Jumatatu, 16 Januari, 2017
Leo ni Jumatatu tarehe 17 Rabiuthani 1438 Hijria sawa na Januari 16, 2017.
Siku kama ya leo miaka 16 iliyopita Rais Laurent Desire Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo alipigwa risasi na mmoja wa walinzi wake katika ikulu ya Rais na kujeruhiwa vibaya. Baada ya tukio hilo kulienea habari za kutatanisha juu ya hatima ya Rais huyo. Tarehe 18 Januari yaani siku mbili baadaye, serikali ya Kinshasa ilithibitisha kufariki dunia Rais huyo. Kabila alizaliwa mwaka 1939 huko Katanga alihudhuria masomo ya Chuo Kikuu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Tanzania. Aliingia madarakani mwaka 1997 baada ya vikosi alivyokuwa akiviongoza kuuteka mji wa Kinshasa, na kupelekea Rais Mobutu Sese Seko kukimbilia nje ya nchi. Tarehe 26 Januari Joseph Kabila mwana wa Rais Kabila alishika hatamu za uongozi nchini Congo.
Katika siku kama ya leo miaka 29 iliyopita, Sayyid Mahdi Hakim aliyekuwa mjumbe muhimu wa Baraza Kuu la Kiislamu la Iraq na mwana wa Ayatullah Sayyid Muhsin Hakim mmoja wa marajii wakubwa wa Kiislamu aliuawa shahidi na makachero wa utawala wa Saddam Hussein dikteta wa zamani wa Iraq, huko Khartoum mji mkuu wa Sudan. Sayyid Mahdi Hakim alikuwa mmoja wa wanafunzi wa shahidi Ayatullah Sadr na miongoni mwa wapinzani wakuu wa utawala wa Saddam Hussein. Miongoni mwa harakati za kijamii na kiutamaduni za msomi huyu wa Kiislamu ni kuanzisha Jumuiya ya Maulamaa wa Baghdad na Kadhimain na kuanzisha vituo vya elimu na malezi vya wanafunzi wa elimu ya dini.
Katika siku kama ya leo miaka 61 iliyopita yaani tarehe 27 Dey 1334 Hijria Shamsia, Sayyid Mujtaba Navvab Safavi, mwanachuoni na mwanaharakati wa Iran aliuawa shahidi pamoja na wenzake watatu, baada ya kuhukumiwa adhabu ya kifo kwenye mahakama ya kimaonyesho tu ya kijeshi katika utawala wa Shah hapa nchini. Akiwa kijana, Navvab Safavi alipata taaluma ya masomo ya kidini nchini Iran na kisha akaelekea Najaf nchini Iraq kwa shabaha ya kujipatia elimu zaidi. Alirejea nchini baada ya miaka kadhaa na kuanzisha mapambano dhidi ya utawala tegemezi na kibaraka wa Shah. Hatimaye katika siku kama hii ya leo Safavi alikamatwa na utawala wa Shah na kuuawa shahidi akiwa na wenzake watatu.
Siku kama ya leo miaka 171 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 16 Januari 1846, vilianza vita baina ya Marekani na Mexico baada ya Washington kuishambulia nchi hiyo. Vita hivyo vilivyochukua muda wa miaka miwili, vilitokea baada ya Marekani kudai kwamba wahajiri wa nchi hiyo wanateswa nchini Mexico. Hata hivyo ukweli ni kuwa, Marekani ilianzisha mashambulizi hayo kwa lengo la kuyatwaa baadhi ya maeneo ya Mexico hususan eneo la Texas. Katika vita hivyo, Marekani iliyakalia kwa mabavu majimbo ya Texas, California, Nevada, Utah, Arizona na New Mexico.
Miaka miaka 60 iliyopita katika siku sawa na ya leo alifariki dunia mtunzi wa nyimbo mwenye asili ya Italia kwa jina la Arturo Toscanini. Toscanini alizaliwa mwaka 1867 na alianza kupenda muziki akiwa kijana. Arturo Toscanini alikuwa kiongozi wa bendi baada ya kufanya mazoezi mengi na kusafiri katika nchi mbalimbali duniani. Aidha alipata umashuhuri kutokana uwezo wake mkubwa wa kuhifadhi na kuwa makini katika utunzi wa nyimbo. Toscanini aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 90 yaani miaka mitatu baada ya kustaafu kazi ya muziki.