Jumatatu, tarehe 13 Februari, 2017
Leo ni Jumatatu tarehe 15 Jamadil Awwal 1438 Hijria sawa na Februari 13, 2016.
Siku kama ya leo miaka 1400 iliyopita kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia, alizaliwa Imam Ali bin Hussein (AS) maarufu kwa laqabu ya Zainul Abidin katika mji mtakatifu wa Madina. Mtukufu huyo ni mwana wa Imam Hussein bin Ali Bin Abi Twalib, mjukuu wa Bwana wetu Muhammad (SAW). Alikuwa kinara wa elimu, uchamungu, wema ukarimu na upendo. Miongoni mwa sifa kuu za Imam Zainul Abidin ni kufanya ibada na kusali Swala za usiku. Alikuwa mwingi wa ibada na alipewa laqabu ya Sajjad kwa maana ya mwenye kusujudu sana na Zainul Abidin kwa maana ya 'Pambo la Wafanya Ibada' kutokana na sijda zake ndefu katika Swala. Imam Zainul Abidin alichukua jukumu la kuendeleza ujumbe wa mapambano ya Imam Hussein ya kupambana na ufisadi na dhulma ya watawala wa Bani Umayyah baada ya kuuawa baba yake katika medani ya Karbala. Aliishi miaka 35 baada ya tukio hilo chungu na aliuawa shahidi na mtawala wa Bani Ummayah Hisham bin Abdul Malik. Athari maarufu zaidi ya mtukufu huyo ni kitabu cha dua na miongozo ya Kiislamu cha al Sahifa as Sajjadiyya.

Tarehe 15 Jamadil Awwal mwaka 38 Hijria miaka 1400 iliyopita aliuawa shahidi Muhammad bin Abu Bakr ambaye alikuwa miongoni mwa maswahaba waaminifu wa Imama Ali bin Abi Twalib (as) na kamanda maarufu wa jeshi la Uislamu katika vita dhidi ya jeshi la Muawiya lililokuwa likiongozwa na Amr bin al As. Mtawala wa kizazi cha Banii Umayyah, Muawiya alituma jeshi la wapiganaji elfu sita nchini Misri kwa ajili ya kupigana na jeshi la Muhammad bin Abu Bakr lililokuwa na wapiganaji elfu mbili. Jeshi la Muhammad bin Abu Bakr lilishindwa katika vita hivyo na kiongozi huyo akauawa shahidi kwa kuchomwa moto baada ya kukamatwa mateka.
Miaka 208 iliyopita na katika siku kama ya leo, Mirza Muhammad Hassan Shirazi, mmoja wa wanazuoni na mamar'ja' mashuhuri wa Kiislamu alizaliwa katika mji wa Shiraz kusini mwa Iran. Baada ya kuhitimu masomo yake ya msingi alielekea katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq kuendeleza masomo yake ya kidini na kupata elimu kwa wanazuoni mashuhuri wa mji huo kama Sheikh Murtadha Ansari. Bidii yake kwenye masomo ilimuwezesha kukwea haraka daraja za elimu na kuwa mhadhiri na mwanazuoni wa ngazi za juu mjini hapo na katika ulimwengu mzima wa Kiislamu. Jina la Mirza Shirazi ni mashuhuri mno kutokana na fatua yake ya kuharamisha tumbaku katika kipindi cha utawala wa Nassir Deen Shah kutoka ukoo wa Qajaar. Fatuwa yake hiyo ya kuharamisha tumbaku na matumizi ya sigara, bidhaa ambayo ilikuwa imehodhiwa na Uingereza, ilitoa pigo kubwa kwa ukoloni wa Uingereza nchini Iran. Fatuwa hiyo ilichukuliwa kuwa mapambano ya moja kwa moja dhidi ya utawala wa Shah na ukoloni wa Uingreza nchini Iran. Kwa hakika iliandaa uwanja wa mapambano ya baadaye ya wananchi wa Iran dhidi ya dhulma, ukandamizaji na ukoloni wa wageni nchini.
Siku kama ya leo miaka 137 iliyopita toleo la kwanza la gazeti la al Uruwatul Wuthqaa lilichapishwa chini ya uongozi wa Sayyid Jamaluddin Asadabadi maarufu kwa jina la Jamaluddin Afghani na Sheikh Muhammad Abduh mjini Paris, Ufaransa. Sayyid Jamaluddin aliasisi Jumuiya ya al Uruwatul Wuthqaa kwa shabaha ya kutimiza lengo lake la kujenga umoja na mshikamano kati ya mataifa ya Kiislamu na akaanza kuchapisha gazeti kwa kutumia jina hilo hilo.
Gazeti hilo lilisimamishwa mwezi Dhilhija mwaka huo huo baada ya kuchapishwa kwa kipindi cha miezi kadhaa tu katika nchi za Ulaya, India, Misri, Iran na katika nchi kadhaa za Kiarabu kutokana na mashinikizo ya kisiasa ya baadhi ya nchi.
Siku kama ya leo miaka 28 iliyopita, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Imam Ruhullah Khomeini alitoa fatuwa iliyomtambua Salman Rushdie, mwandishi wa kitabu cha Aya za Shetani au Satanic Verses kuwa ameritadi na kuondoka katika dini ya Kiislamu. Katika kitabu hicho Rushdie alimvunjia heshima na kudhalilisha Mtume Muhammad (saw), kitabu kitukufu cha Qur'ani na matukufu mengine ya Kiislamu. Uandishi na uchapishaji wa kitabu hicho ulifanyika kwa njama na msaada wa nchi za Magharibi. Hata hivyo fatuwa ya Imam Khomeini dhidi ya murtadi Salman Rushdie, iliwaamsha Waislamu na kuwatahadharisha kuhusu njama hiyo. Fatuwa hiyo ya Imam iliungwa mkono na waandishi wengi huru duniani, maulamaa wa Kiislamu na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC).