa kwa nguvu Hijaz. Hatimaye mwaka 1926 na kwa mujibu wa makubaliano yaliyokuwepo kati ya Uingereza na mfalme huyo wa Kiwahabi, mji wa Hijaz ukatangazwa kuwa mji ulio huru huku Abdul-Aziz Ibn Saud akijitangaza kuwa kiongozi wake. Aidha mwaka 1927 Ibn Saud alijitangaza rasmi kuwa mfalme, huku akikalia kiti hicho cha ufalme tarehe 8 Januari mwaka 1932 Miladia, jambo ambalo lilienda sambamba na kutangazwa eneo hilo kwa jina la mfalme huyo yaani Saudia.
Na siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, alifariki dunia, Zhou Enlai, mwanasiasa na waziri mkuu wa kwanza wa serikali ya Ukomonisti nchini China. Enlai alizaliwa mnamo mwaka 1898 Miladia ambapo akiwa kijana mdogo alielekea nchini Ufaransa kwa ajili ya masomo. Baada ya kurejea nchini kwake alianza kujishughulisha na masuala ya kisiasa ambapo mwaka 1936 alionekana kuwa shakhsia mwenye nafasi kubwa katika chama hicho cha Ukomonisti. Hatimaye mwezi Oktoba mwaka 1949 Miladia Zhou Enlai akateuliwa kuwa kiongozi wa baraza la urais na waziri mkuu wa nchi hiyo.