Ijumaa, 13 Januari, 2017
Leo ni Ijumaa tarehe 14 Rabiuthani 1438 Hijria sawa na Januari 13, 2017.
Siku kama ya leo miaka 1372 iliyopita Mukhtar bin Abi Ubaida al Thaqafi alianza mapambano ya kulipiza kisasi cha damu ya Imam Hussein bin Ali AS, mjukuu wa Mtume Muhammad SAW. Mwaka 61 Hijria Imam Hussein AS akiwa pamoja na wafuasi na watu wa familia yake, aliuawa shahidi na jeshi la Yazid akiwa katika harakati za kuilinda dini tukufu ya Uislamu. Mukhtar alianzisha harakati zake za mapambano katika mji wa Kufa. Kabla yake, kulijitokeza kundi la 'Tawwabiin' ambalo lilipigana na utawala wa Bani Umayyah, kwa lengo la kulipiza kisasi cha damu ya Imam Hussein AS. Mukhtar Thaqafi alitawala Kufa kwa kipindi cha karibu mwaka mmoja na mwishowe alishindwa na jeshi la Mus'ab bin Zubair na kuuawa shahidi.

Miaka 76 iliyopita katika siku kama hii ya leo mkutano wa kihistoria wa nchi waitifaki za Ulaya katika Vita vya Pili vya Dunia ulifanyika mjini London, Uingereza. Mkutano huo ulifanyika kufuatia pendekezo la waziri mkuu wa wakati huo wa Uingereza Winston Churchill, lengo kuu lilikuwa kuratibu siasa za wakuu wa nchi za Ulaya katika medani za vita dhidi ya nchi mbili za Ujerumani na Italia. Vilevile nchi za Uingereza, Uholanzi, Ubelgiji, Ufaransa, Ugiriki, Norway, Luxembourg na Denmark zilishiriki katika mkutano huo.
Tarehe 13 Januari miaka 567 iliyopita alizaliwa baharia na mvumbuzi wa Kireno kwa jina la Bartholomew Diaz. Baada ya kusafiri katika Bahari ya Atlantic kuelekea kusini mwaka 1488, Diaz aligundua Rasi ya Tumaini Jema au (Cape of Good Hope) katika sehemu ya kusini zaidi ya bara la Afrika. Miaka kumi baadaye baharia mwenzake kwa jina la Vasco Da Gama naye pia alifanikiwa kugundua njia ya baharini kuelekea India kupitia eneo hilo.