Ijumaa, Januari 20, 2017
Leo ni Ijumaa tarehe 21 Mfunguo Saba Rabiuthani 1438 Hijria sawa na Januari 20, 2017 Milaadia
Siku kama ya leo miaka 38 liyopita sambamba na kuanza kutetereka nguzo za utawala wa Shah nchini Iran mkabala wa wimbi kubwa la mashinikizo ya wananchi na harakati za Mapinduzi ya Kiislamu, serikali ililazimika kuwaachia huru wafungwa waliokuwa katika jela za Shah na wananchi Waislamu wa Iran wakawapokea watoto wao waliokuwa wakiteseka kwa miaka mingi katika jela hizo. Alasiri ya siku hiyo maafisa wa jeshi la anga la Iran walifanya maandamano na kutangaza uungaji mkono wao kwa harakati ya taifa la Kiislamu la Iran. Siku hiyo hiyo pia magazeti ya Iran yaliandika habari iliyokuwa na kichwa kilochokolezwa wino kwamba: "Imam Khomeini Kurejea Iran Siku Kadhaa Sijazo". Habari hiyo ilizusha wimbi la hamasa na furaha kubwa kati ya wananchi wanamapinduzi wa Iran na kila mtu alianza kujitayarisha kwa ajili ya kwenda kumpokea kiongozi wa kihistoria wa Mapinduzi ya Kiislamu Imam Ruhullah Khomeini.
Tarehe 20 Januari miaka 96 iliyopita alizaliwa mtengeneza filamu mashuhuri wa Italia, Federico Fellini. Alikuwa mtayarishaji filamu mwenye mbinu makhsusi. Fellini alianza kuandika rasimu ya filamu (scenario) mwaka 1938 na baadaye akaingia katika uwanja wa kutayarisha filamu. Baada ya kumalizika Vita vya Kwanza vya Dunia Fellini alishirikiana na mtengenezaji filamu mwingine wa Italia, Roberto Rossellini, katika utengenezaji wa filamu ya "Rome, Open City" (Roma, Mji Usiokuwa na Ulinzi). Miezi sita kabla ya kufariki dunia, Federico Fellini alitunukiwa tuzo ya fahari ya Oscar kutokana na kazi zake kubwa katika medani ya filamu. Filamu mashuhuri zaidi za Fellini ni "Saa Mbili Unusu", "Juliet of the Spirits" na "The Sweet Life".
Siku kama hii ya leo miaka 117 iliyopita aliaga dunia John Ruksin mwandishi na malenga wa Kiingereza. Ruksin alizaliwa mwaka 1819 Miladia katika familia tajiri na ya kicha-Mungu, chini ya ulezi wa baba na mama yake. Ruksin awali alifunzwa na wazazi wake akiwa nyumbani kabla ya kujiunga na chuo cha mjini London na akiwa huko akaanza kutunga mashairi. Malenga huyo wa Kiingereza alikuwa mkosoaji wa sekta ya sanaa na alibainisha juu ya mitazamo yake kuhusu sanaa katika kitabu chake alichokipa jina la "modern painters".