Feb 06, 2017 12:29 UTC
  • Maadhimisho ya Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sehemu ya Nane)

Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Tukiwa tunaendelea na mfululizo wa makala hizi maalumu ambazo tumekuandalieni kwa mnasaba wa maadhimisho ya Alfajiri Kumi, ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ambayo hivi sasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaadhimisha miaka 38 ya tangu kupata ushindi mapinduzi hayo matukufu ambayo yameleta mabadiliko makubwa sana ulimwengu, tunakukaribisheni katika sehemu nyingine ya mfululizo huu tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi.

Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran ambayo yana utambulisho wa kupiga vita mfumo wa kibeberu na dhulma ya aina yoyote ile, ni kikwazo kikubwa kwa madola ya kiistikbari ulimwenguni. Mara baada ya kuasisiwa kwake humu nchini, mfumo huo ulisimama imara peke yake kukabiliana na kambi mbili kubwa za Mashariki na Magharibi za wakati huo. Kipindi hicho kisicho na mfano cha Mapinduzi ya Kiislamu, ni moja ya matukufu ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo ni muhali kuingia doa.

Aidiolojia ya Mapinduzi ya Kiislamu imesimama juu ya msingi wa kupigania uadilifu na kufanikisha lengo kuu la kupambana na madola ya kiistikbari. Akiutolea ufafanuzi uhakika huo, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika moja ya hotuba zake amesema:

Katika fikra za walio wengi duniani kunaenezwa dhana kwamba, amani ni kitu kizuri, hivyo inabidi kuyapa mataifa mengine kitu hicho hata kwa kutumia nguvu. Sisi tunapinga madai hayo. Kwanza ni kweli amani ni kitu kizuri, lakini uadilifu ni bora kuliko amani. Kuna mataifa mengi sana tu ambayo kwa ajili ya kupambana na kuuangamiza ukosefu wa uadilifu, wanavuruga hali ya usalama inayokuwepo katika jamii na wanaanzisha vita. Mapinduzi na mapambano yote ya ukombozi yanatokana na jambo hilo hilo.

Mtazamo huo wa kidini na kimapinduzi; umeleta nuru ya moyo wa mapambano na fikra za kimapinduzi, si kwa taifa la Iran tu, bali kwa mataifa yote yanayopigania uadilifu duniani.

Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yameyaweka madola ya kiistikbari kwenye changamoto kubwa katika masuala mawili makubwa na muhimu sana kwenye mlingano wa nguvu. Suala la kwanza ni kwamba Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yamekuja na kaulimbiu ya kupinga kikamilifu ubeberu wa madola ya kiistikbari dhidi ya mataifa dhaifu duniani na kuthibitisha kivitendo kwamba taifa lolote linaweza kujitoa kwenye makucha ya madola ya kibeberu duniani hata likiwa mikono mitupu. Changamoto ya pili ya Mapinduzi ya Kiislamu kwa madola ya kiistikbari, ni utambulisho wa uhuru na kujitegemea wa Mapinduzi ya Kiislamu katika harakati yake inayozidi kustawi bila ya kutegemea dola lolote kati ya madola mawili makubwa wakati huo yaani wakati Mapinduzi ya Kiislamu yalipopata ushindi nchini Iran. Mara baada ya kupata ushindi humu nchini, Mapinduzi ya Kiislamu yalikuja na kaulimbiu yake maarufu inayosema: Si Mashariki, Si Magharibi, bali ni Jamhuri ya Kiislamu.

Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu)

Leo hii sisi tumesakamwa na madola makubwa duniani. Haijawahi kutokezea hata mara moja Iran kusakamwa kiasi chote hiki. Kwani huko nyuma Iran ilikuwa kama ngómbe aliyejaa maziwa, ambaye kiwele chake alikuwa amekiachilia huru kwa kila mtu kunywa maziwa yake. Lakini leo hii mambo ni kinyume kabisa na hivyo. Leo hii kutokana na mtu huyu kutaka aishi maisha yake ya heshima ya kibinadamu, anapingwa na kila mtu. Mnachopaswa kufanya ni kuendelea na njia yenu hii, kuzidi kushikamana na kuwa kitu kimoja na kutegemea wananchi wenu, kwani ni wananchi wenu ndio watakaoivua nchi kutoka kwenye kusakamwa huku kwa kila upande na maadui…

Katika upande wa kivitendo pia, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeonesha kuwa ina mambo mengi ya kuifanya iwe na nguvu kubwa huku tegemeo lake kuu likiwa ni uungaji mkono wa makundi kwa makundi ya wananchi wake.

