Feb 16, 2017 23:40 UTC
  • Ijumaa tarehe 17 Februari, 2017

Leo ni Ijumaa 19 Jamadil Awwal 1438 Hijria sawa na Februari 17, 2017.

Tarehe 17 Februari miaka 6 iliyopita ilianza harakati ya wananchi wa Libya dhidi ya utawala wa kidikteta wa Kanali Mummar Gadafi. Libya ilikuwa nchi ya tatu kukumbwa na wimbi la mwamko wa Kiislamu na kuziangusha tawala kadhaa za kidikteta. Baada ya kuondolewa madarakani serikali ya Zainul Abidin bin Ali nchini Tunisia na ile wa dikteta wa zamani wa Misri, Husni Mubarak, wananchi wa Libya pia walianzisha harakati kubwa dhidi ya dikteta wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi. Awali Gaddafi alidhani kwamba angeweza kuzima harakati hiyo ya wananchi kwa kutumia jeshi na vyombo vya usalama na kwa msingi huo alianza kutumia mkono wa chuma na kuua wananchi waliokuwa wakiandamana. Wanachama wa shirika la kijeshi la nchi za Magharibi NATO pia walipanda mawimbi ya harakati ya mapinduzi ya wananchi wa Libya na kushambulia vituo vya kijeshi na viwanda vya Libya. Hatimaye dikteta Muammar Gaddafi aliyeitawala Libya kwa kipindi cha miongoni minne kwa mkono wa chuma aliondolewa madarakani kwa madhila na kuuawa kwa kudhalilishwa na kisha akazikwa sehemu isiyojulikana.

Mapinduzi ya watu wa Libya

Siku kama ya leo miaka 208 iliyopita, vilimalizika vita vya umwagaji damu vya Zaragoza vilivyopiganwa kati ya wanajeshi wa Ufaransa na wale wa Uhispania, huku Ufaransa ikipata ushindi na kuukalia kwa mabavu mji wa Zaragoza ulioko mashariki mwa Uhispania. Vita hivyo vilianza Novemba 15 mwaka 1808, kufuatia uvamizi wa jeshi la Napoleon.

Siku kama ya leo miaka 190 iliyopita, aliaga dunia Johann Heinrich Pestalozzi, msomi wa Uswisi na mmoja wa walimu mashuhuri. Pestalozzi alikuwa mjuzi wa elimu nyingi hasa hisabati na tiba na alizungumza lugha kadhaa za kimataifa. Msomi huyo wa Uswisi alikuwa na mtindo wake makhsusi wa kufundishia ambapo aliweza kutoa mafunzo ya masuala mbalimbali kwa watoto kwa wakati mmoja.

Johann Heinrich Pestalozzi

Na siku kama ya leo miaka 527 iliyopita Abulfadhl Abdulrahman Suyuti, mashuhuri kwa lakabu ya Jalaluddin, faqihi, mpokezi wa hadithi na mtaalamu maarufu wa lugha wa zama hizo alifariki dunia mjini Cairo. Jalaluddin Suyuti alizaliwa mwaka 849 Hijria na alihifadhi Qur'ani Tukufu akiwa kijana. Abulfadhl Abdulrahman Suyuti kwa miaka kadhaa alijifunza masomo ya fiqih, hadithi, tafsiri ya Qur'ani na lugha na kupata mafanikio makubwa. Msomi huyo wa Cairo ameandika vitabu vingi vya thamani na miongoni mwavyo ni "Al Iqtirah", "Al Kitabul Kabir" na "Tarikhul Khulafaa".

ابوالفضل عبدالرحمان سیوطی