Mar 20, 2017 03:03 UTC
  • Jumatatu, 20 Machi, 2017

Leo ni Jumatatu tarehe 21 Jamadithani 1438 Hijria sawa na 20 Machi, 2017

Miaka 61 iliyopita katika siku kama ya leo muwafaka na tarehe 20 Machi 1956, nchi ya Tunisia iliyoko katika eneo la kaskazini mwa Afrika ilijipatia uhuru wake kutoka kwa mkoloni Mfaransa. Ijapokuwa harakati za ukombozi nchini humo zilianza baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia, lakini kutokea Vita vya Pili vya Dunia na kudhoofika Ufaransa kwenye vita hivyo, kuliandaa mazingira mazuri ya kujikomboa nchi hiyo. Baada ya kujipatia uhuru, Habib Bourguiba aliongoza nchi hiyo, kwa karibu miongo mitatu lakini kwa mabavu na ukandamizaji. Baada ya utawala wa Bourguiba, nchi hiyo ilitawaliwa na Zainul Abidin Ben Ali ambaye aliingia madarakani mwaka 1982. Kiongozi huyo naye alifuata mbinu na mwendo uleule wa Bourguiba wa kuwakandamiza wananchi na kupiga vita Uislamu, suala lililopelekea wananchi wa nchi hiyo kusimama kidete na kumng'oa madarakani mwezi Januari mwaka 2011.

Bendera ya Tunisia

Tarehe 20 Machi miaka 290 iliyopita, alifariki dunia Isaac Newton mwanafizikia, mwanahisabati na mwanafikra wa Kiingereza akiwa na umri wa miaka 84. Alizaliwa mwaka 1643 na kusoma katika Chuo Kikuu cha Cambridge. Akiwa na umri wa miaka 24, Isaac Newton alifanikiwa kugundua kanuni muhimu ya makanika. Newton alibainisha pia sheria tatu za mwendo yaani (Three laws of motion) katika kitabu chake alichokipa jina la Mathematical Principles of Natural Philosophy.

Isaac Newton

Na miaka 1054 iliyopita, aliaga dunia Muhsin bin Ali Tanukhi mwandishi na mwanahistoria mashuhuri wa Kiislamu akiwa na miaka 55. Muhsin Tanukhi alikuwa na kipawa cha hali ya juu katika nyanja za mashairi na lugha ambapo aliweza kutunga mashairi mengi. Muhsin bin Ali Tanukhi katika kipindi kifupi alijifunza masomo ya dini na mengineyo ya zama hizo na baadaye akaanza kujishughulisha na kazi ya uwakili. Kitabu cha msomi huyo wa Kiislamu alichokipa jina la al-Faraj Ba'da al-Shidda ni mkusanyiko wa matukio ya kihistoria na kijamii yaliyojiri katika zama hizo ambayo aliyaandika kwa umakini mkubwa.