Kwa kweli, mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, tofauti na ilivyokuwa imezoelekea kwenye milingano ya nguvu katika kipindi cha vita baridi, ulikuja na mlingano tofauti kabisa na uliokuwepo wakati huo. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikuja na fikra ya kulinda manufaa ya mataifa dhaifu na kusimama imara kukabiliana na madola ya kibeberu duniani.

Ni kwa sababu hiyo ndio maana ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran ni nukta muhimu sana katika upande wa modeli na vigezo vya mapambano ya kimapinduzi katika zama hizi.

Misingi ya mapinduzi hayo ilitoka mbali sana na kuvuruga mahesabu yote yaliyokuwa yanatolewa kuhusiana na mapinduzi mbalimbali duniani. Mapinduzi hayo ya Kiislamu hayakuwa ni uasi uliotokana na kupigania mkate wala hayakutokana na mirengo ya kikomnusti.

Aidha kamwe mapinduzi hayo hayakutegemea wala hayakuwa na muelekeo kabisa wa kutegemea mfumo wa kibepari, bali msukumo wake mkuu ulikuwa ni watu waliokuwa wanapigania kujikomboa kutoka kwenye dhulma na ubaguzi na kufanya harakati kubwa ya kupigania utawala wa kidini na matukufu ya Kiislamu na hadi leo hii mapinduzi hayo matukufu hayajaachana na shabaha yake yoyote ile. Sajjad al Musawi, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema:

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Leo hii mtu unaona harakati za wazi kabisa za Waislamu katika maeneo mbalimbali duniani ambako kwa miaka mingi Waislamu wa huko walikuwa wanakandamizwa kama vile Kashmir na nchi nyingine duniani. Lakini leo hii Waislamu wamepata fakhari kubwa. Leo hii unapowaangalia wananchi wa Palestina ndani ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu utaona kuwa kwa hakika ni watu waliosimama imara kukabiliana na ukandamizaji. Mapambano yanafanyika katika mazingira magumu, lakini bado unaona wananchi wa Palestina wanaendelea na mapambano yao. Hata taifa la Afghanistan ambalo nalo limekumbwa na matatizo mengi na hakukuwa na mtu yeyote duniani aliyejitokeza kulisaidia, lilisimama peke yake kuendesha mapambano. Hali hiyo inaonekana pia kwenye mataifa mengine duniani. Yote haya ni kutokana na kigezo yalichokipata kutoka kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Ni kwa sababu hiyo ndio maana tukio hili kubwa kwa upande mmoja limeleta wimbi la shauku, hamasa na matumaini kati ya Waislamu na mataifa ya wanyonge duniani na kwa upande wa pili limetoa changamoto nzito katika milingano ya kisiasa ya mabeberu wenye tamaa ya kuzidhibiti na kuzivunja nguvu harakati za kimapinduzi. Kwa kuwa na matukufu yasiyo na mfano, Mapinduzi ya Kiislamu kwa hakika yalivuruga mahesabu ya mfumo wa kibeberu ambao ulikuwa umeyagawa mataifa mengi ya dunia kwenye kambi mbili zenye mgongano za Mashariki na Magharibi na bila ya shaka hilo ndilo lililoyakasirisha madola ya kiistikbari ulimwenguni.

Kutokana na kuja na fikra mpya zilizochimbuka kutoka kwenye matukufu ya kidini, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yamefanikiwa kuvuka mistari yote myekundu ya siasa za kimataifa za kambi mbili na kuarifisha vigezo vipya vya kukabiliana na mfumo wa kibeberu. Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, kwa hakika uliingiza Iran kwenye mkondo mpya ambao unakinzana kikamilifu na malengo ya Marekani na madola mengine ya kiistikbari. Bi Saideh Solhi, mmoja wa wataalamu wa masuala ya kisiasa anasema:

Maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mjini Tehran

Ni jambo lisilo na shaka hata kidogo kwamba Mapinduzi ya Kiislamu ndiyo sababu kuu ya kuamka wananchi wa nchi za Kiislamu. Mimi ni mtu wa Bahrain, na nimekuwa nikifuatilia kila siku masuala ya Iran tangu yalipopata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu nchini humo na kwa kweli kuishi katika nchi kama Iran kwangu mimi ni mithili ya ndoto. Tabán sina budi kusema pia kuwa, Marekani hivi sasa imeelewa zaidi athari za kuenea na kupata nguvu mwamko wa Kiislamu na taathira za Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Hivyo Marekani inafanya njama za kuzuia kila inavyoweza na kuhakikisha kuwa Mapinduzi ya Kiislamu hayaenei, lakini uhakika usiopingika ni kwamba, ujumbe wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran unazidi kuenea na umeshatufikia.

