Jan 15, 2017 02:30 UTC
  • Jumapili, Januari 15, 2017

Leo ni Jumapili tarehe 16 Rabiul th-Thani mwaka 1438 Hijria, sawa na tarehe 15 Januari 2017 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita Muhammad Reza Pahlavi mfalme wa mwisho wa Iran alikimbia nchi kwa kisingizio cha matibabu baada ya kupamba moto mapambano ya wananchi Waislamu wa Iran. Mwaka 1320 Hijria Shamsiya Muhammad Ridha Pahlavi alikalia kiti cha ufalme baada ya serikali ya Uingereza kumbaidisha baba yake Ridha Shah kutokana na hatua yake ya kuiunga mkono Ujerumani wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Mwaka 1332 Hijria Shamsiya Shah kwa mara nyingine tena aliikimbia Iran kufuatia mapambano ya wananchi, hata hivyo siku tatu baadaye yaani, Shah alirejea nchini baada ya mapinduzi yaliyoendeshwa na Marekani na Uingereza dhidi ya wananchi wa Iran.

Siku kama ya leo miaka 973 iliyopita alifariki dunia Abdul-Karim Bin Huzan al-Qushayri, maarufu kwa jina la Zainul-Islam, faqihi na mmoja wa maulama wakubwa wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 376 Hijiria mjini Quchan, kaskazini mashariki mwa Iran ambapo alielekea mjini Nishapur kwa ajili ya kutafuta elimu. Mbali na mjini Makkah alienda pia mara mbili mjini Baghdad, Iraq kwa ajili ya kujiendeleza kielimu. Huzan al-Qushayri alikuwa hodari katika elimu ya sharia za Kiislamu (fiqhi), theolojia, tafsiri na hadithi, huku akiwa mfuasi wa Usufi. Ameacha vitabu kadhaa maarufu zaidi kikiwa ni kitabu cha 'Risaalatul-Qushayriyyah', 'at-Tayassur fi t-Tafsir' na 'Latwaaiful-Ishaaraat.'

Siku kama ya leo miaka 222 iliyopita alizaliwa Aleksandr Griboyedov, mwandishi na mwanasiasa wa Urusi. Alikuwa na uzoefu mkubwa katika fani ya uandishi kiasi cha kuweza kukosoa filamu za kuchekesha. Hata hivyo Griboyedov hakuweza kufanikiwa katika ulingo wa siasa. Katika vita vya pili baina ya Russia na Iran ya wakati huo, alikuwa askari wa kawaida. Baada ya Iran kushindwa katika vita hivyo na kwa amri ya serikali ya Urusi, alielekea mjini Tehran mwaka 1828 kwa ajili ya kuwachukua mateka wa nchi yake waliokuwa wanashikiliwa mjini hapa. Hata hivyo jeuri na kutokuwa na uzoefu Aleksandr Griboyedov katika kutekeleza jukumu hilo kuliibua hasira ya raia wa Iran na hivyo kumvamia na kumuua mwaka 1829.

Siku kama ya leo miaka 178 iliyopita, nchi ya El Salvador ilijitangazia rasmi uhuru wake baada ya kusambaratika Muungano wa Amerika ya Kati. Hata hivyo nchi hiyo haikupata amani na utulivu hata baada ya kupita karne moja. El Salvador ambayo ilikuwa ikikoloniwa na Uhispania kwa miaka kadhaa, ilijipatia uhuru mwaka 1821, na ulipofika mwaka 1824 ilijiunga na Muungano wa Amerika ya Kati, na hatimaye uliposambaratika muungano huo, nchi hiyo ilijitegemea kikamilifu.

Na siku kama ya leo miaka 16 iliyopita ensaiklopidia ya Wikipedia ilianza kazi katika mtandao wa intaneti. Lengo la kuanzishwa ensaiklopidia hiyo limetajwa kuwa ni kupanua maarifa na uelewa wa watu kupitia njia ya kushirikishwa watu wote katika mradi huo. Ensaiklopidia hiyo kubwa ya intaneti ina taarifa na makala kuhusu mamilioni ya vitu kwa lugha mbalimbali na ndiyo inayotembelewa zaidi na watu katika mtandao huo. Hata hivyo uwezekano wa kila mtu kuingia na kuandika anayotaka katika ensaiklopidia hiyo umeshusha chini hadhi na nafasi yake ya kielimu. Zaidi ni kwamba licha ya kuwa wasimamizi wa Wikipedia wanadai hawapendelei upande wowote lakini kwa kawaida makala zinazohusiana kwa njia moja au nyingine na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel huwa za upendeleo. Kituo kikuu cha Wikipedia kiko katika jimbo la Florida nchini Marekani na ensaiklopidia hiyo inafanya kazi kwa mujibu wa sheria za Marekani.