Alkhamisi, 12 Januari, 2017
Leo ni Alkhamisi tarehe 13 Rabithani 1438 Hijria sawa na 12 Januari 2017
Siku kama ya leo miaka 7 iliyopita, mtetemeko mkubwa wa ardhi wenye ukubwa wa 7 kwa kipimo cha Rishta ilitokea huko Haiti katika bahari ya Caribbean. Zilzala hiyo ilikuwa kubwa zaidi kuwahi kutokea duniani katika miongo kadhaa iliyopita na iliua watu karibu laki tatu na kujeruhi wengine wengi. Mtetemeko huo wa ardhi ulioikumba Haiti uliharibu kabisa miundo mbinu na nyumba nyingi za nchi hiyo. Aidha ulipelekea mamia ya maelfu ya raia kuwa wakimbizi.
Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita mapigano makali kati ya polisi wa utawala wa Shah na wananchi wa Iran yalitokea wakati yalipofanyika maandamano makubwa ya wananchi katika miji kadhaa ya Iran. Wananchi wengi wanamapambano waliuawa shahidi na wengine kujeruhiwa katika maandamano hayo. Katika siku hiyo pia wanachuo na wakazi wa mji wa Tehran ambao walikuwa wamekusanyika kwa wingi mbele ya Chuo Kikuu cha Tehran walitangaza upinzani wao dhidi ya utawala wa Shah na wakitaka kurejea Tehran Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu, kutoka uhamishoni huko Paris nchini Ufaransa.

Miaka 352 iliyopita katika siku inayosadifiana na leo, aliaga dunia Pierre de Fermat mwanahisabati wa Kifaransa na muasisi wa nadharia ya leo ya namba yaani Modern Theory of Numbers na ile ya uwelekeo inayojulikana kama Theory of Probability. Pierre de Fermat alizaliwa mwaka 1601 Miladia na alianza kujifunza hesabu tangu akiwa mtoto. Mwanahisabati huyo wa Kifaransa aligundua pia kanuni msingi ya jiometri changanuzi, yaani Analytic Geometry.
Siku kama ya leo miaka 1219 iliyopita yaani tarehe 13 Rabiuthani mwaka 218 Hijria aliaga dunia Ibn Hisham msomi na mwanazuoni mkubwa wa Kiarabu. Ibn Hisham alizaliwa Basra nchini Iraq na alibobea katika elimu na fasihi na utungaji mashairi. Alitumia sehemu kubwa ya umri wake kufanya uchunguzi kuhusu maisha ya Nabii Muhammad (saw). Umashuhuri mkubwa wa Ibn Hisham unatokana na kitabu chake cha al Sira al Nabawiyya ambacho ni miongoni mwa marejeo muhimu kuhusu maisha ya Mtume Muhammad (saw).