Mpenzi msikilizaji, kilichoko hewani ni muendelezo wa vipindi maalumu tulivyokuandalieni kwa mnasaba wa maadhimisho ya miaka 38 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Miongoni mwa matunda ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ni kuliwezesha taifa la kimapinduzi la Iran kulinda heshima yake, uhuru na hadhi yake mbele ya madola ya kibeberu yanayopenda kujikumbizia kila kitu upande wao. Ni kwa sababu hiyo pia ndio maana historia ya Mapinduzi ya Kiislamu imejaa mapambano na kusimama kidete mbele ya madhihirisho yote ya dhulma na utovu wa uadilifu na mapambano hayo hayazuiliki.

Uistikbari wa dunia unaoongozwa na Marekani, tangu mwanzoni kabisa uliamua kupambana na Mapinduzi ya Kiislamu na kulifanya jambo hilo kuwa ajenda yake kuu. Ndio maana madola hayo yamekuwa yakitumia kila fursa yanayoipata kujaribu kutimiza njozi yao ya kuimaliza Jamhuri ya Kiislamu.

Katika kipindi cha miaka 38 iliyopita, Marekani imekuwa ikichukua hatua za mtawalia za kudhihirisha chuki zake dhidi ya taifa la Iran. Tabán vitendo vya kiadui vya Marekani dhidi ya taifa la Iran vilianza zamani, lakini vimeshtadi katika kipindi hiki cha karibu nusu karne ya tangu kuanzishwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.

Katika kipindi hicho chote, Marekani imedhihirisha wazi chuki na uadui wake dhidi ya taifa la Iran kutokana na kutotetereka na kusimama kwake imara kukabiliana na mabeberu. Gladio Mufa, mwanahistoria wa Italia anasema:

Mapinduzi ya kijeshi ya tarehe 19 Agosti 1953; kulibebesha taifa kubwa la Iran sheria ya capitalision kwa ajili ya kulidhalilisha taifa hilo; kuunga mkono na kutia nguvu misingi ya utawala wa kiimla wa Shah; kuendesha operesheni ya Tabas; kuweka vikwazo vya kiuchumi na mashinikizo dhidi ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu; kuichochea Iraq kuanzisha vita dhidi ya Iran; kutungua ndege ya abiria ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuendesha propaganda chafu dhidi ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, ni sehemu ndogo tu ya uadui mkubwa wa kila aina unaofanywa na Marekani dhidi ya Iran na ambao umo kwenye rekodi za historia.  

Vikwazo vya kila namna kwa karibu nusu karne sasa havijaizuia Iran kupiga hatua kubwa za maeneo ikiwa ni pamoja na kutuma satalaiti anga za mbali kwa kutegemea wataalamu wake wa ndani

Kufanya njama za mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu, ujasusi mkubwa wa ubalozi wa Marekani uliokuwepo Tehran wakati huo, kuingia kijeshi nchini Iran katika operesheni iliyofeli ya Tabas, kuiwekea Iran vikwazo vya kiuchumi, kuzuiwa mali na fedha za Iran huko Marekani, kuuruhusu utawala wa Saddam kuanzisha vita vikubwa na vya pande zote dhidi ya Iran sambamba na kuiwekea vikwazo visivyo vya kiuadilifu Iran na vile vile kuivurumishia Iran tuhuma zisizo na msingi kuhusu kadhia ya nyuklia na kuvuruga uhusiano wa Iran na nchi nyingine, kwa kweli ni sehemu ndogo tu ya chuki na uadui mkubwa uliofanywa na unaoendelea kufanywa na Marekani dhidi ya Iran.

Uadui wa Marekani dhidi ya Iran haujawahi kusita hata mara moja, bali mbinu na namna za uadui huo zinaongezeka na kuwa tata zaidi kadiri siku zinavyosonga mbele. Kwa njama na vitendo vyake hivyo vya chuki, Marekani imekuwa ikijaribu kuilazimisha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran isalimu amri mbele ya ubeberu wake. Hata hivyo taifa la Iran katika miaka yote hii ya muqawama na kusimama imara mbele ya njama za waistikbari wa dunia, haijawahi hata mara moja kuwapigia magoti mabeberu, bali inazidi kuwa imara na madhubuti zaidi mbele ya njama za madola hayo ya kinyonyaji.

