Jumatatu, 30 Januari, 2017
Leo ni Jumatatu tarehe Mosi Jamadil Awwal 1438 Hijria sawa na tarehe 30 Januari 2017.
Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita gwaride la mwisho na kimaonyesho la vikosi vya majeshi ya utawala wa Shah lililokuwa na lengo la kuwatia hofu na woga wananchi Waislamu wa Iran, lilifanyika katika mitaa mbalimbali ya Tehran. Katika gwaride hilo, wanajeshi wengi walionesha mshikamano wao na kuungana na wananchi Waislamu wa Iran na kuamua kuanza mapambano dhidi ya utawala wa kibeberu wa Shah.
Katika siku kama ya leo miaka 69 iliyopita, kiongozi wa taifa la India na mpigania uhuru wa nchi hiyo Mohandas Karamchand Gandhi aliuawa na kijana mmoja wa Kihindu mwenye misimamo mikali. Gandhi alizaliwa mwaka 1869 na baada ya kukamilisha masomo alitunukiwa shahada ya digrii katika taaluma ya sheria nchini Uingereza. Mohandas Gandhi kwa muda fulani pia alikuwa kiongozi wa wanamapambano wa Kihindi huko Afrika Kusini. Gandhi pia aliwaongoza wananchi wa India dhidi ya serikali ya kikoloni ya Uingereza katika kupigania ukombozi wa nchi hiyo. India ilipata uhuru mwaka 1947 chini ya uongozi wa Gandhi.
Miaka 83 iliyopita katika siku kama ya leo, kilianza kipindi cha uongozi wa Adolph Hitler, dikteta mbaguzi wa Kinazi wa Ujerumani. Chama cha Taifa cha Kisoshalisti cha Wafanyakazi wa Ujerumani ambacho kiliasisiwa na Hitler kilishinda viti 107 vya bunge katika uchaguzi wa mwaka 1930. Adolph Hitler alijitangaza kuwa kiongozi wa Ujerumani mwaka 1934 baada ya kuwa Kansela na Rais wa nchi hiyo. Hitler aliwafanya mamilioni ya wanadamu kuwa wahanga wa malengo yake ya kibaguzi. Hatua ya Adolph Hitler ya kuivamia Poland mwezi Septemba mwaka 1939 ilichochea Vita vya Pili vya Dunia na hatimaye Ujerumani na waitifaki wake walishindwa katika vita hivyo. Hitler alijiua mwaka 1945 baada ya Ujerumani kushindwa katika vita hivyo.
Siku kama ya leo miaka 128 iliyopita Ayatullah Mirza Muhammad Hassan Shirazi alitoa fatuwa maarufu ya kuharamisha tumbaku na sigara ili kuzuia uporaji uliokuwa ukifanywa na wakoloni wa Kiingereza katika nchi za Kiislamu. Fatua hiyo ilitolewa baada ya mfalme Nasiruddin Shah wa Iran kutia saini mkataba wa kuipa kampuni moja ya utawala wa kikoloni wa Uingereza mamlaka ya kuuza na kununua tumbaku nchini Iran kwa kipindi cha miaka 50. Jina la Mirza Shirazi ni mashuhuri mno kutokana na fatua hiyo ya kuharamisha tumbaku. Fatua yake hiyo ya kuharamisha tumbaku na matumizi ya sigara, bidhaa ambayo ilikuwa imehodhiwa na Uingereza, ilitoa pigo kubwa kwa ukoloni wa Uingereza nchini Iran. Vilevile fatua hiyo ilitambuliwa kuwa mapambano ya moja kwa moja dhidi ya utawala wa Shah na ukoloni wa Uingreza nchini Iran na iliandaa uwanja wa mapambano ya baadaye ya wananchi wa Iran dhidi ya dhulma, ukandamizaji na ukoloni wa wageni.
Na miaka 227 iliyopita siku kama ya leo yaani mwaka 1211 Hijiria, alifariki dunia mshairi mkubwa wa Kiislamu Sheikh Kadhim Tamimi Baghdadi, maarufu kwa jina la Uzri akiwa na umri wa miaka 80. Alikuwa msomi na mwanafasihi mkubwa na ameacha diwani ya mashairi. Miongoni mwa mshairi ya malenga huyu maarufu wa Kiislamu ni shairi maarufu la "Al Uzriya" ambalo linamsifu Mtukufu Mtume Muhammad (saw) na kizazi chake kitukufu na kubainisha misingi ya dini ya Uislamu. Shairi hilo lina zaidi ya beti 1000.