Katika sehemu moja ya miongozo yake ya busara, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema:

Nara na makelele ya madola makubwa zaidi duniani leo hii, ni kupambana na Jamhuri ya Kiislamu! Madola hayo yanajidanganya kuwa yanawezi kulitia hofu taifa la Iran kwa jambo hilo. Wanatoa vitisho, lakini hawajui kuwa kwa vitisho vyao hivyo, taifa la Iran linazidi kuhisi umuhimu wa kulinda utambulisho wao. Taifa la Iran linaona namna madola khabithi zaidi, na yanayopenda dunia kupindukia, na yenye nguvu kubwa za kimaada, leo hii yanaona kikwazo chao kikuu kinachowakwamisha kufikia malengo yao maovu, ni taifa la Iran. Jambo hilo si dogo hata kidogo. Utayasikia yanasema, tumekusudia kufanya hili na lile Mashariki ya Kati, na hayo ni katika yale machache wanayoyasema; kwani makumi ya malengo yao maovu hawayasemi. Lakini taifa la Iran ni kizuizi kwao, taifa la Jamhuri ya Kiislamu ni kikwazo kikubwa kwao. Jambo hilo linazidi kuonesha adhama ya taifa hili, adhama ya mfumo huu, adhama ya utawala huu wa Kiislamu ambao umeweza kuwa kizuizi kikubwa kwa mabeberu kiasi kwamba leo hii umewazuia mabeberu wa dunia kufikia malengo yao maovu angalau katika eneo moja maalumu la kijiografia ulimwenguni.

Kusimama imara na kutotetereka taifa la Iran mbele ya mabeberu, si nara na maneno matupu, bali ni bango la matukufu ambayo taifa hili lina itikadi nayo na limefanikiwa kwa kuyategemea matukufu hayo, kusimama imara na kushinda mbele ya njama zote za maadui.

Mikakati na stratijia za Magharibi, iwe ni katika kile kipindi cha vita vilivyoanzishwa na utawala wa wakati huo wa Iraq dhidi ya Iran au baada yake, ni kutaka kulipigisha magoti taifa la Iran. Hata hivyo, muqawama na kusimama imara huko taifa la Iran kumewapa maadui wa taifa hili ujumbe ulio wazi. Kama alivyosema Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, wingi wa vitisho unaonesha nguvu na uwezo mkubwa wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, kwani kama Jamhuri ya Kiislamu isingelikuwa na nguvu kubwa za kuathiri mataifa mengine, wanaolitakia mabaya taifa la Iran kamwe wasingelichanganyikiwa kiasi chote hiki na wala wasingelianza kuchukua hatua hizi na zile kukabiliana na Jamhuri ya Kiislamu.

Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yameyaamsha mataifa ya dunia na kuyafanya yasimame kupiga vita dhulma na tawala za vibaraka wa mabeberu

 

Hivi sasa taifa la Iran linaadhimisha miaka 38 ya ushindi wa Mapinduzi yake ya Kiislamu, na hadi leo hii mapinduzi hayo matukufu yana mvuto maalumu kwa mataifa yaliyo macho na yanayopigania heshima na ukombozi.

Mapinduzi ya Kiislamu yamewaonesha walimwengu namna dini tukufu ya Kiislamu ilivyo na uwezo mkubwa wa kusimamia na kuendesha masuala ya kisiasa. Harakati ya Mwamko wa Kiislamu nayo imetokana na mataifa ya Kiislamu kupata ilhamu na somo la kupambana na ukoloni, kutoka kwa Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran.

Leo hii tunaweza kusema kwa yakini kwamba, moja ya sababu zinazoyafanya madola ya kiistikbari kuwa na woga na hofu kubwa, ni uhakika huo, yaani uwezo na nguvu za Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran za kuyaathiri mataifa mengine. Ni kwa sababu hiyo pia ndio maana maadui wanashindwa kuficha chuki zao na wanafanya njama za kila namna dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu; uadui mkubwa ambao, ulianza tangu siku za awali kabisa za ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na hauwezi kamwe kumalizika.

Noam Chomsky, mwandishi mashuhuri na mwanafikra wa Marekani

 

Noam Chomsky, mwandishi mashuhuri na mwanafikra wa Marekani anaamini kuwa, uadui wa kila namna na njama na upinzani wa kila upande wa Marekani na nchi za Magharibi dhidi ya Iran unatokana na kukataa Iran kuburuzwa na kuwa kibaraka wa mabeberu. Katika sehemu moja ya matamshi yake amesema:

Hadi pale Iran itakapoendelea kuwa huru na kutokuwa tayari kuipigia magoti Marekani, uadui na upinzani wa kila namna wa Marekani nao utaendelea kuwepo. Kwa mtazamo wa Marekani, haikubaliki kabisa kuendelea kuwepo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwani haiko tayari kufumbia macho uhuru wake.

tamati

 

Tags